Serikali imeombwa kujenga mfumo mzuri utakaowawezesha vijana kujiunga katika vikundi vya uzalishaji ili wawe na uwezo wa kukopesheka katika taasisi zinazotoa mikopo na kujiajiri katika miradi ya kilimo.
Akizungumza na JAMHURI Mkuu wa kitengo cha utafiti wa taasisi ya Well Told Story Dk Anastasia Mirzoyants amesema kutokana na ukosefu wa ajira nchini na duniani kote kuna haja taifa kuelekeza nguvu katika kilimo, maana ni sekta pekee inayozalisha ajira nyingi kwa vijana.

“Sote ni mashuhuda duniani, hali ya uchumi siyo nzuri kila mahali makampuni yanapunguza wafanyakazi ajira pekee iliyobaki ni kilimo na kwa bahati Tanzania bado tuna ardhi ya kutosha,” amesema Mirzoyant.
Amesema katika utafiti uliofanyika mwaka 2016 na kuupa jina la Shujaa 360Tz ulifanyika kwa vijana kwa asilimia 23 ulionyesha kati ya vijana 9 na 10 walio hojiwa walisema wanajihusisha na kilimo kwa kuwa wanatoka katika familia za kilimo.
“Ni jukumu la Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kuhakikisha taifa linajitosheleza kwa chakula lakini wadau wengine wa kilimo wanajukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya nini kifanyike kulisaidia taifa kukuza kilimo,” amesema Dk Anastasia.

Amesema ni wajibu wa Serikali kuchukua hatua za makusudi kuwafumbua vijana akili juu ya kujua umuhimu wa kushiriki katika kilimo kama njia ya kujikomboa na kuachana na umasikini.
Amesema ni wajibu wa Serikali pia kuratibu na kujenga utamaduni wa kuendesha tafiti kuhusu mazao, mifugo, uchumi wa jamii, kilimo cha misitu, udhibiti wa udongo, maji na uhandishi wa kilimo cha kisasa.
“Vijana wanapaswa kuachana na dhana ya kusubiri ajira toka serikalini badala yake waangalie namna ya kujiajiri katika sekta ya kilimo ambako bado kuna nafasi ya kutosha ya kujiajiri,” amesema Dk Anastasia.
Dk Mirzoyants amesema katika miaka ya hivi karibuni sekta ya Kilimo imeendelea kuwa muhimu katika uchumi na maendeleo ya nchi kwa kuwa inatoa ajira kwa asilimia 65.5 na kuchangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini.

Amesema kuanzia 2015 sekta ya kilimo ilichangia asilimia 29 ya pato la taifa ikilinganishwa na asilimia 28.8 mwaka 2014 ambacho ni kiashiria kuwa endapo nguvu zitaelekezwa huko taifa linaweza kunufaika.
Mtayarishaji wa maudhui wa taasisi hiyo Allan Lucy amesema utafiti huo uliojikita katika sekta ya kilimo umebaini changamoto nyingi zinazo wakabili vijana wengi wanaojihusisha na kilimo hasa vijijini.
Amesema katika utafiti wao wametoa ushauri kwa serikali kuangalia jinsi ya kuweza kutoa hamasa kwa vijana wasomi kuungana katika makundi na kuanzisha kilimo cha kisasa
“Katika kufikia malengo Benki za hapa nchini hazina budi kuangalia upya juu ya sera zao na kuangalia utaratibu wa kuweza kutoa mikopo kwa vijana ambao wameanzisha makundi ya kilimo na ufugaji,” amesema Lucy.
Katika hotuba yake Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Dk Charles Tizeba juu ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2017/2018 amesema Wizara kupitia kikosi kazi cha kitaifa cha kuendeleza kilimo hifadhi imeandaa kijitabu, bango na vipeperushi kwa ajili ya kutoa elimu na namna ya kuanzisha kilimo hifadhi.

Amesema Wizara kwa kushirikiana na mtandao wa kilimo hifadhi Africa cha (Africa conservation Tillage Network – ACTN) imetoa mafunzo kwa wakulima wakufunzi 130 watakaofundisha kuhusu Kilimo Hifadhi.
Amesema mafunzo hayo yamefanyika katika Wilaya 13 za Sumbawanga, Momba, Mbozi, Mbeya Vijijini, Kyela, Mbarali, Kilolo, Ludewa, Songea Vijijini, Namtumbo, Chamwino, Kongwa na Chemba. Wakulima wakufunzi 100 wamepewa baiskeli kuwarahisishia usafiri waweze kutoa huduma za ugani.

3389 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!