WAKILI ALIYEMUAPISHA RAILA ODINGA AZUHIRIWA UWANJA WA NDEGE

Bw Miguna

Wakili wa upinzani aliyeidhinisha kiapo cha Bw Raila Odinga alipokuwa anajiapisha kuwa ‘Rais wa Wananchi’ mwezi Januari bado amekwama katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi.

Bw Miguna Miguna alijaribu kurejea Kenya Jumatatu lakini akazuiwa kuingia baada yake kudaiwa kutowasilisha pasipoti ya Canada ambayo ilitumiwa kumsafirisha kwa nguvu hadi Canada.

Wakili huyo alisisitiza kwamba ni raia wa Kenya na hafai kuzuiwa kurejea.

Taarifa zinasema Bw Miguna, ambaye pasipoti yake ya Kenya ilitwaliwa na polisi kabla ya kuondolewa kwake Kenya mwezi jana, alikuwa ametakiwa kuwasilisha ombi la kupata visa ya kukaa Kenya kwa miezi sita kwa kutumia pasipoti hiyo yake ya Canada.

Alikataa jaribio hilo na badala yake kutoa kitambulisho chake cha taifa kuonesha kwamba yeye ni Mkenya na kutaka aruhusiwe kuingia.

Bw Miguna, aliyekuwa amewasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mwendo wa saa nane adhuhuri, alikesha kwenye uwanja huo.

Maafisa walijaribu kumsafirisha kutoka uwanja huo kwa kutumia ndege ya shirika la Emirates ambayo ilikuwa inaelekea Canada kupitia Dubai.

Wakili wa upinzani James Orengo, seneta ambaye majuzi alichaguliwa kuwa kiongozi wa upinzani Bunge la Seneti, ameambia Reuters kwamba maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia ndio waliojaribu kumlazimisha Bw Miguna kupanda ndege hiyo iliyokuwa inaondoka.

Lakini wakili huyo alikataa kuingia ndani ya ndege hiyo na mtafaruku ukazuka.

Video iliyopeperushwa moja kwa moja na runinga ya kibinafsi ya Citizen ilimuonesha Bw Miguna akiwa kwenye lango la ndege akiwaambia wahudumu: “Siendi popote, hamuwezi kuniondoa kutoka kwa nchi yangu kwa nguvu.”

Bw Orengo ameambia Reuters kwamba maafisa hao wa polisi baadaye walimuondoa mwanasiasa huyo kutoka kwenye ndege hiyo na kumzuilia kwa muda katika afisi za uhamiaji katika uwanja huo wa JKIA.

Baadaye asubuhi, walimhamishia kituo cha polisi cha uwanja huo na kuendelea kumzuilia.

Bw Odinga alikuwa amefika uwanjani humo Jumatatu usiku kujaribu kutatua mzozo huo.

Kwa mujibu wa Bw Orengo, Bw Odinga alikuwa ametoa wito kwa serikali kumrejeshea Miguna pasipoti yake ya Kenya.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Uhamiaji mapema Jumanne ilisema Bw Miguna alianza “kuzua fujo na kulalamika” uwanja wa ndege na kwamba alikuwa anataka kuruhusiwa kuingia Kenya bila kuidhinishwa na maafisa wa uhamiaji.

Wizara hiyo imesema inafanikisha utaratibu wa kumuwezesha Bw Miguna kuwasilisha tena ombi la kuwa raia wa Kenya.

Taarifa ya wizara hiyo ilisema fomu za kuwasilisha maombi hayo zimetumwa uwanja wa Ndege.

Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Joseph Munywoki kwenye taarifa alisema: “Badala ya kuonesha hati za kusafiria alizotumia kwenda Canada, Miguna alianza kuzua fujo na kulalamika akisema kwamba yeye ni Mkenya na anafaa kuruhusiwa kuingia Kenya bila kupitia kwa meza ya idara ya uhamiaji kama inavyotakiwa kwa abiria wote wanaowasili bila kujali uraia wao.”

“Hatujamzuia kuingia Kenya, tunamtaka tu afuate utaratibu kama watu wengine wote,” msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani

Mwenda Njoka aliambia Reuters kwa njia ya simu

 

821 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons