Wakubwa wanavyotafuna Bandari

*Waanzisha EPA mpya, Bandari waitengea CCM bilioni 10
*Kinana aukana mradi, walipanga kujenga yadi ya malori
*Dk. Mwakyembe ampa onyo Kipande, agoma kuhojiwa
*Ikulu yakana kumlinda, wakili adai milioni 205/- kwa siku
*Mkurugenzi anyanyasa wanawake, Bodi ‘imewapotezea’
*Wataalamu waacha kazi TPA, Magesa akiri hakuna ulinzi

Utaratibu wa baadhi ya wanasiasa kuchota mabilioni ya shilingi kutoka kwenye Hazina ya Taifa kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu umeendelea.
Wakati mwaka 2005 zilitumika kampuni kama Kagoda, Deep Green na nyingine kuchota mabilioni ya EPA, zamu hii Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wameanzisha mradi kama huo kwa ajili ya mwaka 2015, ambapo wameitengea CCM Sh bilioni 10 kwa ajili ya mradi wa kuegesha magari.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Bandari, ambazo gazeti JAMHURI limezithibitisha, bajeti ya Mamlaka ya Bandari inaonesha kuwa wajanja wametumia kampuni tanzu ya CCM (SUKITA) Sh bilioni 10 kama kianzio kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya mradi wa kuegesha malori.
Mradi huu umeingizwa kiujanja kupitia Kampuni ya Lori Parking Yard kwenye Bonde la Msimbazi, eneo la Tabata Matumbi yaliko majengo ya SUKITA. JAMHURI imeshuhudia pilikapilika za ujenzi katika eneo hilo.
“Huwezi kuamini, huu ni mradi hewa. Wanatafuta fedha za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Kwenye bajeti ya 2014/2015 wanasema kiasi cha Sh bilioni 10 kilichotengwa ni cha kuanzia. Mwakani kitatengwa kiasi kikubwa zaidi. Lakini ukiangalia uhalisia, hata kama kweli wangekuwa wanajenga maegesho ya malori, eneo hili haliruhusu uwepo wa maegesho haya.
“Pale Tabata ni katikati ya jiji kwa sasa, tuna msongamano mkubwa wa magari kuelekea kwenye makutano ya Ubungo, leo unasema unaweka yadi ya kuegesha malori Tabata! Utatengeneza msongamano wa kiasi gani? Kama ni yadi ya malori ilipaswa kujengwa hata nje ya Kibaha kuelekea karibu na Mlandizi, ila si katikati ya jiji. Lakini tunaojua, tunasema wajinga ndiyo waliwao. Ni mradi wa uchaguzi,” kilisema chanzo chetu.
Kinana aukana mradi wa malori
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipoulizwa juu ya kuwapo kwa mpango huo wa kuchota Sh bilioni 10 kutoka bandarini, alijibu kwa ufupi hivi: “Sina taarifa wala sijawahi kuusikia [mpango huo]. Jihadhari na taarifa hizo.”
Hatua ya Kinana kukana kuufahamu mradi huo imeibua hisia kuwa huenda baadhi ya watu wanatumia jina la CCM, au CCM wenyewe wameanza kuchota mabilioni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani. Zipo taarifa za uhakika kuwa mkataba kwa ajili ya mradi huu umetiwa saini mwishoni mwa mwaka jana.
Katika hali inayofanana na hiyo, inaelezwa kuwa Madeni Kipande kwa nia ya kumzawadia Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, bila kufuata utaratibu wa kibajeti, ametenga Sh milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa rest house(nyumba ya kupumzikia) huko Matema Beach, kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa, jimboni Kyela.
“Unajiuliza ni mapato gani yanatokana na Matema Beach kama si kumfurahisha waziri jimboni kwake? Ukiangalia vitabu vya uhasibu vya Mamlaka ya Bandari, huwezi kukuta mahala popote ambapo Bandari ya Matema ambayo kimsingi wala si bandari ni mwalo, imepata kuingiza hata Sh 100,000 kwa wiki.
“Unajiuliza katika nchi hii zipo bandari ngapi hadi hii tu ndiyo isiyoingiza hata senti tano kwenye pato la Bandari ndiyo itengewe bajeti ya Sh milioni 400 kujengewa rest house? Tena kibaya zaidi, wamekwenda kwenye huo mwalo wa Matema wakakuta kuna wamiliki halali wa ardhi ambao si Serikali.
“Katika kutaharuki, wamejikuta sasa hawana mwelekeo. Waziri ndiyo yupo anafanya kazi ya ziada kuhakikisha anapata ardhi na hati ya kiwanja aweze kupata kibali cha kujenga hiyo rest house. Kuna kila dalili kuwa katika mwaka huu wa fedha hizi fedha hazitatumika maana muda umeisha na ardhi ya kuenga hiyo rest house haijapatikana,” kilisema chanzo chetu kingine.
Ujumbe wa mwisho kwa Dk. Mwakyembe mwishoni mwa wiki uliomtaka kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma hizi na nyingine, aliotumiwa na hakuujibu ulisema hivi: “Dk. Mwakyembe shikamoo. Naomba comment yako, maana nakupigia simu inaita tu. Madeni Kipande ametenga Sh bilioni 10 kwa ajili ya mradi hewa wa malori SUKITA – CCM, Sh milioni 400 kwa ujenzi wa rest house Matema Beach bila kufuata taratibu na hakuna ardhi.
“Kakudanganya kuwa bandari inakusanya Sh bilioni 50 kwa mwezi, wakati si kweli. Wafanyakazi watatu wamefariki bandarini kutokana na vitisho anavyowapa akidai hakuogopi hata wewe. Je, huoni Kipande anastahili kukemewa kwa atendayo? Asante – Balile.” Dk. Mwakyembe hakujibu ujumbe huu.
Waziri Dk. Mwakyembe kwa zaidi ya miezi mitatu sasa hapokei simu wala kujibu ujumbe unaotumwa kwake na hata waandishi wetu walipokwenda ofisini kwake kuomba miadi na kuacha maswali, hayakuwahi kujibiwa.
Saa chache kabla ya kwenda mtamboni, Dk. Mwakyembe alijibu kwa ujumbe mfupi, akisema: “Ulishamhukumu [Kipande] tayari bila kutuuliza. Endelea tu.”
Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Joseph Msambichaka, naye alipelekewa maswali kwa njia ya barua pepe, lakini kama alivyofanya Dk. Mwakyembe, hakujibu barua pepe hiyo wala kupokea simu za mwandishi wa habari hizi.
Dk. Mwakyembe ampa onyo Kipande
Kutokana na mchezo wa ulaji fedha, Juni 11, 2013 Dk. Harrison Mwakyembe, kupitia barua yenye Kumb. Na. CCB 364/505/01 alimwandikia barua ya onyo, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Madeni Juma Kipande, kutokana na kukaidi agizo lake.
Agizo la Dk. Mwakyembe lilitokana na Kipande kuwapa “upendeleo maalum” au kuibeba kampuni ya magari ya Silver, hata baada ya Waziri Dk. Mwakyembe kuzuia utaratibu huu uliodhaniwa kutumika kutokana na shinikizo maalum.
Barua ya Dk. Mwakyembe iliyokuwa na aya tatu ilisema hivi: “Nimefedheheshwa sana na taarifa kuwa kampuni ya kuhifadhi magari ya Silver bado inapewa “preferential treatment” au inabebwa na TPA tofauti na kampuni nyingine za aina hiyo, na kinyume kabisa na taratibu za ushindani wa kibiashara na maelekezo niliyoyatoa mbele yenu, viongozi wa wizara na wawakilishi wa ICDVs tarehe 5 Machi, 2013.
Kwa staili hii ya uongozi, hatutafika!
Sitisheni “preferential treatment” kwa Silver ‘asap’ na nipatie taarifa ya utekelezaji tarehe 15 Juni, 2013 bila kukosa.
Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb)
Waziri wa Uchukuzi
Nakala kwa: Prof. Joseph Msambichaka,
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi,
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari,
Dar es Salaam
Ikulu yasema haimlindi Kipande
Ofisi ya Rais Ikulu kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, imetoa tamko rasmi kuwa haina mpango wa kumkingia kifua Kipande, kutokana na matendo yake, au mtumishi yeyote wa Ikulu haruhusiwi kumkingia kifua mtu anayeharibu utendaji.
“Ikulu haikingii mtu yeyote kifua. Hawezi kufanya mambo yake ovyo akasema ana kinga ya Ikulu,” alisema Balozi Sefue na kuongeza kuwa Mamlaka ya Bandari ina Bodi ya Wakurugenzi na waziri mwenye dhamana na masuala ya uchukuzi, ambao wanapaswa kuhakikisha kuwa utendaji unakwenda kwa mujibu wa sheria.
Balozi Sefue aliahidi kulifuatilia suala hilo kubaini uhalisia wa kinachoendelea.
Katika toleo la wiki iliyopita, JAMHURI ilichapisha habari zenye kuonesha kuwa Kipande anajidai kuwa na kinga ya Ofisi ya Rais Ikulu, huku akidaiwa kuwatisha baadhi ya watu walioko karibu naye kuwa yeye ni mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Rais Kikwete hahusiki na ubabe anaofanya Kipande, bali anapata kinga kutoka kwa Kassim Mtawa, ambaye ni Msaidizi Binafsi wa Rais Kikwete, akishirikiana na Mnikulu Gurumo, ambao wamekuwa wakimhakikishia usalama wake kwa kuwa wanatoka pamoja Bagamoyo.
Kipande anatumia udugu wa Mtawa, ambaye ni mjomba wa damu wa Rais Kikwete, kujihalalishia matendo ya kibabe anayoyafanya kila sehemu ya kazi aendako. Gurumo na Mtawa wanampa kiburi Kipande bila baraka za Rais Kikwete, uchunguzi umethibitisha.
Wakili adai alipwe milioni 205 kwa siku
Wakati hayo yakiendelea, Afisa Sheria Mwandamizi wa TPA, Erasto Rugenge, amesimamishwa kazi miezi minane hadi sasa baada ya kufanyia kazi maelekezo aliyopewa na Madeni Kipande.
Rugenge alisimamishwa kazi tarehe 3/9/2013 kwa tuhuma alizoandikiwa kwenye barua yake zikisema: “Wewe ukiwa kama Afisa Mwandamizi wa Huduma za Sheria ulishindwa kuishauri Mamlaka katika mikataba ifuatayo: Mkataba wa CCCC (China Communications Construction Company) iliyokuwa imepewa zabuni ya kujenga gati No 13 na 14 pamoja na shauri la Oryx Company Limited. Kwa hiyo, tunakusimamisha ili kupisha uchunguzi wa masuala hayo.
“Katika kipindi chote hutatakiwa kusafiri nje ya Mkoa wa Dar es Salaam ili kuruhusu Kamati ya Uchunguzi iweze kukupata pale ambapo watadhani wanakuhitaji. Kipindi chote utaendelea kupokea mshahara wako na staili zako zote.”
Leo ni miezi minane tangu Rugenge asimamishwe kazi, hajaandikiwa barua ya kujieleza au kushtakiwa wakati msururu wa watu aliowasimamisha kazi Kipande wote wameishapewa barua za kujieleza.
Kilichotokea CCCC ambayo ni kampuni ya Kichina iliyokuwa imepewa zabuni ya kujenga gati Na 13 na 14 ni kichekesho. Iliomba zabuni na TPA wakaonesha nia ya kuwapa zabuni hiyo. Baadaye ilibainika kuwa Benki ya Dunia ilikuwa imezuia kampuni hii kupewa zabuni kutokana na kudaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa visivyokubalika kwa mujibu wa vigezo vya Benki ya Dunia.
Kampuni hii kwa kutumia kampuni ya Rweyongeza Limited, walifungua kesi Mahakama Kuu kuomba Bandari isimpe zabuni mtu mwingine yeyote, kwani wao ndiyo waliokuwa washindi halali. Bandari kwa upande wake ina mkataba wa huduma za kisheria na Kampuni ya Trust Mark Attorneys.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Bandari, Kokutulage Kazaura, aliiandikia kampuni ya Rweyongeza Ltd iandae utetezi (WSD) kuitetea TPA.
Siku ya kutajwa kwa kesi hiyo, mawakili wa CCCC wakaieleza Mahakama kuwa mteja wao ambaye ni CCCC anataka kuondoa kesi yake. Kutokana na ombi hilo, Jaji Bukuku akauliza upande wa mlalamikiwa iwapo hauna pingamizi kuondoa mashtaka mahakamani.
Mawakili wa TPA walisema hawana pingamizi, ila kwa mujibu wa sheria ya uwakili, walisema mteja wao ametumia gharama, zilipwe. Iwapo wasingeomba gharama za kesi wakati wa ukaguzi lingekuwa tatizo kuwa kesi iliishaje.
Kumbe nyuma ya pazi, Wizara ya Ujenzi ilikuwa imezungumza na Ubalozi wa China wakakubaliana kampuni yao iondoe kesi, lakini Kipande pamoja na kwamba alikuwa na taarifa hizo, hakupata kuiambia Idara ya Sheria kuwa kesi hiyo ingeondolewa. Pia, Kipande hakufahamu kuwa kuondoa kesi mahakamani bila kudai fidia kungeleta shida katika ukaguzi wa hesabu (audit query).
“Kilichotokea kilikuwa kichekesho. Pamoja na kwamba mteja amejitoa kwenye kesi, na huyu mteja CCCC angelipa gharama zingeingia kwenye akaunti ya TPA, Kipande akasema, tena kwa maandishi, kuwa Rugenge amefanya kituko kuomba gharama za kesi mahakamani. Kwa minajili hiyo akaagiza aondolewe kwenye idara hiyo.
“Mkuu wa Idara, Koku, akamwendea Kipande akamweleza kuwa Rugenge hakufanya kosa lolote. Sheria ya Uwakili inataka hivyo kwa mteja anayeondoa kesi kulipa gharama za mawakili na fidia nyingine ikiwamo usumbufu. Baada ya maelezo hayo, Kipande akakaa kimya na hivyo Rugenge akabaki ofisini bila kuguswa,” kilisema chanzo chetu kingine.
Kuhusu kesi ya Oryx; kampuni hii ilikuwa inaagiza mafuta ya kusafirisha kwenda nje ya nchi. Siku za nyuma waliwahi kupewa kibali cha miezi sita, lakini baadaye ikadaiwa kuwa mafuta inayoagiza kampuni hii yanauzwa kwenye soko la ndani hayapelekwi nje. Ilipofahamika hivyo, TPA wakawafutia kibali. Wakaanza kuwatoza kodi kama kawaida.
Kampuni ya Oryx ikafungua kesi kupinga uamuzi huu na ikadai fidia ya mabilioni. Idara ya Sheria ilimwandikia Kipande (nakala tunayo) ikimuomba ushauri iwapo kesi hiyo waipeleke kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, au kwa kampuni ya Trust Mark Attorneys ambayo wana mkataba nayo wa kutoa huduma za kisheria.
“Kama unavyoona Kipande aliandika hapa akaelekeza kuwa ‘mwandikie Katibu wa Waziri, A. Mwingira, apendekeze nioption gani tuitumie’. Mwingira akamteua mtu mmoja anaitwa Mpare Mpoki, kinyume na taratibu za ununuzi lakini. Rugenge kwa upande wake alikuwa ameishajibu na kupeleka mahakamani utetezi wa TPA, ndipo Mwingira akajibu kuwa apewe Mpoki.
“Huwezi kuamini. Siku ya kwanza tu, Mpoki alipokwenda mahakamani kwa ajili ya kesi hii kutajwa, walalamikaji wakajitoa. Hii ina maana wakili huyu alifanya kazi kwa dakika zisizozidi 10, lakini baadaye akaleta fee note ya dola 126,000 za Marekani (Sh milioni 205) akitaka alipwe kwa kazi ya kesi hiyo. Uhalisia, kampuni ile iliyoingia mkataba na TPA kutoa huduma za kisheria inalipwa Sh 4,500,000 kwa kesi za kawaida na 7,500,000 kwa kesi serious,” kilisema chanzo chetu kingine.
Hata hivyo, Kipande aliyeelekeza Mwingira, ambaye ni Katibu wa Waziri Dk. Mwakyembe, ndiye ateue wakili wa kusimamia kesi hiyo, akamgeuzia kibao Rugenge na kudai kuwa alimpa Mpoki ushauri adai fedha nyingi, hivyo akaelekezwa afukuzwe kazi, lakini Rugenge akaishia kusimamishwa.
JAMHURI ilipowasiliana na Rugenge, alisema kwa sasa hayuko kwenye nafasi ya kulizungumzia suala hilo, ingawa alikiri kuwa lipo na akaomba mwandishi awasiliane na Kipande au Kazaura kuepusha kuingilia taratibu za uchunguzi kama zipo. Miezi minane sasa anapata mshahara na marupurupu mengine bila kufanya kazi wala kushtakiwa iwapo ana kosa kwa mujibu wa Kipande.
Juhudi za kumpata Mpoki ili kupata ukweli huo ziligonga mwamba lakini bado JAMHURI inaendelea kumtafuta.
Kipande adaiwa kunyanyasa wanawake
Uchunguzi wa Gazeti JAMHURI umebaini kuwa Kipande ni kinara wa kudharau wanawake na haamini kama mwanamke anaweza kuwa kiongozi. Ni kutokana na hali hiyo, baada ya kufanikisha uvunjaji wa Bodi ya Wakurugenzi iliyoteuliwa mara tu yalipofanyika mabadiliko ya uongozi bandarini, alihakikisha hakuna mwanamke anayeingia katika Bodi ya Wakurugenzi.
Bodi aliyoivunja Dk. Mwakyembe baada ya kuwapo tuhuma kuwa inavujisha siri za Bandari kwenye vyombo vya habari, ilikuwa na wanawake watatu ambao ni Caroline Kavishe, anayefanya kazi Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Asha Nassoro anayefanya kazi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Dk. Hilderbrand Shayo wa Open University of Tanzania (OUT).
Wakurugenzi wengine walioondolewa kwa fitina za Kipande kuwa walikuwa wafuasi wa Chadema na ni kabila moja la Wachagga ni John Ulanga wa Civic Right Forum, Dk. Jabir Bakari, anayesimamia mpango wa e-Government na Eng. Julius Mamilo wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC).
Baada ya kujihakikishia kuwa wanawake wameondolewa kwenye Bodi, alimshinikiza Waziri Dk. Mwakyembe akateua wanaume tu, walioungana na Profesa Msambichaka, ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya. Pamoja na Prof. Msambichaka, wengine kwenye Bodi sasa ni Said Sauko, ambaye ni Naibu Mkurugenzi Tazara na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia.
Pia wamo Jaffer Machano, Meneja TIB, Eng. Amani Kisamfu, Mkurugenzi Mkuu wa TRL na Edmund Njowoka, ambaye ni mfanyakazi wa kawaida wa TPA, ila ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Bandarini Tanzania (DOWUTA).
Ukiacha unyanyasaji huo wa Bodi ya TPA kutokuwa na mwanamke hata mmoja, viongozi wengi wanawake waliopo TPA, Kipande kwenye mikutano mingi huwaita vihiyo, huwafokea wanawake hao, ambao wengi huishia kulia kwa uchungu mbele yake. “Wakilia tu mbele yake, basi Kipande hufurahi mno. Wale wanawake anaowafokea hawalii, anatangaza kuwa atawang’oa kazini,” kilisema chanzo chetu.
Orodha ifuatayo ni ya wanawake ambao wamepata kusulubiwa na Kipande katika unyanyasaji wa aina yake. Hawa ni Prediganda Assenga, Rukia Shamte, Apolonia Mosha, Fransisca Muindi, Kokutulage Kazaura, Adelaide Lukaija, Janet Ngowi, Vulfrida Teye, Winnie Mulindwa, Florence Nkya, Maimuna Mrisha, Levina Kato, Beatrice Jairo na wengine wengi. Vielelezo hadi barua za malalamiko kwenye Bodi ya Wakurugenzi vipo.
Wafanyakazi mahiri waacha kazi TPA
Idadi kubwa ya maafisa na watendaji wenye weledi na elimu ya kutosha, wameamua ama kustaafu kabla ya kufikisha umri wa miaka 60 au wametafuta kazi sehemu nyingine kutokana na manyanyaso ya Kipande. Hata hivyo, inaelezwa kuwa azma ya Mzee Kipande (58) ni kuondoa mameneja wote waliopata kufanya kazi chini ya Ephraim Mgawe, Mkurugenzi Mkuu aliyeondolewa na Dk. Mwakyembe.
Mara kwa mara Kipande amekuwa akisema kuwa anayo orodha ya watu 100 aliowaandaa kuchukua nafasi za wakurugenzi na mameneja atakaowaondoa. Mbinu anayotumia kuwachanganya akili mameneja na wakurugenzi ni kuwanyima uhuru wa kufanya kazi, kuwadhalilisha kwenye Bodi ya TPA, kuwapeleka Takukuru kwa tuhuma hewa, kuwanyima fursa za kujiendeleza kazini, kuwahamisha, kuwashusha vyeo na kuwakashifu mbele ya kadamnasi na wafanyakazi kuwa ni wabadhirifu na wezi.
Kutokana na unyanyasaji huu, orodha ya watumishi wanaoomba kustaafu mapema imezidi kuongezeka siku hadi siku. Wataalamu 13 hadi mwishoni mwa wiki walikuwa wameomba kustaafu wakiwa na umri kati ya miaka 55 na kabla ya kufikisha 60.
Walioomba kustaafu ni Winnie Mlindwa, Meneja Msaidizi wa Bandari ya Dar es Salaam (Uendeshaji), Kapteni Juma Sayire aliyekuwa Habour Master, Anthony Masawe aliyekuwa Meneja Udhibiti, Ephraim Magula (Principle Marine Engineer), Nusura Othuman (Principle Procurement Officer), Msechu (Principle Internal Auditor), Piece Mteketa (Office Management Secretary), Raymond Simon (Senior Technician), Veronica Katumba (Assistant Operations Officer), Ayubu Msangi (Computer Operator), Yasinta Mango (Finance Officer), Monica Lema (Office Management Secretary) na Adelaida Lukaija (Procurement Officer).
Hawa wote wameomba kustaafu kutokana na kukerwa na tabia ya Kipande ya kuburuza watu badala ya kuongoza sawa na alivyopata kuambiwa na Profesa Msambichaka.
Magesa akiri kamera za CCTV hazifanyi kazi
Mkurugenzi wa ICT, Phares Magesa, Februari 18, 2014 alihojiana na JAMHURI, ambapo alithibitisha karibu kila kitu kuhusu upungufu uliopo bandarini, ila akakanusha suala kwamba watu walioomba nafasi pamoja naye ya ukurugenzi wa ICT hawasumbuliwi.
“Watu walioomba nafasi au kuonesha nia si kweli kuwa niliwatishia. Taratibu za kuomba nafasi ziko wazi na zinasimamiwa na taratibu za kisheria watu wote wana haki sawa za kuomba, mimi si ninayefanya shorlisting kwani nami nilikuwa naomba.
“Wakati huo nikiwa Kaimu Mkuu wa Idara nina wajibu wa kuhakikisha kazi zinafanyika kama kawaida. Wote walio chini yangu nina wajibu wa kuwasimamia kiutumishi, kitaaluma na kiidara. Mtu akishindwa kusimamia hayo, katika mchakato anaweza kudhani kuwa labda kwa kuwa wote tumeomba ndiyo maana nafuatilia. Unaomba ripoti mtu hatoi itakuwaje?
“Hizo ni taratibu za kawaida za kiuongozi. Kama kuna malalamiko katika eneo hilo, hayana msingi. Sikuwa na uwezo wa kuzuia wasiombe, hakuna hata mmoja anayeweza kusema aliomba akanyimwa.
“Mchakato ulikamilika … kikao cha Bodi cha mwisho kilichokaa Mtwara tarehe 28-29 Desemba, 2013, Bodi ya Wakurugenzi ikafanya uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi, tarehe 3 Januari Mwenyekiti alitangaza mbele ya vyombo vya habari. Miongoni mwa waliokuwa wanakaimu nafasi tulipewa nafasi, akiwamo Mkurugenzi wa Utumishi,” alisema Magesa.
Kuhusu mfumo wa kufuatilia mizigo, alisema: “Mfumo huu unafuatilia tangu mizigo inapopakiwa na mfumo huu waElectronic Cargo Tracking Note (ECTN), document mteja anapaswa kuziwasilisha uzisubmit electronically. Unatoa commercial invoice, export document zinakuwa verified na authorities mbalimbali kuthibitisha uhalali wake. Tunazipata kwa njia ya kimtandao. Tunajua particulars za mzigo, na gharama halisi ya mzigo iliyothibitishwa na mamlaka ya nchi husika.
“Changamoto ni kujua gharama halisi ya mzigo, mapato, ushuru wa bandarini (wharfage). Mfanyabiashara akitaja thamani ndogo hata Mamlaka inakosa mapato yake. Wafanyabiashara hicho kitu hawakipendi wanaona inavujisha siri.”
Alipoulizwa iwapo TPA ina uwezekano wa kupata thamani halisi ya mzigo unaoingizwa nchini, alisema: “Hakuna mfumo kama huo, isipokuwa kilichopo ni kwamba meli zina mifumo yao ya kufuatilia mizigo kwenye meli zao, accessanayo mwenye meli, agent wake na mwenye mzigo. Tukisema tunataka kujua mizigo yote inayoingia Dar es Salaam,unless tuziandikie meli zote zinazoingia bandarini zitupe taarifa. Hakuna mfumo integrated wa kufuatilia mizigo, kila taasisi ina mfumo wake.
Kuhusu suala la kamera za CCTV kutofanya kazi, alisema: “Kamera zilikuwa zimewekwa kwenye baadhi ya maeneo si bandari nzima. Bandari imepanuka mno, miundombinu mingine wakati wanabadilisha baadhi ya nyaya zinazohusika na baadhi ya vifaa, vikawa vimekatika, mfumo ule ukawa umekatika.” Tangu mwaka 2008 hakuna kamera za usalama bandarini, mizigo inalindwa kwa nguvu za Mwenyezi Mungu.
Suala la mafuta ya petroli na dizeli kuingizwa nchini bila kupimwa kwenye flow meter kwa muda mrefu sasa tangu mwaka 2011, Magesa alisema: “Flow meters wale wa vipimo walisema mita hazitoi vipimo sawa sawa. Walizuia zisitumike kwa sasa taratibu zilizopo ni kununua mita nyingine.”
Magesa alisema zabuni ya kufunga mifumo ya usalama na mitandao mingine ya kuongeza ufanisi wa Bandari, zabuni ilishatangazwa ila wanasubiri ‘no objection’ ya Benki ya Dunia ila ana uhakika ndani ya miezi saba hadi tisa watakuwa wamefunga mifumo hiyo.
Mkurugenzi huyo alieleza malengo: “Lengo sasa hivi ni kutumia TEHAMA kuongeza ufanisi wa Mamlaka kwa upande wa kazi ya utekelezaji kupakia na kupakua mizigo, kudhibiti matumizi ya mamlaka ya fedha na rasilimali nyingine na kuwezesha kufanya uamuzi wa haraka ya kimenejimenti kwa nia ya kuongeza tija.
“Miradi tunayotekeleza kwa sasa electronic single window system, tunatarajia tumeanza utekelezaji, mkandarasi amepatikana na wadau wote wameshirikishwa vizuri, tunatarajia mradi huu utachangia kutimiza moja ya malengo makubwa ya taasisi na ya Serikali, ni mmoja wa miradi iliyoainishwa katika Matokeo Makubwa Sasa. Ukamilikaji wa mradi huu unatarajiwa kupunguza dwell time kwa kiasi kikubwa kutoka siku tisa hadi tano. Na miradi mingine, awamu ya kwanza miezi saba na nyingine kuna awamu tatu.
“Pia tuna mradi wa electronic payment system – kurahisisha mfumo wa malipo, kwa wateja na watumiaji wote wa bandari. Mradi wa udhibiti wa mafuta (fuel management system) ndani ya Mamlaka. Kudhibiti matumizi ya mafuta na vifaa (mitambo), ambayo lengo ni kupunguza matumizi kwa asilimia 40 ya kwenye eneo. Itasaidia kupunguza tatizo la wizi pia,” alisema.
Magesa hakutaka kuzungumzia tuhuma kuwa yeye ndiye anayeendesha fitina bandarini dhidi ya wafanyakazi, na kwamba yeye kuwa Mjumbe wa NEC-CCM kunachangia siasa kuingizwa kwenye utumishi wa umma. “Chama kimetuzuia kuzungumza siasa, tusubiri 2015.”
Je, unajua Bodi ya Wakurugenzi iliyovunjwa kabla ya kuvunjwa kwake ilisema nini juu ya Madeni Kipande na utendaji wake? Je, unajua kuwa Bandari imeshindwa kutekeleza maagizo ya Kamati iliyoteuliwa na Waziri Dk. Harrison Mwakyembe? Usikose toleo lijalo.
Kilichotokea mwandishi alipomtafuta Kipande
Aprili 1, 2014 mwandishi wa habari hizi alimpigia simu kuulizia iwapo maswali yake yalifika, au yalipotelea njiani kwani hayajajibiwa. Kwa dharau ya aina yake, alisema:
“Hivi wewe Balile una uzalendo kweli? Maswali yenyewe ya kitoto, ulitaka nijibu nini?”
Baada ya kauli hiyo, mwandishi wa habari hizi aliamua kumpasulia ukweli hadi Kipande akanyamaza kimya. Alimweleza wizi anaoufanya kwa kutumia mifumo mipya ya mawasiliano bandarini (ICT), alimweleza kamera za CCTV zilivyoachwa makusudi kwa nia ya kufanikisha wizi na kwamba Mkurugenzi wake wa IT alikwishakiri kuwa hazifanyi kazi tangu mwaka 2011.
Kisha mwandishi wa habari hizi alimuonya Kipande kujiepusha na tabia ya kufokea au kudharau watu asiowafahamu, hasa ikitiliwa maanani kuwa tabia hii ilikuwa imeushawishi uongozi wa juu kumuondoa bandarini Desemba 31, mwaka jana, lakini Mtawa na Gurumo wakafukia mashimo. Baada ya majibizano, Kipande alikaa kimya sawa na mtu aliyenyeshewa na mvua kwani inawezekana hakuyatarajia majibu aliyopewa, kisha akasema:
“Samahani kaka, hayo tuyaache sasa tumeishia wapi?” Mwandishi akamwambia kinachotakiwa ni miadi kwa nia ya kumuonesha vielelezo vilivyopo aweze kuvitolea ufafanuzi, likiwamo hili la kumdanganya Dk. Mwakyembe kuwa Bandari inakusanya Sh bilioni 50 wakati haijawahi kufikia kiwango hiki. Baada ya kibano hicho, Kipande akasema.
“Kaka sasa naomba tukutane Ijumaa (Aprili 4) saa 8 ofisini kwangu na Magesa atakuwapo.”  Mwandishi alimshukuru na kukata simu.
Ilipofika saa 10:13 jioni, Meneja Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi, alimpigia simu mwandishi wa habari hizi na kwa mshangao akasema.
“Hallo, ni kaka Balile?” Mwandishi akaitikia ndiyo. “Mkurugenzi Mkuu ameniambia nikupigia simu.” Mwandishi akasema sawa nimepokea, niambia kakupa ujumbe gani.
Janeth akasema: “Hakunipa ujumbe wowote ila ameniambia nikupigia simu tu.”
Mwandishi akamuuliza kama hana ujumbe anapiga kwa ajili gani.
Ndipo akamwambia kilichotokea na jinsi mwandishi alivyomweleza ukweli bila kificho mkurugenzi huyo.
Inawezekana katika hali ya kuchanganyikiwa, Kipande alimwambia Janeth apige simu bila kujua ujumbe upi aufikishe kwa mwandishi na hali hiyo ilijitokeza tena siku ya Ijumaa. Mwandishi alipofika lango kuu, alijitambulisha na mlinzi akapiga simu kwa Katibu Muhtasi wa Kipande, aliyeruhusu aende ofisini kwa Kipande, kuna maelekezo yake.
Mwandishi alipofika kwenye lango la pili, walinzi walipopiga simu, mara Katibu Muhtasi akasema mwandishi akazungumze na Janeth… mara akasema mwandishi aondoke kwani Kipande aliitwa wizarani na Naibu Katibu Mkuu, na baada ya mkanganyiko huo mwandishi aliondoka.
Mwandishi alimtumia Kipande ujumbe mfupi akimweleza jinsi alivyotekeleza wajibu wake kisheria wa kumpa fursa ya kufafanua tuhuma dhidi yake, kwa miadi na maswali yaliyowasilishwa ofisini kwake, kisha Kipande akajibu ujumbe huo kwa SMS hivi:-
“Nimeitwa wizarani tangu saa tatu, niliacha maelekezo kumuona meneja wa Communications, hawakukwambia?” Mwandishi alipomjibu kuwa hawakufanya hivyo, akajibu ujumbe wa mwisho, hivi: “Pole brother.”