Baada ya kusomwa makala zangu, watu wengi wameniletea ujumbe kwa simu ya kiganja na kwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms). Kwa vile niko wodini hoi hapa Lugalo sikuruhusiwa kuongea na simu ila mjukuu wangu Max Mchola alikuwa ananiarifu nani kanipigia simu na kasema nini.
Kwa faida ya wasomaji wa makala zangu nimeona basi angalau zile sms azinakili pindi nikipata unafuu nitazisoma. Baada ya kusoma ninaona niwaletee wale wasomaji wa JAMHURI waone zimesemaje. Moja ya sms hizo kumbe imetoka kwa mjane wa Paulo Sozigwa, ndipo nikafarijika kuwa ujumbe wangu umesikika na ninaamini Ikulu – Chief Accountant na Hazina watachukua hatua mwafaka katika hili.
Hapa basi naleta baadhi ya hizo sms wasomaji waone. Kilichonifurahisha sana ni ule uamuzi wa Serikali ya Rais John Magufuri uliotangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, bungeni kuwa “WAZEE zaidi ya miaka 60 KUTOLIPA KODI YA MAJENGO (Property Tax). [Tazama Habari Leo, Toleo Na. 03838 la Ijumaa Juni 23, 2017].

Basi nikaona lile ombi la wazee tulilolitoa kwa Serikali Oktoba Mosi-Siku ya Wazee Dunlani na Rais Benjamin Mkapa akalitolea uamuzi, sasa limesikilizwa.
Basi kwa faida ya wazee wote nimeomba JAMHURI wanukuu wakala ule “VERBATUM” ili wazee waone Serikali ilitoa uamuzi upi. Mhariri ameniahidi kuuchapisha toleo lijalo.
Sms kutoka kwa 0783 935030 Apirili 16, 2017
1. Hongera sana mzee wetu kwa makala kuhusu hayati Paulo Sozigwa. Pamoja na kuandika naomba pia jaribu kufuatilla mwenyewe kujua kilijili nini? Nahisi anaweza kuwa kaponzwa na 2005 ila hiyo haitoshi kutendwa aliyotendwa.

2. Sms kutoka 0754 837229
Asante kwa makala nzuri inayosimamiwa Roho Mtakatifu azidi kukujalia neema zake ili kusimamia na hivyo kumdhihirisha Bwana jinsi anavyotenda kazi katika maisha na wajibu wetu. Umeandika na kuudhihirisha ukweli na hata kutufundisha vile inavyotupasa kuwa (Toleo na 297, JAMHURI, Jumanne Juni 6-12, 2017) Uk 10-18)… Naye Bwana akuzidishie Imani Tumaini letu.

3. Sms kutoka 0753 123231 Juni 13, 2017
Mungu akubariki sana tena sana mkuu kwa kuwaeleza ukweli juu ya mlezi wangu marehemu Mzee Paulo A. Sozigwa. Hakika binafsi nimefurahi mno kwa upendo wako wa dhati juu ya marehemu Sozigwa kwa kweli amefanyiwa ukatili uliopitiliza.

4. Sms kutoka 0716 100382 Juni 13, 2017
Nimesoma makala zako kuhusu malipo ya Mzee Paulo Sozigwa. Hakuna ubishi kuwa alifanya kazi GT tangu ukoloni hadi Uhuru na baadaye hoja moja muhimu hujazungumzia. Je, kwanini alipostaafu at the age of 55 ie 1988 hakudai mafao yake ya kustaafu? Alikuwa anasubiri nini? Ajizi nyumba ya njaa.

5. Sms kutoka 0715 287 406
Amani iwe juu yako, kazi nzuri sana umeifanya katika suala la hayati Sozigwa, yeye alikuwa mwadilifu mwenye mamlaka na sasa ni watazamaji ndiyo walioamua kumuokoa. Dhulma tupu. Mola akujaalie siha njema.

6. Sms kutoka 0753 123231 Juni 13, 2017
Mungu akujalie na akupe afya njema. Ni kwa namna gani unavyotetea wazee wastaafu wa miaka hiyo. Paulo Sozigwa alikuwa afisa wa ngazi ya juu. Je, wale wa chini, si ndiyo wanaambulia njoo mwakani, umewasha moto wa haki na upendo. Familia ya P. Sozigwa itakujalipwa. Mimi Sgt. Charles Mwanjelwa Police HQs DSM.

7. Sms kutoka 0788 515472 Juni 21, 2017
Nimesoma makala yako kuhusu Paulo Sozigwa alivyotendewa, lakini ungeenda kwa undani hilo tatizo la Sozigwa, bali ni kilio cha wastaafu wengi ambao walitumikia nchi kwa uadilifu mkubwa, lakini bado wanahangaika, wengine wameshatangulia mbele za haki na hawajapata chochote.

8. Sms kutoka 0716 612 960
Pole sana kwa utetezi wa Mzee Sozigwa, lakini kumbuka anyimwae hana utetezi ni huruma ya mtoaji tu, sio mtetezi maana huyu amenyimwa sio hana haki, haki kanyimwa.

9. Sms kutoka 0787 413 280
Nimefuatilia sana maelezo yako juu ya suala la mzee wetu marehemu Sozigwa. Hongera sana Baba kusema ukweli kama wahusika na suala lile watatumia hekima na busara, haki ile walipwe warithi wake. Mungu atawatolea hukumu kwenye maisha yao yajayo, umesema maneno makubwa sana, Mungu akubariki wewe na familla yako.

10. Sms kutoka 0716 656 877
Nimefuatilia kwa makini na shukrani juu ya masikini Sozigwa katika gazeti la JAMHURI -tangu mwanzo mpaka hitimisho lake leo. Japo sijawa na nguvu sana, nimepata changamko la moyo kuweza kutoa shukrani kwa ujasiri na umakini wa uliyoyazungumza. Tuache mwamuzi wa haki mapenzi yake yatimizwe.
(Mrs. Sozigwa Paul) Monica Kuga.

11. Sms kutoka 0712 192717
Nilikuwa nasoma makala yako kuhusu Sozigwa, leo na jana nimesikia msamaha wa kodi ya majengo kwa wazee umepitishwa bungeni. Hongera sana natumaini na haki kwa hayati Sozigwa itatendeka. Mada hii imenigusa sana kwa kuwa nilimsaidia sana mama yangu kufuatilia mafao yake pale Hazina kwa sasa ni marehemu. Bahati aliyapata. Haki inapiganiwa, haiji kirahisi.

12. Sms kutoka 0676 792023
Hongera kwa kujali wanaodhurumiwa. Mungu akulipe, watasikia tu.

Ndugu zangu, nimeona niwaletee sms hizi ili kuonyesha namna wasomaji walivyoguswa na suala hili. Mungu awabariki.

2902 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!