Wamdanganya Magufuli

Kashfa imegubika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wafanyakazi, Mei Mosi mwaka huu yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya.

Kashfa hiyo imekikumba Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU). Ndani ya chama hicho, baadhi ya viongozi wake wanadaiwa kuwasilisha jina la kigogo asiyestahili kuwa mfanyakazi bora, akapewa mkono na Rais Dk. John Magufuli na kukabidhiwa cheti cha mfanyakazi bora na zawadi ya hundi.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa katika mchakato wa kumsaka mfanyakazi bora kutoka katika Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania, kinachohusisha pande mbili, wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) na wale wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), mambo yalikwenda vizuri, lakini yaligeuzwa kwa wafanyakazi wa TRL dakika za mwisho wakati shughuli za kilele cha Mei Mosi zikiendelea Uwanja wa Sokoine, mgeni rasmi akiwa Rais Dk. Magufuli.

Katika mchakato wa upigaji kura, JAMHURI limethibitishiwa kuwa mfanyakazi wa kada ya chini, James Kunena, ndiye aliyeshinda kuwa mfanyakazi BORA kwa mujibu wa kura zilizopigwa kupitia TRAWU.

Hata hivyo, kwa njia ya hila zilizofanywa na baadhi ya viongozi walifanya uchaguzi wa kumpata mfanyakazi HODARI, kwa hiyo kulikuwa na mshindi wa kundi la mfanyakazi BORA ambaye ndiye anastahili kuhudhuria sherehe za kitaifa za Mei Mosi na kukabidhiwa zawadi zake na mgeni rasmi. Mshindi wa kundi la mfanyakazi HODARI, kwa kawaida, kwa mujibu wa taratibu za TRAWU huhudhuria sherehe za Mei Mosi kikanda na hukabidhiwa zawadi na mgeni rasmi wa sherehe hizo za kikanda ambazo ni ndogo ukilinganisha na zile za kitaifa.

“Mshindi wa tuzo ya mfanyakazi BORA TRAWU kwa mujibu wa kura za wafanyakazi ni James Kunena, na mshindi wa tuzo ya mfanyakazi HODARI ni Focus Sahani, ambaye ushindi wake ulipatikana baada ya kura kupigwa kwa raundi tatu.

“Wafanyakazi wote tulijua kwamba Kunena ndiye mshindi wetu, na atakuwa katika sherehe za kitaifa Mbeya kukabidhiwa zawadi zake, jambo ambalo lingetupatia hamasa zaidi sisi wafanyakazi wa kawaida, lakini kinyume chake, akatangazwa Focus Sahani ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji TRL,” ameeleza mmoja wa watoa habari wetu aliyeshiriki mchakato wa kusaka mfanyakazi bora.

Ilivyokuwa Uwanja wa Sokoine  

Dalili za mipango hiyo ya ‘kupindua’ mshindi zilianza kubainika wakati shughuli ikiendelea. Wakati wa kusoma majina ya washindi wa kipengele cha wafanyakazi bora kwa upande wa TRAWU – TRL akatajwa Focus Sahani badala ya James Kunena.

Sahani akasogea mbele ya Rais Magufuli na kukabidhiwa zawadi, lakini kutokana na hilo, Kunena akawa mkali, akawahoji viongozi wake, imekuwaje?

Hili analibainisha mwenyewe Kunena katika mazungumzo yake na JAMHURI. Anasema: “Sikuelewa kilichotokea, nilisafirishwa kwenda Mbeya kwa kuwa ndiye mshindi wa kipengele cha mfanyakazi bora, nikashangaa mfanyakazi hodari ndiye anaitwa badala yangu, huyu mfanyakazi hodari alipaswa kushiriki sherehe za Mei Mosi kikanda ili apewe zawadi yake huko.

“Kutokana na hali hiyo ilibidi nimuulize Katibu Mkuu wa TRAWU (Taifa) kuhusu jina langu kuondolewa kinyume cha matakwa ya wafanyakazi walionipigia kura za ushindi. Akaniambia waliwasilisha jina langu, na kwamba nisubiri wafuatilie kilichotokea.

“Focus Sahani alikwenda kushikana mkono na rais na kupewa zawadi ya mfanyakazi bora, baada ya mimi kuhoji Katibu Mkuu akaniletea bahasha ndogo ya kaki yenye hundi mbili. Hundi ya kwanza yenye shilingi milioni mbili, na hundi ya pili ya shilingi laki tano. Nikauliza, vipi kuhusu zawadi ya cheti? Akasema ‘utapatiwa Dar es Salaam’.

“Hiyo iliniumiza sana kwa kuwa washindi wote walipewa zawadi na kushikana mkono na Mheshimiwa Rais. Sikutaka kuhoji sana kwa kuwa viongozi hao ndio walionisafirisha kwenda Mbeya, sikuwa na nauli ya kurudi. Nimerudi Dar es Salaam, wafanyakazi wenzangu wananilaumu…nimeingia katika mgogoro na wafanyakazi wenzangu walionipigia kura kuwa mfanyakazi bora kwa mwaka 2019. Wanasema nimehongwa pesa ili niondoe jina langu na kuwekwa jina la bosi wetu, Focus Sahani.

“Nimekanusha hili kwao, lakini hawanielewi, nimewasilisha malalamiko kwa wakubwa zangu wa chama ngazi ya mkoa na kanda, wanasema wanalifanyia kazi suala hili,” amesema James Kunena.

Gazeti hili limewasiliana na Focus Sahani, ambaye alimweleza mwandishi wetu kuwa yuko katika mkutano na atumiwe ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, lakini hadi tunakwenda mitamboni hatua zote hizo hazikuzaa matunda katika kupata maelezo yake ingawa juhudi hizo zinaendelea.

Vigogo walonga

Katika kuzungumzia kadhia hiyo, Katibu Mkuu wa TRAWU – taifa, Nashoni Mariyeri, ameliambia JAMHURI kwamba wote wawili – James Kunena na Focus Sahani walistahili kupata zawadi kwa kiwango sawa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Magufuli.

Amefafanua kuwa, kutokana na muda kuwa mfupi na matakwa ya kutaka orodha ya wanaotakiwa kupewa zawadi kupunguzwa, James Kunena alikubali mwenzake amwakilishe kupokea zawadi hizo.

“Walikubaliana kwamba mwenzake amwakilishe. Kila mmoja aliandaliwa zawadi ya hundi ya shilingi milioni 2.5 pamoja na cheti,” amesema.

Kiini cha utata

Utata unaogubika sakata hili ni kwamba, cheti cha mfanyakazi (bora) kwa upande wa wafanyakazi wa reli kinapaswa kutwaliwa na watumishi wawili tu, mtumishi mmoja kutoka TAZARA na mtumishi mwingine kutoka TRL, kwa maana hiyo, ahadi ya kumtengenezea cheti kingine James Kunena cha ufanyakazi bora itaifanya TRL kutoa wafanyakazi bora wawili kwa mwaka 2019, jambo ambalo linatajwa kutokuwahi kutokea katika historia ya Mei, Mosi nchini.

“Shida iliyopo sasa ni kupata cheti halisi. National Best Workers (wafanyakazi bora) vyeti vyao hutoka Shirishiko la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), ushindi wa madaraja mengine ya chini (mfanyakazi hodari) hutolewa na ngazi za vyama vyenyewe si shirikisho.

“Kwa maana hiyo, katika rekodi za wafanyakazi bora mwaka huu pale TUCTA, kutoka TRL hatakuwapo James Kunena kama alivyochaguliwa na wafanyakazi wenzake, atakuwapo James Focus.

“Wakisema wampe cheti sasa, TRAWU haijapata kuwa na ‘Best National Workers’ watatu kwa mara moja, huwa ni mmoja kutoka TAZARA na mwingine kutoka TRL, sasa hicho cheti kinaweza kuwa ‘feki’.

“Cheti hiki cha kupeana baada ya Mei Mosi hakitaingizwa kwenye rekodi za mwaka huu,” ameeleza mmoja wa viongozi wa juu aliyeshiriki Mei Mosi mwaka huu mkoani Mbeya, ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini.

Akizungumzia kuhusu hoja za Katibu wa TRAWU kwamba kulikuwa na makubaliano kati ya Focus na Kunena, kiongozi huyo naye amehoji: “Kama kulikuwa na makubaliano kwa nini James Kunena anahoji kuhusu haki yake kuporwa?

“Amekwisha kulalamika rasmi kwa Mwenyekiti wake wa Kanda ya Dar es Salaam TRAWU, kuna viongozi kadhaa wamekwisha kufikishiwa malalamiko haya, Mei 4, 2019 tulikaa kikao kilichohusisha mwenyekiti na katibu wa matawi mawili ya TRL, tawi la Karakana na tawi la Makao Makuu kujadili suala hili, tuliazimia apewe cheti chake cha mfanyakazi bora kama ilivyostahili.”

Taarifa zaidi zilizolifikia JAMHURI zinabainisha kuwa suala hilo halikuwafurahisha wafanyakazi wa kawaida wa TRL kiasi cha kutikisa ufanisi wao kikazi, wakiamini kuwa utashi wao wa kutaka mwenzao awe mfanyakazi bora umepuuzwa.

“Sisi tumemwinua mfanyakazi mwenzetu, akashikane mkono na Rais Magufuli, apewe zawadi zake na Mheshimiwa Rais. Matokeo yake mlala hoi mwenzetu ameenguliwa, tumesikitishwa sana na hili, tunaomba haki itendeke,” amesema mmoja wa wafanyakazi aliyepata kupiga kura ngazi ya tawi kumchagua mfanyakazi bora ndani ya TRAWU, akitaka jina lake lihifadhiwe ili kutoshughulikiwa kinidhamu na watendaji wa ngazi za juu.

TUCTA wazungumza 

JAMHURI lilifika ofisini kwa Katibu Mkuu wa TUCTA, Dk. Yahya Msigwa, kupata ufafanuzi wa kadhia hiyo. Pamoja na mambo mengine, JAMHURI lilitaka kufahamu, kwanza, barua iliyowasilishwa kwao kutoka TRAWU ilibainisha nani mfanyakazi bora. Pili, hundi iliyoandaliwa na cheti kiliandikwa kwa jina la nani.

“Siioni barua yao. Hawakuleta barua yenye majina hapa ofisini, walikuja Mbeya (kwenye kilele cha Mei Mosi) moja kwa moja, tulipata jina kwenye maadhimisho hayo,” amesema Katibu Mkuu huyo wa TUCTA, lakini alipoulizwa kufafanua kuhusu utaratibu wa ofisi yake kupata majina ya wafanyakazi bora kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini alijibu:

“Mimi (Katibu Mkuu TUCTA) ndiye ninawaandikia barua vyama vyote kuwataka wawasilishe majina ya wafanyakazi bora kwa barua. Nikishapokea barua, ndipo tunaandaa vyeti na zawadi. Orodha hiyo ndiyo inayosomwa katika kilele cha maadhimisho ya Mei Mosi.”

Kuhusu suala hilo la TRAWU alisema jina alilopewa katika hatua za mwisho ni Focus Sahani, na kama kuna kasoro nyingine si suala la TUCTA bali uongozi wa TRAWU.

Sherehe za kitaifa za Mei Mosi mwaka huu zilifanyika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, mgeni rasmi akiwa Rais Dk. Magufuli.