Na Nizar K Visram (Canada)

Machi 10 hadi 12, mwaka huu wanaharakati kutoka nchi za Afrika wamekutana Dakar, Senegal. 

Hawa ni wawakilishi wa makundi kutoka Botswana, Cameroon, Cote d’Ivoire, DR Congo, Gambia, Ghana, Guinea-Bissau, Mauritania, Morocco, Msumbiji, Namibia, Tunisia,  Zambia, Malawi, Sudan, Tanzania, Senegal, Nigeria, Zimbabwe, Kenya na Afrika Kusini.

Makundi haya yanaungana chini ya mtandao wa umajumui wa Kiafrika wa mshikamano na Palestina (Pan-African Palestine Solidarity Network – PAPSN).

Mkutano wa Dakar uliandaliwa na ulingo wa mshikamano wa Senegal na Palestina (Plateforme de Solidarieté Sénégal-Palestine) pamoja na tawi la Senegal la Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu (Amnesty International – AI). 

Kaulimbiu yao ilikuwa; ‘Kuanzia Afrika hadi Palestina: Umoja Dhidi ya Ukaburu’.  

Senegal ilichaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano kwa sababu nchi hiyo ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU). Pia Senegal imekuwa mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu haki za kimsingi za wananchi wa Palestina (UN Special Committee on the Exercise of the Inalienable Rights of the Palestinian People – CEIRPP).

Kuhusu Amnesty International, mkutano huo ulifanyika mwezi mmoja tu tangu asasi hiyo ya kimataifa kutoa ripoti ikifafanua jinsi Israel inavyoendesha utawala wa kikaburu dhidi ya Wapalestina.

Roshan Dadoo, msemaji wa PAPSN na mratibu wa asasi ya Afrika Kusini inayotetea vikwazo na marufuku dhidi ya Israel (Boycott, Divestment and Sanctions Coalition) anasema:

“Hii ni mara ya kwanza wanaharakati wa Kiafrika wanaounga mkono Palestina kukutana pamoja. Mkutano kama huu haujawahi kufanyika katika bara letu.”

Wajumbe walijadili jinsi ya kukabiliana na mikakati ya Israel ya kuvuruga msimamo wa Afrika wa siku nyingi wa kuunga mkono harakati za Wapalestina. 

Mkutano ukapitisha azimio la kuimarisha mshikamano wa Bara la Afrika na Palestina na kuanzisha kampeni kabambe ya kuisusia na kuigomea Israel (BDS), sawa na harakati ya ukombozi wa Afrika Kusini. 

Kutoka Palestina alikuwapo Jamal Juma, mwanachama mwanzilishi wa kamati ya Palestina ya BDS. Yeye anasema: “Uamuzi wa PAPSN wa kuimarisha mfungamano wa Bara la Afrika na Palestina unatupa matumaini na kututia moyo sisi Wapalestina, jambo ambalo ni muhimu sana katika harakati zetu dhidi ya ukaburu wa Israel.” 

Kutoka Afrika Kusini alikuwapo Nkosi Zwelivelile Mandela, mbunge na mjukuu wa baba wa taifa wa nchi hiyo Nelson Mandela. Yeye anasema:

“Mkutano huu unatuma ujumbe kwa wananchi wa Palestina kuwaambia kuwa msijisikie wapweke, kwani wananchi wa Afrika wako pamoja nanyi, sawa na nyinyi mlivyosimama nasi wakati tukipigania ukombozi wa bara letu. 

“Sauti zetu lazima ziungane na kushikamana na wananchi wanaoteseka kote duniani, kuanzia Ukraine, Kashmir, Myanmar, Syria, Sahara Magharibi, Amerika Kusini hadi Palestina. Huu ni urithi tulioachiwa na shujaa wa ukombozi, Rais Nelson Mandela ambaye alisema ukombozi wetu hautakamilika mpaka kila binadamu duniani akombolewe.”

Akazungumza kuwa PAPSN inapaswa kuwahamasisha wananchi wa Afrika ili wakatae njama za Israel za kueneza katika bara letu siasa yao ya uzayuni. Akawataka wajumbe wafanye kampeni ya BDS dhidi ya Israel barani Afrika. 

Akaongeza kuwa katika bara letu Israel imekuwa ikitumia diplomasia ya kuhonga (chequebook diplomacy), huku wakijifanya wanasaidia maendeleo yetu.

Akakumbusha kuwa leo hii Wapalestina milioni sita wanaishi ukimbizini, wakinyimwa haki yao ya kurudi nyumbani. Pia maelfu ya wafungwa wa kisiasa wameswekwa gerezani bila ya kufikishwa mahakamani au kupewa haki ya kujitetea. 

Wakati huohuo ardhi ya Wapalestina inaendelea kuporwa na walowezi wanaojenga makazi haramu, huku makazi ya Wapalestina yakibomolewa. 

Haya yanafanyika katika maeneo ya Sheikh Jarrah, Silwan, Hebron Kusini na kwingineko katika Ukingo wa Magharibi.

Kutoka Tanzania walikuwapo wajumbe wawili nao ni Hassan Khamis wa kamati ya mshikamano wa Tanzania na Palestina (TPSC) na Emma Lwaitama Nyerere kutoka umoja wa wanawake katika umajumui wa Afrika (Pan-African Women’s Organization). 

Hassan alimnukuu Mwalimu Nyerere akionyesha jinsi Tanzania ilivyokuwa siku zote ikiunga mkono harakati za Wapalestina. Emma alieleza jinsi mawazo ya Mwalimu Nyerere yalivyoimarisha mshikamano wa Tanzania na wanaukombozi wa Palestina. Kwani Mwalimu aliwahi kusema:

“Sisi hatukusita hata siku moja kuwaunga mkono wananchi wa Palestina katika harakati ya kuikomboa nchi yao. Hali yao ni mbaya kuliko sisi tulivyokuwa wakati wa ukoloni. Tulipokuwa tukipigania uhuru wetu, mimi nilikuwa nikiishi nchini Tanganyika. Lakini Wapalestina wamenyimwa hata haki ya kuishi nchini mwao.”

Kutoka baraza la mshikamano wa Zimbabwe na Palestina (ZPSC) alikuwapo mwenyekiti wake Mafa Kwanisai Mafa ambaye alisema wajumbe wanakutana wakati Waafrika wanalaani Israel kupewa hadhi ya mtazamaji katika Umoja wa Afrika (AU). Hii inafanyika licha ya ripoti ya AI kudhihirisha kuwa Israel ni nchi ya kikaburu inayowanyima Wapalestina haki zao za kimsingi. 

Mafa pia alitaka mkutano uandae kampeni ya kufichua mbinu za Israel barani Afrika, hasa miongoni mwa Wakristo wanaoamini kuwa Israel ni nchi takatifu. Akasema asasi yake nchini Zimbabwe inashirikiana na vikundi mbalimbali vya kijamii. 

Mwisho wa mkutano huu wa kimkakati wanaharakati wakatoa risala wakisema wametiwa moyo sana na wananchi wa Palestina jinsi walivyojizatiti, wakitaka ulimwengu uwaunge mkono kwa kutumia mbinu za BDS.

Wajumbe pia walitiwa moyo na ripoti ya AI na mashirika mengine ambayo yamedhihirisha ukaburu wa Israel dhidi ya Wapalestina, mfumo ambao umekuwa ukiendeshwa zaidi ya miongo saba. 

Mkutano ulizungumzia mshikamano wa Afrika na Palestina pamoja na mbinu za Israel za kupenyeza sera yao ya ukaburu katika Afrika. Matokeo yake ni Israel kupewa hadhi ya waangalizi katika Umoja wa Afrika, kitendo cha aibu kilichofanyika Julai 2021. 

Wakati huohuo Israel imekuwa ikitumia Afrika kama soko la kuuza silaha zake za kijeshi na teknolojia ya ujasusi aina ya Pegasus. Yote haya yanadhoofisha demokrasia na kukuza udikteta katika Bara la Afrika.

Mkutano pia ulizungumza jinsi uzayuni ulivyojipenyeza barani Afrika kwa njia ya kitheolojia, kwa madhumuni ya kuhalalisha ukaburu wa Israel. 

Mkutano ukatoa wito kwa serikali za Afrika na Umoja wa Afrika zichukue hatua zifuatazo:

  • • Batilisha nafasi ya Israel katika AU. 

 .Tambua Israel kama utawala wa kikaburu na kutaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya uhalifu huo. 

. Simamisha mara moja ununuaji wa silaha za kivita na teknolojia ya kijasusi kutoka Israel. 

  • • Vunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel kama tulivyofanya kwa utawala wa makaburu wa Afrika Kusini. 

Wanaharakati waliokusanyia mjini Dakar kutoka Bara zima la Afrika wakaamua kuimarisha mshikamano wao na wananchi wa Palestina, kwa vile waliamini kuwa Afrika haiwezi kuwa huru mpaka Wapalestina nao wawe huru kutokana na ukandamizaji, uvamizi na ukoloni wa Israel. 

Wakaamua waimarishe mtandao wa PAPSN ili kuwahamasisha wananchi katika Bara la Afrika, hususan wanawake na vijana, kwa nia ya kuunga mkono Wapalestina katika harakati zao za kujikomboa.  

Ni vizuri tukaongeza kuwa Amnesty International ilisambaza ripoti yake tarehe 1 Februari 2022 baada ya utafiti uliochukua miaka minne. Ripoti hiyo inaeleza kirefu jinsi Israel inavyopora ardhi na mali za Wapalestina, inavyowaua, inavyowafukuza kutoka katika ardhi na makazi yao, inavyowanyima haki ya kutembea au kusafiri na inavyowanyima uraia. 

Ripoti inasema yote haya ni makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria ya kimataifa kama ilivyoainishwa katika Waraka wa  Rome kuhusu Ukaburu. AI kwa hiyo imetoa wito kwa Mahakama ya Kimataifa (ICC) na mataifa yote yachukue hatua za kisheria dhidi ya Israel.  

Licha ya AI, mashirika mengine ya kutetea haki za binadamu ambayo yamelaani ukaburu huu ni pamoja na Al-Haq, Al-Mezan, Human Rights Watch, UN ESCWA, B’Tselem na Adalah. 

 [email protected] 

By Jamhuri