Wananchi Mtwara walia na Tanesco

MTWARA
NA CLEMENT MAGEMBE
Wananchi wa Mtwara wamelilia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kukatika kwa
umeme mkoani humo kuwa unawanyima fursa ya kuendesha shughuli zao za uzalishaji mali na
kujikwamua na umaskini.
Wakizungumza na JAMHURI mkoani humo mwishoni mwa wiki iliyopita, wamesema hawaoni
faida yoyote ya kuwa na umeme kutokana na kukatikakatika hovyo kila siku, na sababu
zinazotolewa na Tanesco zinakuwa za kisiasa zaidi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Namela, Hassan Matimbango, amesema licha ya kijiji hicho kupata
umeme wa REA, imekuwa kawaida kukosa umeme kwa muda mrefu na shughuli zote
zinazohitaji umeme zinakwama.
Matimbango amesema bado wananchi hawajaona faida ya umeme kutokana na mgawo
unaoendelea kila siku bila sababu zinazoeleweka.
Mwajuma Abdallah, mfanyabiashara na mkazi wa Mtwara Mjini, amesema kila siku umeme
umekuwa ukikatika na kuwaka, na wakati mwingine kuunguza vifaa vyao vinavyotumia umeme.
Abdallah amesema kilichotawala sasa ni siasa ambazo hazina tija kwa uchumi wa nchi na
iwapo utaratibu utaendelea kuwa hivi ndoto ya kuwa na viwanda inaweza kuchelewa, huku
mikoa ya kusini ikikabiliwa na umaskini wakati ina rasilimali nyingi.
“Gesi inapatikana hapa lakini umeme tunaoupata ni ubabaishaji mtupu, tunachosubiri ni ahadi
ya Serikali kuboresha miundombinu ya umeme ili tupate umeme wa uhakika,” amesema
Abdallah.
Amesema usumbufu mwingine wanaoupata kutoka Tanesco ni pale wanapotaka kuwekewa
umeme wanakabiliwa na usumbufu mkubwa licha ya kutakiwa kulipia huduma hizo mapema.
Hata hivyo JAMHURI limefanya mahojiano na Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mtwara,
Mhandisi Fadhili Chilombe, ambaye amekiri kuwapo matatizo ya kukatika kwa umeme mara
kwa mara yanayochangiwa na upungufu wa uzalishaji.
Chilombe amesema mahitaji ya umeme ni makubwa kuliko kiasi kinachozalishwa kutokana na
mashine tisa tu zilizopo katika mkoa huo, huku kila moja ikiwa na uwezo wa kuzalisha megawati
mbili tu.
Amesema mashine hizo ziliwekwa muda mrefu wakati mahitaji yote ya Mkoa wa Mtwara yakiwa
ni megawati kumi tu, lakini kwa sasa mahitaji hayo yameongezeka hadi kufikia megawati 16.
Chilombe, ambaye ni Mhandisi wa Mkoa wa shirika hilo, amesema awali wakati mahitaji ni
madogo iliwalazimu kuendesha mashine sita tu, na sasa mitambo yote iliyopo imelemewa na
mzigo na hicho ndicho chanzo cha kukatika hovyo kwa umeme.
Pamoja na hayo, amesema Serikali tayari imenunua mashine nyingine mbili za kuzalisha
umeme zitakazopunguza mzigo uliopo sasa na kuondoa usumbufu ambao unawakabili
wananchi.
Amesema pia Serikali imefunga mashine Somangafungu ili kuongeza kiasi cha umeme katika
mikoa ya Lindi na Mtwara, huku wilaya za Ikwiriri na Kibiti zitatumia umeme kutoka Mbagala
jijini Dar es Salaam.

“Huo ndiyo mwarobaini wa tatizo hili la umeme hapa Mtwara, katika mpango wake wa muda
mrefu, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) inajenga mtambo wa
kuzalisha megawati 300 katika eneo la Kisiwa na pia ujenzi wa njia ya umeme hadi Somanga,”
amesema.
Amesema mradi huo utakuwa ni ufumbuzi mkubwa wa tatizo hilo, pia amewataka watumiaji wa
umeme mkoani humo kufuata utaratibu na matumizi sahihi ya nishati hiyo ili kuepukana na
kuungua kwa vifaa vyao.
Amesema kitendo cha mtu kuweka umeme kwenye nyumba yake ni uwekezaji wenye gharama,
hivyo wananchi wasitumie kampuni za ukandarasi wa umeme ambazo hazijasajiliwa na kukidhi
vigezo vya Ewura.
Pia amewataka wananchi ambao wanahitaji huduma sahihi za shirika hilo kuonana na msemaji
rasmi badala ya kuwafuata wasiohusika na kujikuta wametapeliwa fedha zao na watu
wanaojifanya wafanyakazi wa Tanesco.