Na Nizar K Visram

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth) ulifanyika mjini Kigali, Rwanda Juni 20 hadi 25, mwaka huu. Mwenyekiti alikuwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Sherehe za ufunguzi wa mkutano ziliongozwa na mwanamfalme Charles akimwakilisha mama yake, Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza ambaye ndiye Mkuu wa Jumuiya hiyo yenye nchi wanachama 54, mengi yakiwa makoloni ya zamani ya Uingereza.

Katika hotuba ya ufunguzi, Charles aliuambia mkutano uliohudhuriwa na wakuu wa nchi wanachama kuwa: “Katika Jumuiya kuna nchi ambazo zimeendelea kuwa na uhusiano wa karibu na familia yangu na kuna nchi ambazo hazina uhusiano huo.”

Alikuwa akizungumzia nchi ambazo zinatawaliwa na malkia na zile ambazo ni jamhuri. 

Akaongeza kuwa kila nchi ina uhuru wa kubakia na malkia kama mkuu wa nchi au kujitangazia jamhuri na kuachana na utawala wa malkia. 

Akasema uamuzi huo unaweza ukafanywa na nchi husika bila ya “chuki wala uhasama.”

Matamshi haya yametokana na matukio ya hivi karibuni katika nchi za Karibiani ambazo zimedhihirisha kutopenda kuwa na malkia kama mtawala wao. 

Tayari nchi hizo zimechukua hatua za kuwa jamhuri zikiongozwa na Rais aliyechaguliwa badala ya malkia au mfalme wa kigeni asiye na asili ya nchi hizo.

Suala la Malkia wa Uingereza kuzitawala nchi za Jumuiya lilijitokeza wakati William, mtoto wa Charles, alipotembelea nchi za Karibiani Machi mwaka huu. Yeye na mkewe Kate walitembelea Belize, Jamaica na Bahamas kwa siku nane.

Suala lilijitokeza tena kwa sababu tangu mwaka 1966 Guyana ilipopata uhuru kutoka ukoloni wa Uingereza, malkia aliendelea kuwa mtawala wa Guyana hadi mwaka 1970 ndipo nchi hiyo ilipoamua kuwa na rais wake kama mkuu wa nchi. 

Guyana ikafuatiwa na visiwa vya Trinidad na Tobago mwaka 1976 na baada ya miaka miwili ikafuata Dominica. Na sasa Kisiwa cha Barbados nacho kimeamua kuwa jamhuri. 

Kisiwa hicho chenye wakazi takriban 300,000 kilijipatia uhuru mwaka 1966 lakini kiliendelea kutawaliwa na malkia.

Karne tatu zilizopita Waingereza walikivamia kisiwa hicho na kuanzisha koloni lenye mashamba ya miwa. Wakawakamata watumwa kutoka Afrika na kuwatumikisha katika mashamba hayo. Sasa baada ya kupata ‘uhuru’ waliamua kutawaliwa na ufalme wa Uingereza, yaani kumtambua Elizabeth kama malkia wao. 

Hata hivyo, baada ya miaka 55, Novemba mwaka jana, Barbados ikaamua kuwa jamhuri na ikamuapisha rais wake wa kwanza, akishuhudiwa na mwanamfalme Charles. 

Sanamu ya Lord Nelson, aliyeunga mkono utumwa na ukoloni, iliyowekwa tangu mwaka 1813 ikang’olewa na kuwekwa katika makumbusho.  

Wakati Barbados inajitangazia jamhuri, wananchi wakaamua kuiondoa sanamu hiyo kwa shamrashamra na vifijo. Waliamua sanamu hiyo iondoke pamoja na malkia. Wananchi wa Barbados waishio Marekani, Canada na kwingineko walishangilia.

Katika hotuba yake, Charles anasema: “Utumwa ulikuwa unyama uliotia doa kubwa na la kudumu katika historia ya Uingereza.” 

Sisi tuliofundishwa historia ya Uingereza shuleni kwa ajili ya mtihani wa Cambridge, hatukuwahi kuambiwa hata chembe kuhusu doa hilo. 

Na huko Belize, siku chache baada ya mwanamfalme William na mkewe Kate kumaliza ziara, serikali ikatangaza bungeni kuwa: “Wakati umefika sasa nasi tuchukue hatua ya kuwa na uhuru kamili.” Uamuzi huo wakaachiwa wananchi.

Tangazo hilo lilikuja baada ya wananchi kuchachamaa wakipinga ziara hiyo ya kifalme. William alipangiwa kutembelea shamba la kakao, lakini hafla hiyo ikafutwa.

Naye Waziri Mkuu wa Jamaica, Andrew Holness, ametangaza kuwa nchi yake itajitangazia jamhuri. Alisema haya wakati kisiwa hicho kilipotembelewa na mwana mfalme William. 

Wananchi wa Jamaica waliandamana wakimwambia mwana mfalme huyo kuwa kwa muda wa karne tatu Waingereza wamewatawala na kujitajirisha kwa kuwatumia wananchi kama watumwa, na sasa wakati umefika wa kujitawala wenyewe. 

Si hayo tu, wananchi wakamwambia wakati umefika kwa wakoloni kuomba radhi na kulipa fidia kwa unyonyaji huo.

Nje ya Ubalozi wa Uingereza, wananchi wa Jamaica walibeba mabango yakisomeka: “Wafalme na wana wafalme wanapaswa kubaki katika vitabu vya historia na wala si katika Jamaica.” 

Wakadai kuwa William aombe radhi. Kwa Kiingereza chao wakamwambia: “Seh yuh sorry!”

Wananchi wakaandika barua ya wazi wakieleza kwa nini Jamaica inapaswa iwe jamhuri na malkia anapaswa kuifidia Jamaica. 

Walisema wafalme wa Uingereza walihusika moja kwa moja katika biashara ya watumwa na wakatajirika kutokana na ukamataji, usafirishaji na uuzaji wa watumwa. 

Kwa mfano, John Hawkins alikuwa mfanyabiashara mkubwa wa watumwa katika karne ya 16. Malkia Elizabeth wa Kwanza aliingia naye ubia kwa kumpa majahazi yaliyotumika kusafirisha shehena za watumwa kutoka Afrika hadi Amerika kaskazini na kusini.

Biashara ikapanuka na ubia wa wafalme ukaendelea chini ya Mfalme Charles wa Pili. Wakaanzisha Kampuni ya Royal Adventurers iliyokuja kuitwa Royal African Company.

Ndipo, kwa mujibu wa jarida la Forbes, aila ya malkia leo hii inamiliki mali za dola bilioni 28 na malkia binafsi anamiliki dola milioni 500.

Canada nako kuna mjadala kuhusu umuhimu wa kuendelea na utawala wa malkia. Kihistoria nchi hii ilianzishwa na wakoloni wa Kiingereza waliopigana vita dhidi ya waliotaka kumaliza ukoloni. 

Matokeo yake waliopinga ufalme wakaasisi nchi ambayo leo ni Marekani (USA) na waliotaka ufalme wakaanzisha Canada. 

Katika sehemu zote mbili hizo wazawa wenye asili ya bara hili (indigenous) wakateketezwa na waliobaki leo wanaishi katika maeneo tengefu (native reserves).

Leo hii Canada ni nchi yenye wahamiaji kutoka kote duniani. Kuna Wachina, Waafrika, Wahindi, Wajerumani na kadhalika. 

Wafaransa wana Jimbo lao la Quebec ambako lugha inayotumika ni Kifaransa. Ndipo watu wanajiuliza nchi hii ina unasaba gani na ufalme wa Uingereza?  Kuna mantiki gani kwa kila kiongozi anayechaguliwa ale kiapo cha utii kwa Malkia wa Uingereza? 

Aprili mwaka huu, asasi ya Angus Reid Institute ilifanya utafiti na matokeo yake ni kuwa asilimia 51 ya Wakanada wangependa waondokane na Malkia Elizabeth. Asilimia 26 walitaka wabaki na malkia na asilimia 23 hawakuwa na hakika. 

Msimamo huo unabadilika wanapoulizwa ikiwa wangependa watawaliwe na mwanawe Charles baada ya kufariki dunia malkia. Asilimia 90 walisema hapana.  

Walipoulizwa kama wanakubaliana na nchi kama Barbados na Jamaica kujitoa kutoka ufalme wa Uingereza, watatu kati ya watano walisema ndiyo.

Jimbo la Quebec liliongoza katika kukataa ufalme. Asilimia 71 ya wakazi wake walitaka nchi iache kutawaliwa na mfalme. Hii inafuatiwa na asilimia 59 katika Jimbo la Saskatchewan

 Utafiti mwingine ulifanywa na Shirika la Habari la Global News Machi 2021.  Asilimia 66 walisema malkia na familia yake wahesabiwe kama “matajiri na watu mashuhuri tu na si vinginevyo.” Kiasi hiki kimeongezeka kwa asilimia mbili tangu mwaka 2020 na asilimia sita tangu mwaka 2016. 

Hata hivyo si rahisi kuuondoa ufalme nchini Canada, kwa sababu kuna mchakato mrefu. Itabidi mabadiliko ya katiba yapite bila ya upinzani katika mabaraza mawili ya bunge la nchi (House of Commons na Senate). Pia itabidi muswada huo upitishwe bila ya upinzani na mabaraza ya wawakilishi katika majimbo yote 10. Bado kuna baraza la wazawa. Hawa waliandikiana mkataba na mfalme wa Uingereza, kwa hiyo itabidi waukubali muswada.  

Mabadiliko haya yanaweza pia yakaibua mabadiliko mengine. Kuna jimbo kama Alberta ambalo linazalisha mafuta kwa wingi. Halafu Quebec nayo inataka kujitenga kutoka Canada kwa sababu wao ni “Wafaransa.”

Mustakabali wa ufalme sasa unajadiliwa hata huko nyumbani Uingereza. Habari za hivi sasa zinasema waziri kiongozi wa Uskoti (Scotland), Bi Nicola Sturgeon, ametangaza kuwa kura ya maoni itapigwa kwa mara ya pili Oktoba mwakani ili kuamua iwapo wananchi wanataka kubaki chini ya muungano wa kifalme (United Kingdom) au wanataka Uskoti ijitenge. 

Sturgeon anaongoza Uskoti yenye wakazi milioni 5.5 chini ya chama chake cha Scottish National Party chenye itikadi ya kujitenga. Serikali yake itaendesha kura ya maoni Oktoba 19, 2023. Amesema atamuarifu Waziri Mkuu wa UK, Boris Johnson. Iwapo Serikali ya UK itapinga, atafikisha kesi mahakamani. 

Kura kama hiyo ilipigwa Uskoti mwaka 2014 na waliotaka kujitenga walipata asilimia 45. Wakati huo ni kwa sababu Waskoti hawakutaka kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya. Sasa UK yenyewe imejitoa kwa hiyo suala hilo halipo tena.

[email protected] 

+1 343 204 8996 

By Jamhuri