Wakazi wa Kijiji cha Picha ya Ndege wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani wamemtaka Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Filberto Sanga, kuwachukua watendaji wa kijiji hicho na kuwapangia kazi sehemu nyingine.

Filberto Sanga, akihutubia mkutano wa hadhara.

Kauli hiyo ilitolewa na mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Bakari Chilumba, aliyesema kuwa watendaji hao wamegeuka kuwa kero na changamoto kubwa kwa wanakijiji.

Kilichotokea ni kuwa watendaji wawili wamepangwa katika kijiji hicho na kila mmoja anajitambulisha kuwa yeye ndiye mtendaji halali na kutaka mwenzake apuuzwe.

“Kila mmoja anadai yeye ndiye mtendaji halali, sasa hii imekuwa changamoto kwa wanakijiji kwa sababu hatujui ni yupi anastahili kutusaidia,” amelalamika Chilumba na kuongeza kuwa wananchi  wamekuwa wakipokea maagizo tofauti kutoka kwa watendaji hao kila wanapokwenda kufuata huduma.

“Cha kushangaza tangu kipindi cha mwaka jana tumeona wafanyakazi wa serikali wameongezeka humu ndani katika ofisi, sijui kama mheshimiwa wewe una makatibu tawala wawili pale katika ofisi yako au kama kuna ‘medical officer’ wawili wa wilaya pale katika ofisi yako au kuna wakurugenzi wa wilaya wawili pale katika ofisi yako. Lakini hapa tuna watendaji wawili, hatumjui mtendaji wetu ni nani, wote wameletwa na serikali na kawaida ya kijiji mtendaji ni mmoja, kuna vijiji vingine havina watendaji, kwa nini asitolewe mmoja akaenda kule? Wanajazana hapa wanaleta jasho tu kwenye ofisi, hii inaleta maana gani?” alihoji mwananchi huyo.

Akaongeza: “Ukifika unaeleza tatizo lako unaambiwa msubiri mtendaji mkubwa… unafika unaeleza tatizo lako unaelezwa mtendaji ameondoka… wakati mwingine tunashindwa kuulizia sana, kwa sababu unaogopa kutiwa ndani kwa sababu wao ni watumishi wa serikali.”

Mtendaji wa Kata ya Vikindu, Shaaban Mponda, amekiri kuwapo kwa changamoto hiyo na kuwataja watendaji hao kuwa ni Hadija Mosha na Rhoda Charge, ambao wanafanya kazi katika ofisi moja. Alisema suala hilo tayari lilikwisha kufikishwa katika ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo.

Jitihada za kumtafuta mkurugenzi huyo ziligonga mwamba lakini Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga, anasema analifanyia kazi na atalipatia ufumbuzi baada ya muda mfupi.

563 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!