Waliokuwa wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), Kampuni ya mizigo Dahaco na baadaye Swissport Tanzania, wamelalamikia uongozi wa kampuni hiyo kwa kushindwa kuwalipa waliokuwa wafanyakazi wake 109, zaidi ya Sh bilioni 15 ikiwa ni malimbikizo ya mishahara na stahiki nyingine kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wastaafu hao wanasema Swissport inawajibika kuwalipa stahiki zao  kwa mujibu wa makubaliano ya awali kabla ya kuinunua kampuni hiyo kutoka Dahaco.

“Wakati tunahamishwa kutoka Dahaco kwenda Swissport uongozi ulisema stahiki zetu zote zitakuwa zikilipwa na mwajiri wetu mpya ambaye ni Swissport,” wanasema.

Wanasema mgogoro wa nani anastahili kulipa stahiki zao ulianza mwaka 1995 baada ya waliokuwa wafanyakazi wa ATC kuhamishiwa Dahaco, hali iliyowalazimu kwenda mahakamani kupata ufumbuzi wa madai yao.

Wanasema katika hukumu iliyotolewa katika Mahakama ya Kazi chini ya Jaji JohnTendwa, iliamuriwa kuwa wafanyakazi wote wanastahili kulipwa haki zao kulingana na makubaliano yao ya awali walipokuwa wakihamishwa kutoka kampuni moja kwenda nyingine.

Katika kesi hiyo Namba 11 ya 1995, Mahakama iliona umuhimu wa wafanyakazi hao kulipwa stahiki zao kwa mujibu wa sheria.

Wamesema Oktoba 1, 2005 kampuni ya Swissport Ltd ilipoanzishwa ilikuwa inamiliki asilimia 51 ya hisa, hivyo haki na stahiki zote za wafanyakazi wa iliyokuwa Dahaco zikahamishiwa katika kampuni hiyo.

Makamu mwenyekiti wa wastaafu hao, Hussein Kilango, amesema utaratibu wa kuwahamisha waliokuwa wafanyakazi wa ATC/Dahaco na baadaye Swissport haukufuata misingi ya kisheria, hali ambayo imeendelea kuleta mkanganyiko kwenye malipo yao.

“Kila tulipokuwa tukihamishwa kutoka kwa mwajiri wetu wa awali ATC/ Dahaco/ hadi Swissport Ltd stahiki zetu zote tulikuwa tukilipwa na kampuni husika, lakini ilipofika muda wa kustaafu malipo yetu yamegeuka kuwa kaa la moto,” amesema Kilango.

Amesema hata wakati wa mchakato wa kuuzwa kwa kampuni hiyo, waliokuwa wafanyakazi hawakupewa uhuru wa kutoa maoni yao na wala hawakuambiwa thamani ya nguvukazi na kwa kiasi gani kampuni iliuzwa.

“Wakati  wa utekelezaji wa zoezi la kuuzwa kwa Dahaco  wafanyakazi walihoji juu ya stahiki zao lakini mwajiri wao mpya Swissport kwa kushirikiana na uliokuwa uongozi wa Dahaco ulisema kuwa stahiki zote zinahamishiwa kwa mwajiri mpya.

“Ilitakiwa wafanyakazi wapewe barua za mkataba kutoka shirika mama la Swissport International ikionesha ajira zao mpya kwa mmiliki mpya, kitu ambacho hakikufanyika,” amesema Kilango.

Amesema ilitakiwa wafanyakazi kulipwa mishahara tofauti na walivyokuwa wakilipwa na mwajiri wao wa awali, Dahaco, kama vile walivyokuwa wakilipwa wenzao wa viwanja vingine kama vile Nairobi, Johannesburg na viwanja vingine vya ndege.

Mweka hazina wa walalamikaji hao, Jamal Mayele, amesema kampuni ya Swissport ilianzishwa na kulinyang’anya Shirika la Ndege la Tanzania majukumu yake na kupewa raia wa kigeni wakishirikiana na mmoja kati ya wakurugenzi wa kampuni mama ya ATC (Dahaco) ambaye alikuja kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Swissport.

“Tulijaribu kuhoji uhalali wa kampuni kuuzwa lakini uongozi ulituambia kuwa haki zetu zitakuwa salama huko tuendako, hali ambayo ilikuwa kinyume,” anasema Mayele.

Anasema hata huo ubinafsishaji haukufanyika kwa lengo la kuinua ufanisi na kuongeza faida kwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali hizi, bali ilichangiwa na tabia ya rushwa ya kutaka asilimia 10 ya faida kutoka kwa watu waliokuwa wakitaka kulinunua shirika hilo.

Anasema ni katika kipindi hiki ATC ilipoanza kuyumba na viongozi  wa Wizara  ya Mawasiliano na Uchukuzi  katika  kitengo  cha usafiri wa anga walipoanza kuuza njia (routes) za kampuni hiyo kwa mashirika mengine  ya ndege na kuilazimisha kuingia kwenye mikataba mibovu ya ushirikiano (joint venture) iliyokuwa na lengo la kulifilisi.

“Katika madai yetu haya Kampuni ya Swissport hawana jinsi ya kukwepa kwa maana hata wakati wanauziwa Dahaco walisema watawajibika kulipa madeni yote ya wafanyakazi.

“Serikali iliangalie suala hili kwa macho mapana ya uzalendo na kwa kuzingatia usalama wa nchi yetu. Kwa kuwa uwanja wa ndege ni mahali nyeti, maadui wa Taifa wanaweza kutumia udhaifu wa watendaji wa kigeni wasiokuwa na uchungu na nchi yetu kuruhusu vitendo visivyo vya kizalendo kutokea,” anasema.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Swissport Tanzania, Mrisho Yasin, amesema ni kweli madai ya wafanyakazi hao ameyakuta ofisini kwake tangu alipoingia madarakani, lakini kampuni hiyo haihusiki na madai yao.

“Hawa watu wengi walikuwa ni wafanyakazi wa iliyokuwa ATC na baadae Dahaco, sasa sisi tunahusika vipi… hapo ni bora wakawafuata hao wanaowadai,” anasema Yasin.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Adelhelm Meru, alipoulizwa anasema malalamiko ya wastaafu hao hayajamfikia ofisini kwake.

“Tuna malalamiko mengi sana kutoka kwa wastaafu wa kampuni mbalimbali wanaowalalamikia waajiri wao wa zamani na tunayafanyia kazi,” amesema Dk. Meru.

Amesema Wizara inafanya juhudi za kupambana na matatizo kama hayo, hivyo anawaomba wahusika wampelekee madai yao kwa maandishi.

1928 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!