Watanzania mbona tunalumbana hivi? Tatizo liko wapi?

Kutolewa kwa ripoti ya kwanza ya makinikia kulizua mjadala mkali miongoni mwa Watanzania; kutolewa kwa ripoti ya pili kumemwaga mafuta ya taa kwenye moto uliyowashwa na mjadala uliotangulia.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi uliofanywa na kamati ya rais iliyoteuliwa na kutoa ripoti ya kwanza, tuliarifiwa kuwapo kwa tofauti kubwa ya thamani ya madini aina ya dhahabu, shaba, na fedha zilizoripotiwa na wamiliki wa makontena 277 yaliyozuiliwa.
Kamati ilisema kuwa thamani ya dhahabu, shaba, na fedha ndani ya makontena hayo ni kati ya Sh bilioni 696 hadi Sh trilioni 1.1727 ingawa wazalishaji wanasema thamani ya madini hayo kwenye makontena ni Sh bilioni 112.1.

Kamati ya pili nayo imeeleza kubaini masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na kampuni ya Acacia Mining kufanya shughuli za uchimbaji wa dhahabu bila kusajiliwa, na kwamba kampuni za uchimbaji, kampuni za usafirishaji na upimaji madini yametenda makosa ya jinai ikiwa ni pamoja na kukwepa kodi, kujipatia mali kwa njia za udanganyifu, kutoa taarifa za uongo, kuhujumu uchumi, na kukiuka sheria mbalimbali nchini.
Si rahisi kusikiliza malumbano yaliyopo sasa bila kuona umuhimu kwa Watanzania kukata shauri kutathmini kwa kina matamshi na hatua zinazoashiria kunufaisha wote, na kuzipima na maneno na hatua ambazo zinakusudia kunufaisha upande mmoja au mwingine katika malumbano ambayo mara nyingi yanawekwa vionjo vya masuala ya kisiasa.

Mwalimu Julius Nyerere, katika kijitabu chakeTujisahihishe anasema: “Kujielimisha ni kutafuta ukweli wa mambo. Kwenda shule hutusaidia. Lakini japo hatuwezi kwenda shule twaweza kujifunza.”
Anaongeza: “Elimu ya kweli ni ujuzi wa sababu za mambo mbalimbali; na kama ni mambo mabaya ni kujua jinsi ya kuyaondoa; na kama ni mema, jinsi ya kuyadumisha.”
Haya maneno aliyaandika kuzungumzia uhusiano wa viongozi, chama, na wananchi wanaoongozwa ndani ya jamii. Kwa upande wa chama na serikali inayoiongoza maana yake iko wazi: upo wajibu wa kurekebisha sera, sheria, na utekelezaji pale inapoonekana kuwa yalifanyika makosa.

Na kama ipo mifano ya serikali za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukubali kuwa haikutafakari vyema athari za uamuzi wake wa kisera, kisheria, na kiutendaji basi uamuzi ambao tunaambiwa serikali itachukua kurekebisha kasoro hizo kutokana na kutolewa taarifa za kamati za kuchunguza biashara ya makinikia, huu ni mfano wa kuigwa wa dhana ya kujisahihisha.
Kwetu sisi wakazi wa Kanda ya Ziwa ambao habari haiwi habari mpaka itoke Radio Free Africa (RFA), labda tatizo la CCM ni kuwa bado hawajasimamisha shughuli za matangazo ya kawaida ya RFA na kututangazia kuwa walifanya makosa. Lakini kwa hali ya kawaida hatuna budi kuamini kuwa zinachukuliwa hatua za kurekebisha kasoro za uamuzi uliopita.

Ripoti ya kwanza ilipowekwa hadharani tulitahadharishwa kuwa kampuni inayotuhumiwa, Acacia, ingetushitaki kwenye taasisi za kimataifa zinazolinda maslahi ya wawekezaji.
Baada ya kutoka taarifa ya pili, tumesikia kuwa mwakilishi wa kampuni ya Barrick Gold Corporation, kampuni ambayo ni mmiliki mkuu wa hisa za Acacia akielezea nia ya kampuni yake kukaa kwenye meza ya majadiliano na serikali ili kufikia mwafaka wenye manufaa kwa pande zote.

Kwa kawaida maneno kama haya yanabeba tafsiri pana sana; yanaweza kuwa utangulizi wa mtu anayetafuta suluhu, lakini yanaweza pia kuwa utangulizi wa mtu ambaye hana nia yoyote ya kutafuta suluhu.
Lakini tunafahamu pia kuwa mtu mwenye imani juu ya uhalali wa madai yake asingefika Ikulu kuongea na Rais Magufuli; angebaki Canada, na kutuma ujumbe kupitia mwanasheria wake kuwa tutakutana mahakamani.
Vilevile hatuwezi kupuuza athari za kibiashara kwa wanahisa kama Barrick, ambayo inamiliki asilimia 63.9 ya hisa za Acacia, za kurefusha mzozo na Serikali. Baada ya ripoti ya kwanza kutolewa, bei ya hisa za Acacia zilianza kuanguka. Baada ya Serikali na Barrick kukubaliana kumaliza mgogoro kwa majadiliano, bei za hisa za Acacia zilianza kupanda. Kipaumbele kilikuwa kurudisha imani ya soko la hisa juu ya shughuli za Acacia, na hili kwa sasa limetimia.
Kama ni kipaumbele pekee kinaifanya Barrick kukubali mazungumzo, au ni kulemewa na uzito wa tuhuma zilizopo kwenye taarifa za kamati mbili si muhimu kupambanua kwa sasa. Muhimu ni kuwa waliokuwa wanagombana (serikali kwa niaba ya Watanzania) wamekubali kuongea na kutafuta suluhu. Serikali iliyokuwa ikilaumiwa kutosikia ushauri, inaelekea kuanza kusikia ushauri. Inajisahihisha. Sasa tatizo liko wapi?
Ukimwambia dereva anayekutoa sehemu moja kwenda nyingine, mwanzo kabisa wa safari, kuwa kwenye makutano ya barabara ya kwanza aende kushoto halafu yeye asikusikie akaenda kulia kama vile amezibwa pamba masikioni, huyo anastahili kuelezwa mpaka aelewe somo.

Dereva kaelewa somo, kageuza gari na, kwa mtazamo wa wengi, anaelekea kule kule ambako ulisema twende. Tutakuelewa kama ukiendelea kumsema kwa kilomita kumi baada ya kugeuza gari ni kwa jinsi gani, kama angekusikiliza, tungeokoa gharama kubwa ya muda na mafuta yaliyopotea. Zikitimia kilomita 100 na somo bado linaendelea kuna baadhi ya abiria wataanza kulala usingizi.
Baadhi ya waliolala wakiamka baada ya kilomita 500 wakakuta mwelekeo ni ule ule na somo halijaisha wataanza kuhoji kama mtoa somo ana nia ya kweli ya kufika huko alikosema twende.
Mimi naamini kuwa sasa tunahitaji raia aliyeundwa upya ambaye, pamoja na kuwa anaweza kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa, anapaswa kuanza pia kuongozwa na ukweli. Tukiweka jitihada ya kujielimisha juu ya masuala yanayogusa maendeleo yetu itakuwa rahisi kwa raia wa kawaida kufikia uamuzi unaoshibishwa na ukweli, badala ya kufuata tu yale tunayoyasikia kwa wale tunaowaunga mkono kisiasa.
Siyo kweli kuwa ipo serikali au chama cha siasa duniani ambacho chenye jibu la kila tatizo linalomkabili mwanadamu. Na hasa kwa sababu hii kuna umuhimu mkubwa sana wa kutoa fursa za wazi na za kweli za kushirikisha wananchi katika michakato ya maendeleo na uundwaji wa mazingira ya kisera, na kisheria yanayosimamia michakato hiyo.

645 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons