Wizara ya Nishati ya Kenya imepiga marufuku gesi ya kupikia kutoka Tanzania kuingia nchini humo. Upigaji marufuku huo umefanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Kenya, mwezi Aprili mwaka huu.
Uamuzi huu wa Kenya ni kinyume na misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania na Kenya ni wanachama. Kwa mujibu wa Itifaki ya Soko la Pamoja, bidhaa za nchi zetu zinaruhusiwa kusambaa ndani ya Jumuiya bila vikwazo.
Kwa mujibu wa Ibara ndogo za 76(1) na 104 (2) za Mkataba wa kuanzisha Jumuiya Afrika Mashariki maeneo ya msingi yaliyohusishwa katika Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Soko huru linasimamiwa na Itifaki ya Umoja wa Forodha na Sheria ya Afrika Mashariki ya Usimamizi wa shughuli za Forodha ya mwaka 2004. Utekelezaji wa Umoja wa Forodha ulianza rasmi mwezi Januari, 2005 na kipindi cha mpito cha miaka mitano cha kuondoa ushuru wa forodha katika biashara ya bidhaa kwa nchi wanachama kiliisha rasmi Desemba 31, 2009.
Kuanzia tarehe 1 Januari, 2010 biashara ya bidhaa zote zinazozalishwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kukidhi vigezo vya utambuzi wa uasili wa bidhaa, zinaweza kusafirishwa kutoka nchi moja hadi nyingine bila kutozwa ushuru wa Forodha hutumika kwa bidhaa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Gesi ya kupikia kuingia Kenya hutokea Tanzania kwa sababu Tanzania ni nchi pekee katika ukanda huu ambayo imewekeza mitambo ya kupokea gesi na kuiweka kwenye mitungi. Kutokana na mfumo mzuri wa kupokea gesi uliowekwa na Bandari ya Dar es Salaam hivyo kuifanya gesi inayotoka Tanzania kuwa na gharama nafuu nchini Kenya kuliko gesi inayoagizwa kupitia Bandari ya Mombasa, Kenya.
Uamuzi wa kuzuia gesi kutoka Tanzania ni uamuzi wenye kulenga kuilinda Bandari ya Mombasa kwa kuvunja mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa kutaka kuifanya Tanzania iendelee kuwa muuzaji wa malighafi kwenda Kenya.
Uamuzi huu wa Serikali ya Kenya hauna lengo zuri kwa nchi yetu, hivyo kuathiri biashara kati ya Tanzania na Kenya ambapo kwa miaka ya hivi karibuni Tanzania imekuwa ikiuza bidhaa nyingi zaidi kwa nchi hiyo.
Ikumbukwe kuwa, viwanda vingi vya Kenya hutegemea malighafi kutoka Tanzania. Kuzuia gesi ya kupikia na kuendelea kuagiza malighafi za kuendesha viwanda vyao ni sera ya Kenya kuifanya Tanzania kuwa chanzo cha malighafi tu na siyo chanzo cha bidhaa zilizoongezwa thamani.

Mbali na hilo, Kenya pia imeipiga marufuku Tanzania kuhusu ununuzi wa ngano, suala ambalo ni kinyume na makubaliano ya biashara ya Afrika Mashariki.
Viongozi wetu wanapashwa kuwa na msimamo thabiti katika kupambana na urasimu huu na mwingine wowote unaofanywa na utakaofanywa na nchi jirani, hasa Kenya, ambao kila mara wamekuwa wakijiita ndugu zetu huku wakitutendea mambo ya ajabu.
Siyo mara ya kwanza jirani zetu hao kuibuka na kauli zenye utata kuhusu nchi yetu. Miaka yote tumeishi maisha ya kuwabembeleza na kuonekana kuwa ni haki yetu kunyanyaswa na jirani zetu hao.
Ifike mahali tukatae kufanyiwa vitimbwi na majirani zetu, kwani nchi yetu ni nchi huru yenye serikali yake. Watanzania tumekuwa tukibezwa na kuonekana hatuna haki kutokana na upole wetu. Ifike mwisho na kurudisha heshima ya nchi yetu.
Serikali ya Tanzania isikubali upuuzi wa aina hii kuendelea. Iwapo Serikali ya Kenya itaendelea na msimamo wake, basi ni wakati wa nchi yetu kuchukua hatua na kuhakikisha hakuna bidhaa yoyote ya nchi hiyo inayoingia nchini hasa maziwa ambayo yamejaa kwenye soko letu.

Ni wakati wa kujinasua kutoka kwenye shamba la bibi na dampo la bidhaa kutoka nje ya nchi na kuanza kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kulinda heshima yetu. Vibweka vya jirani zetu vimekuwa vikiongezeka kutokana na baadhi ya viongozi wetu kuwa na maslahi binafsi.
Sina shaka na Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na dhamira yake ya kulinda rasilimali za nchi pamoja na kuongeza viwanda. Naamini ya kuwa Rais wangu, Dk. John Magufuli, hawezi kufumba macho na masikio pale atakapoona jirani zetu wanatutumia salamu za kichokozi.
Siamini kama hizi ni zama za kumbembeleza jirani mgomvi asiye tayari kuwa jirani mwema, jirani mbinafsi na mwenye nia ya kutuangamiza. Jirani zetu hawa tunapaswa kuwaangalia kwa jicho la ziada maana wamekuwa si wema sana kwetu.
Nashindwa kuyasema ninayopaswa kusema eti kwa vile kuna mambo ya kidiplomasia! Wacha nikomee hapa, ila nitoe tahadhari ya kuwa makini na majirani zetu hawa ambao si majirani wema kwa nchi yetu.

Mungu Ibariki Tanzania.

Na Angela Kiwia
0715 446 194

981 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!