Watanzania tunahitaji kuongeza uelewa wetu wa sheria

Kwa siku chache juma lililopita nimetoa darasa fupi juu ya sheria ya kutunza kumbukumbu za waasisi wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Sheikh Abeid Amani Karume. Hii sheria inajulikana kwa Kiingereza kama Founders of the Nation (Honouring Procedures) Act 2004. Sijaona tafsiri yake kwa lugha ya Kiswahili.

Madhumuni ya msingi ya sheria hiyo ni kuweka taratibu za namna ya kuenzi na kutunza urithi wa kihistoria wa waasisi wawili wa Tanzania. Ni sheria ambayo haijulikani sana, na ni sheria ambayo inakiukwa mara kwa mara.

Si vigumu kubaini sababu za msingi za sheria hii kutofahamika kwa Watanzania. Yapo makosa mengi makubwa yanayolikabili Taifa; kama ujambazi, ujangili, na ufujaji wa mali ya umma, na ni makosa ambayo yanajulikana vyema kwa polisi na waendesha mashitaka kuliko makosa yaliyaoainishwa ndani ya sheria hii.

Sheria yoyote ngeni inachukua muda kueleweka vyema kwa waliopewa mamlaka ya kufungua mashitaka. Nimegundua hayo hivi karibuni nilipojaribu kufungua mashitaka dhidi ya mtu ambaye, kwa maoni yangu, alikuwa amekiuka makosa chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015. Mimi ndiye nilikuwa nawaelimisha polisi juu ya yale ambayo niliyaona kuwa makosa kwa mujibu wa sheria hiyo.

Mwanamuziki mashuhuri,  Diamond, amejiingiza kwenye malumbano na baadhi ya wanajamii baada ya kutumia picha ya Mwalimu Nyerere kwenye kasha la wimbo wake mpya, Acha Nikae Kimya. Diamond analaumiwa kwa kutumia picha ya Mwalimu kwa ujumbe ambao mwanamuziki huyo anauwasilisha kwenye wimbo wake.

Sijausikiliza wimbo wote kwa hiyo sitazungumzia maudhui yake, ila nilichoona awali kabisa ni kuwa Diamond amekiuka kipengele cha sheria kinachokataza kutumika kwa picha za waasisi wa Tanzania kwa manufaa ya kibiashara. Wanaokutwa na hatia wanaweza kutozwa faini isiyozidi Sh milioni 5, au kutumikia kifungo kisichozidi miezi 12, au kutozwa faini pamoja na kutumikia kifungo.

Wengi wetu tunakiuka sheria bila kufahamu, na tatizo halipo tu kwa raia, bali, kama nilivyobainisha, hata kwa baadhi ya maafisa wa Serikali. Yapo makosa ya kila siku tunayoyasikia kwenye vyombo vya habari, lakini hutasikia mtu kukutwa na hatia kwa kuuza fulana yenye picha ya Mzee Karume.

Nilimwambia mmiliki wa duka mmoja mjini Musoma ambaye alikuwa anauza fulana zenye picha ya Mwalimu Nyerere kuwa anakiuka sheria, lakini baada ya kushangaa sana akanijibu kuwa hiyo ni sheria ambayo watu wengi hawataikubali.

Jibu la aina hii linaibua masuala mawili ya msingi. Kwanza, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume ni viongozi ambao wanaonekana kuwa ni mali ya Taifa kwa maana ya msingi kabisa. Kwamba ni watu ambao kila Mtanzania anayo haki kuwatumia kwa namna anavyoona sahihi. Hawa si mali ya Serikali, au ya familia zao.

Ninao mfano mzuri wa msimamo wa aina hii kwa mtu ambaye alidurusu nakala za kitabu kimojawapo cha Mwalimu Nyerere na akanieleza anaamini anayo haki ya kukigawa kwa watu bila kupata idhini ya familia ya Mwalimu Nyerere.

Kwa upande mmoja msimamo huu una manufaa katika kuhuisha masuala yale muhimu na yenye manufaa kwa jamii ambayo tunayahusisha na waasisi wetu.

Pili, jibu hili linadhihirisha ni jinsi gani baadhi yetu hatuoni umuhimu wa kufuata sheria, hata kama tunakiri kuwa ziko sheria nyingine ambazo hatuzipendi au kukubaliana nazo. Ipo hoja ya kutosha ya kupinga sheria ambazo zinakiuka haki zetu za msingi, lakini sikubali kuwa kutumia picha za waasisi kwa manufaa ya kibiashara ni mojawapo ya haki hizo.

Ndiyo maana naamini bado upo umuhimu wa kuwapo kwa sheria hii. Tanzania bado haijafikia ngazi ya Marekani, ambako mtu anaweza akashona ‘nguo ya ndani’ kwa kutumia bendera ya Marekani na kuivaa au kuiuza bila tatizo lolote na sheria zikamlinda kwa kufanya hivyo.

Sheria zinaakisi mila na desturi zetu, na zuio la kutumia picha hizi kwa masuala ya biashara ni njia mojawapo ya kulinda hadhi ya watu ambao tunawaenzi ndani ya jamii.

Jiji la Dar es Salaam lilipopitisha uamuzi wa kubadilisha jina la Barabara ya Pugu na kuiita Barabara ya Nyerere, Mwalimu Nyerere alipinga mabadiliko hayo, akisema kuwa wasubiri mpaka afe ndiyo wafanye uamuzi wa aina hiyo. Hawakumsikiliza.

Namkubalia kuwa tumuamulie wakati hayupo, ingawa hakuna uhakika kuwa tutaafikiana. Kwangu mimi hata isingekuwepo sheria inayokataza kutumia kumbukumbu za waasisi kwa masuala ya kibiashara, bado naamini isingekuwa sahihi kufanya hivyo.

Labda ipo siku sheria zitalinda haki ya Mtanzania kubuni ushonaji na uuzaji wa chupi za Muungano, ambazo zitakuwa na picha za waasisi wetu wawili, lakini hiyo siku bado haipo jirani na tuwaombee busara viongozi wa wakati huo kuwa jambo hilo lisiruhusiwe.

Kuepuka aliyoyafanya Diamond ni muhimu sheria hii itangazwe sana ili kujulikana kwa wengi. Mimi naifahamu vyema hii sheria kwa sababu tu nilishiriki kwenye kamati iliyochangia mawazo ya muswada wa sheria yenyewe na ni mjumbe wa bodi iliyoundwa kusimamia kumbukumbu za waasisi hawa baada ya sheria kupitishwa.

Mwito wangu kwa Serikali ni kutenga pesa za kutosha kwenye bajeti kila mwaka kuhakikisha kuwa majukumu ambayo bodi yetu inayo, ambayo ni pamoja na kuwaelimisha watu juu ya uwepo wa sheria hii, yanatekelezwa kwa ukamilifu.

Elimu zaidi kwa raia itaongeza ufahamu wao wa sheria, itatupunguzia muda wa malumbano, na kutuongezea Watanzania muda wa kufanya kazi.

392 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons