Wauza ‘unga’ wabuni mbinu

Wafanyabiashara haramu ya dawa za kulevya nchini wamebuni mbinu mpya za kukwepa kukamatwa na vyombo vya dola wanapofanya biashara hiyo, JAMHURI limebaini.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebainisha kuwa wafanyabiashara wamefikia hatua hiyo kwa nia ya kusafirisha ‘mizigo’ bila kukamatwa.

Kwasasa wanasafirisha dawa za kulevya kwa kuzichomekwa kwenye nepi za kutupa (pampers) na taulo za kike (pads).

Vyanzo vya habari vimesema wauza unga wamebuni njia hiyo isiyotiliwa shaka na vyombo vya dola na hivyo kuwa rahisi kwao kusafirisha ‘unga’ bila kubughudhiwa.

“Ni vigumu kushtukia mzigo unapokuwa umewekwa vizuri kwenye pedi au pampers na kufungwa upya. Tumekuwa tukifanya hivi na hakuna mtu anayeweza kudhani kama tumebeba unga,” anasema mmoja wa watu wanaofanya biashara hiyo wakati akimfunda mwenzake eneo la Kinondoni mwishoni mwa wiki.

Inaelezwa kuwa wamelazimika kutumia njia hiyo ambayo ni vigumu kubaini uwepo wa unga katikati yake ukiwekwa.

“Katika pedi kuna dawa ambayo huwekwa kuitunza. Tunapofumua tunahakikisha karatasi ya juu ya nailoni hatuigusi zaidi ni kuchomoa pamba ya katikati na kuweka unga uliofungwa vizuri kuuchomeka eneo ilikotolewa pamba, kisha tunachukua gundi maalum na kurudishia eneo lililokuwa na pamba,” anasema binti mrembo bila kufahamu kuwa JAMHURI linamsikiliza .

Anasema wanavyopakia unga kwa kutumia njia mpya si rahisi kukamatwa au kubainika katika mashine za ukaguzi zinazotumika kukagua mizigo katika viwanja vya ndege nchini.

Anaeleza kuwa baada ya kufungwa vizuri, hulazimika kuhakiki usalama wa mzigo kwa kuupitisha katika mashine maalumu kabla ya kuusafirisha.

Mashine imekuwa ikitumiwa kuhakiki usalama wa mzigo (unga) uliofungashwa kitaalam usibainike katika nchi husika na kurahisisha usafirishwaji wake.

“Kabla mzigo haujasafirishwa unafungwa vizuri na kupitishwa kwenye mashine hiyo ili kuhakiki usalama wake. Iwapo kutakuwa na shaka ya kubainika kwake, basi unafunguliwa na kufungwa upya na kuupitisha tena kwenye mashine. Ukishaonyesha kuwa uko sawa ndipo unaposafirishwa,” anamwambia mwenzake.

Imeelezwa kuwa kutokana na ufungashaji madhubuti wa dawa za kulevya na kuhakikiwa na mashine, ni vigumu kuzibaini kutokana na utaalam unaotumika.

“Ukweli ni vigumu kutambua kilichomo ndani ya huo mzigo baada ya kuufunga na kuupitisha kwenye mashine, hivyo mashine hiyo inarahisisha kusafirisha mzigo bila kuwa na shaka ya kukamatwa kama hapo awali,” Anatamba.

Pia imeelezwa kuwa katika ufungaji wanatumia karatasi za kurudufisha (carbon papers)ambazo husaidia kuficha kilichomo ndani ya mzigo.

“Ipo mizigo inayofungwa kwa kutumia carbon papers ambazo ni vigumu kubainisha kilichomo ndani, ingawa mingine hunyunyiziwa marashi maalumu ambayo mbwa wanaotumiwa kunusa hawawezi kubaini lolote,” anasema Dada mrembo wakiwa katika salon ya kike wakirembeshana nywele.

Akizungumza na JAMHURI, Kamanda wa Kikosi cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, ACP Mihayo Msikhela amesema kwani imekuwa mara ya kwanza kusikia mbinu hizo kutumika nchini.

Anasema anachofahamu ni kwamba mbinu hizo zimekuwa zikitumiwa nje ya Tanzania, lakini si jambo la ajabu kuona zimeanza kutumika nchini.

Amesema kinachohitajika ni umakini wa askari waliopo katika mashine za mizigo kwa viwanja vya ndege.

“Nimesoma kupitia mitandao kuwa nchi za wenzetu wameanza kutumia mbinu hizo, lakini jambo la muhimu ni umakini wa askari walio kwenye mashine za ukaguzi. Kwa hapa nchini bado hatujamkamata mtu yeyote anayetumia njia hii mpya, ila mashine zetu za ukaguzi ziko vizuri sana,” anasema Kamanda Mihayo.

Anabainisha kuwa changamoto kubwa iliyopo katika kukabiliana na usafirishaji wa dawa za kulevya ni mipaka ya nchi kuwa wazi na kutokuwa na mbwa wa kutosha wanaoweza kubaini dawa hizo.

Kuhusu wauza unga kumiliki mashine za kukagua mizigo, amesema wafanyabiashara hao haramu wanaweza kumiliki hizo mashine kutokana na kuwa na uwezo mkubwa kifedha na njia wanazobuni kukwepa mikono ya dola.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani,Hamad Masauni  hakutaka kuzungumzia suala hili kwa maelezo kuwa yuko kwenye kikao hata baada ya kutafutwa kwa zaidi ya wiki mbili ofisini kwake na kuachiwa ujumbe wa maandishi

Wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kurahisisha usafirishaji wa ‘unga’ ambapo mwaka 2012 walikuwa wakiwatumia wanawake wajawazito kusafirisha dawa hizo bila kukamatwa.

Wajawazito walisafirisha ‘unga’ bila kukamatwa kutokana na mashine za ukaguzi kushindwa kutambua dawa za kulevya zaidi ya kuonyesha kiumbe kilichopo tumboni kwa mwanamke husika.

Walifanikiwa kuwatumia wajawazito kutokana na kutoruhusiwa kupita katika mashine mara kwa mara wakaanza kuwashawishi mabinti kushika mimba kwa ajili ya kusafirisha dawa hizo.

Pamoja na kutumia wanawake wajawazito, pia walibuni mbinu ya kutumia mabarafu na sigara.

Kumekuwa na idadi kubwa ya Watanzania wanaokamatwa na dawa za kulevya ambao wapo katika magereza mbalimbali nje ya nchi.

Taarifa zinaonyesha kuwa Watanzania 176 wanatumikia vifungo katika magereza mbalimbali nchini China, huku asilimia 99 wakiwa wamekamatwa kwa dawa za kulevya.

 Takwimu zilizotolewa na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, zinaonyesha kuwa Watanzania 103 wamekamatwa nchini Brazil kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, huku wengine 132 wakikamatwa katika nchi nyingine, ikiwamo Pakistan.

Pia wafanyabiashara hao wameelezwa kutumia fukwe za baadhi ya hoteli kubwa za kitalii jijini Dar es Salaam kuingiza dawa za kulevya nchini.

Waharifu wamekuwa wakitumia fukwe hizo kutokana na kutotiliwa shaka na vyombo vya dola hivyo kuwa rahisi kuingiza ‘unga’ bila kubughudhiwa.

“Ni vigumu kushtukia mambo yanayofanywa katika fukwe ambazo zipo katika hoteli za kitalii. Huko wamekuwa wakiingiza mizigo ya ajabu ajabu huku vyombo vya dola vikiwa havijui lolote,” anasema mmoja wa watu waliohojiwa ambaye ni mfanyakazi wa moja ya hoteli za kitalii jijini Dar es Salaam.

Mizigo mingi, haramu na halali husafirishwa kwa kutumia boti ambazo hutia nanga karibu na hoteli na kushusha mzigo bila kushtukiwa.

“Mfano mzuri ni hotel ya (jina linahifadhiwa). Hoteli hii imekuwa kichochoro cha bidhaa hatari nchini. Watu wanafanya yao bila kujali kuwa kuna dola Unga umekuwa unapita kila mara. Ndiyo njia yao kuu, lakini hakuna mtu anayeshtukia hata.

 “Ukifika pale ufukweni ukakaa tu, utaweza kuona watu wanakuja na boti yao, wanashusha mzigo halafu kuna watu wanakuwa wamekaa hotelini wanawasubiri. Wakishafika wanachukua mifuko yao na kuweka katika mifuko na kuondoka tena kwa kupita hapo hapo hotelini Hii ni hatari kwa usalama wa nchi na hoteli husika,” anasema.

Taarifa zinaonyesha kuwa hivi sasa wahalifu wamekuwa na mazoea ya kutumia fukwe bila hofu yoyote jambo ambalo si la kawaida.

Tangu ameingia madarakani, Rais John Magufuli alitangaza kupambana na dawa za kulevya na wengi wanaamini hata hao wanaofanya siku zao zinahesabika. “Ninavyomfhamu Rais Magufuli hawa dawa yao inachemshwa. Hii hoteli kama ilifunguliwa kuwezesha uuzaji wa unga mwisho wao umewadia,” anasema.

2001 Total Views 3 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons