Mbunge Musukuma adaiwa hotelini Arusha

NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
 
Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku (Musukuma) ameingia matatani akidaiwa kukaidi kulipa pango la hoteli mkoani Arusha.
Habari za uhakika kutoka katika hoteli inayomdai Msukuma, zinasema Kasheku anadaiwa Sh 680,000 ambazo kati ya hizo, Sh 500,000 ni kwa ajili ya malipo ya vyumba alivyokodi yeye na wageni wake; na Sh 180,000 ni za vinywaji vya aina mbalimbali. Jina la hoteli hiyo tunalihifadhi kwa sasa.
Imeelezwa kuwa mbunge huyo aliingia gharama hizo tangu Februari mwaka huu alipokuwa kwenye harakati za kampeni za uchaguzi mdogo mkoani Kilimanjaro na maeneo mengine ya Mkoa wa Arusha.
Taarifa za kudaiwa kwake zimetolewa kwa JAMHURI na mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo ambao wanakatwa mishahara kufidia hasara hiyo.
“Mshahara tunaopata ni mdogo, hali ya maisha ni ngumu, sasa pamoja na hali ilivyo bado tunakatwa ili kulipa deni ambalo halituhusu. Tuliponzwa na imani yetu kwake kwa sababu ni mbunge. Tunampigia simu anafoka na kutukaripia,” amesema mmoja wa watumishi hao.
Kasheku amezungumza na JAMHURI kwa simu na kusema anachojua hadaiwi kwa sababu hizo fedha alishawapelekea wahusika kwa kutumia M-Mpesa.
“Mimi ni mteja wao wa siku nyingi, kama hao barmaid (wafanyakazi wa hoteli wa kike) ndio wanasema hayo maneno basi wewe andika halafu wote niwapeleke mahakamani.
“Mimi sishughuliki na barmaid, nashughulika na mwenye hoteli, siwezi kutuma hela kwa barmaid, sihitaji kushirikiana nao; na wala sihitaji kukuambia kama nimelipa au sijalipa, lakini najua nilishalipa kwa M-Pesa,” amesema Kasheku kwa ukali.
Kasheku ni miongoni mwa wabunge wa CCM wanaotajwa kuwa na hali nzuri kifedha akiwa anajihusisha na ufugaji, kilimo, madini na biashara mbalimbali.
Alipata umaarufu mkubwa mwaka 2015 alipotua kwa helikopta katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Edward Lowassa, alipokuwa akitangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM. Hata hivyo, baadaye wakati wa kampeni Lowassa akiwa Chadema, aligeuka na kumshambulia kwa maneno makali.
Kumekuwapo matukio kadhaa ya wabunge kudaiwa na watu binafsi na taasisi mbalimbali nchini. Baadhi ya malalamiko yamekuwa yakifikishwa katika Ofisi ya Spika na vyombo vingine vya kisheria kuwabana wabunge waweze kulipa.
Januari, mwaka huu Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara (Bwege), amefikishwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Lindi akituhumkiwa kutolipa deni la Sh milioni 12 analodaiwa na Hamisi Kaudunde tangu Februari 28, 2016.
Deni hilo lilitokana kwa kuuziana viwanja saba vyenye thamani ya Sh milioni 42, ambazo kati ya hizo, Sh milioni 30 zilishalipwa tangu mwaka juzi. Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Lindi, Said Wambili alisema kesi hiyo namba 50 ya mwaka 2017, ilifunguliwa Oktoba mwaka jana.
Mwenyekiti huyo alisema kwa mkataba waliokubaliana baina yao, Kaudunde na Bungara, mbunge huyo alitakiwa ifikapo Februari 28, 2016 kiasi kilichosalia Sh milioni 12 kiwe kilishalipwa.
Alitaja viwanja hivyo kuwa viko katika barabara ya Nangurukuru Kilwa Masoko. Namba za viwanja hivyo ni 17(A), 18 (A), 19(A), 19(1A), 22(A), 23(A) na 24(A), vyote vina thamani Sh milioni 42.
Kwa upande wake, Bungara alithibitisha kununua viwanja hivyo kwa kiasi hicho cha fedhana kudaiwa Sh milioni 12.
Alisema alisita kumalizia deni hilo baada ya kubaini kuwa viwanja hivyo havikupimwa.
Mwezi huu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amempa Mbunge wa Kwimba, Shanif Mansoor, siku saba awe amelipa deni la Sh milioni 529 za kodi ya ardhi anazodaiwa tangu mwaka 2010

 SOMA GAZETI LOTE LA JAMHURI HAPA

4627 Total Views 40 Views Today
||||| 7 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons