Wazawa wawezeshwe kumiliki migodi

Wiki iliyopita Tanzania ilipiga hatua kubwa na ya kihistoria katika sekta ya madini nchini, baada ya kushuhudiwa utiaji saini wa mikataba kati ya serikali na kampuni za kimataifa.

Mikataba hiyo yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1 inatarajiwa kuchochea na kuchagiza ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja katika maeneo husika na kwa taifa zima.

Hii huenda ni mara ya kwanza kwa mikataba mikubwa kama hii kusainiwa hadharani tangu kuanza kwa uchimbaji mkubwa wa madini (migodi) nchini zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Ikumbukwe kwamba taifa limewahi kutumbukia kwenye malumbano makubwa baada ya kuibuka kwa madai kuwa Mkataba wa Mgodi wa Buzwagi ulifanyika kwa usiri mkubwa, kukidaiwa kuwapo kwa harufu ya rushwa.

Kwa kuwa safari hii mikataba imesainiwa mbele ya kamera za waandishi wa habari, ni matumaini yetu kwamba haitasababisha kuibuka kwa malumbano ya aina yoyote na italeta tija kwa taifa.

Inafahamika kwamba uwekezaji katika migodi mikubwa ya madini kama dhahabu huhitaji uwekezaji mkubwa wa mabilioni ya fedha, suala linalowatupa nje ya ushindani wawekezaji wazawa.

Mbali na kuhitajika uwekezaji wa aina hiyo, bado mwekezaji huhitaji muda mrefu kabla ya kuanza kupata faida, kwa hiyo ni lazima kampuni husika iwe na ukwasi wa kutosha kuweza kuanzisha migodi mikubwa.

Hata hivyo, ipo migodi mingine ya kati ambayo inaweza kuendeshwa na Watanzania wazawa ama kwa kusaidiwa na serikali au kwa kukopeshwa na taasisi za fedha za ndani na nje ya nchi.

Kwa mfano, wakati Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani ikipambana kuwainua wananchi kiuchumi, upo mgodi wa madini aina ya kaolin (dongo jasi) uliopo huko ambao umesimama kazi kwa miongo takriban mitatu sasa.

Madini ya dongo jasi hutumika kutengenezea vyombo vya udongo, ‘tiles’ na vifaa vingine vya ujenzi vinayohitajika sana kwa sasa ndani na nje ya nchi, huku eneo la Kisarawe likitajwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini hayo.

Pugu Kaolin Miners Ltd., inamilikiwa na wazawa na kwa kuwa wameonyesha nia ya kuendeleza machimbo ya kaolin nchini, ni vema serikali ikajipanga na kuwasaidia waweze kuwa mfano na kuonyesha njia kwa wazawa.