WAZIRI MKUU AKAGUA MRADI WA USAMBAZAJI MAJI

Bomba la maji likiwa tayari kwa kukingwa maji
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Akinga maji
Waziri Mkuu akimtwisha ndoo ya maji mmoja wa mkazi wa eneo ilo

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua mradi wa usambazaji wa maji kwenye vijiji vinavyopitiwa na mradi wa maji Mbwinji na ameridhishwa na unavyoendelea.

Mradi huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea (MANAWASA) unatarajiwa kukamilika Machi 31, 2018.

Waziri Mkuu alifanya ukaguzi huo jana (Alhamisi, Machi 01, 2018) katika kioksi cha kuchotea maji kilichopo kwenye kijiji cha Mbecha wilayani Ruangwa.

“Huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo vijiji vyote vitapata maji”.

Waziri Mkuu alisema vijiji ambavyo vimenufaika na mradi huo wilayani Ruangwa ni sita ambavyo ni Chiyapi, Nandanga, Ipingo, Lucheregwa, Litama na Mbecha.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote yenye ctatizo hilo nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MANAWASA Mhandisi David Mwamsojo alisema mradi huo utagharimu sh. milioni 870.738 hadi kukamilika.

Alisema mradi huo unahusisha vijiji 12 vilivyo kwenye umbali wa kilomita tano kutoka kwenye bomba kuu pamoja na ujenzi wa vioksi 18 vya kuchotea maji.

Mhandisi Mwamsojo alisema hadi sasa tayari kazi ya ulazaji mabomba na kuweka vituo 16 vya kuchotea maji katika vijiji 11 vinavyonufaika na mradi huo imekamilika na wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji.

Alitaja vijiji hivyo kuwa ni Mtepeche, Magereza, Mailisita, Mkotokuyana na Naipanga vya wilaya ya Nanchingwe na Chiyapi, Nandanga, Ipingo, Lucheregwa, Litama na Mbecha vya wilaya ya Ruangwa.