Waziri Mkuu anena


RUANGWA

Na Deodatus Balile
 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa, amevunja ukimya dhidi ya watu wanaomsakama mitandaoni wakidai anataka kugombea urais mwaka 2025, akiwataja kuwa watu hao wana nia ya kumchafua na kuvuruga utulivu na kasi ya maendeleo yanayopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, JAMHURI limeelezwa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na JAMHURI, mahojiano maalumu ya kwanza, Januari 1, 2022 nyumbani kwake kijijini Nandagala – Ruangwa, Waziri Mkuu Majaliwa amesema: “Mimi ni Mjumbe wa Kamati Kuu, nafahamu utamaduni wa CCM, nina akili timamu, ninajitambua, nina heshimu mamlaka iliyopo juu yangu na mahusiano miongoni mwetu. Kama chama tunao utaratibu kuwa yeyote anayepata urais, huwa anatumikia vipindi viwili. Utamaduni huu tunaendelea nao kwa Mheshimiwa Rais Samia, sitarajii mwana-CCM yeyote mwaka 2025 achukue fomu ya kugombea urais.”
Alipoulizwa mbona anatajwa sehemu mbalimbali hata kwenye mitandao ya kijamii kuwa anajiandaa kugombea urais kwa kuunda mtandao wa kufanikisha hilo, akasema: “Huo ni mkakati wa kuchafuana unaofanywa na baadhi ya vikundi vya watu wasiofahamu watendalo. Hawa ni wanaokwazwa na utendaji wangu, hivyo wanaona watumie njia hiyo ya kunichafua. Kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, mimi wala sijawahi kuwaza kugombea urais. Sijawahi kuwa na mpango huo kabisa. Mwaka 2025 mgombea wetu CCM ni Rais Samia tu.
“Chama hakiwezi kuruhusu wana-CCM waparurane kugombea nafasi ambayo ina utaratibu wake uliokomaa na mgombea anafahamika, ana uwezo na anatosha.   Chama kikiruhusu watu kumpinga Rais aliyeko madarakani, jambo ambalo halijawahi kutokea na halitatokea, hawa wenye nia ya kugombea urais wanaowasingizia wengine nia hiyo, wataishia kuchonganisha watu, kuendeleza majungu, chuki na dharau, ambapo utaratibu huu wa kuchafua watu wasio na hatia ukiendelea, utavunja moyo kwa watumishi bora na wachapa kazi ndani ya serikali na chama. Naamini CCM haitaruhusu hilo litokee.”
Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza: “Namuunga mkono Mheshimiwa Rais, amenipa heshima ya kufanya naye kazi kama msaidizi wake, na siku zote kama msaidizi nitatumika kwa niaba ya mkuu wangu. Yote ninayofanya mimi kama Mtendaji Mkuu wa Serikali nafanya kwa niaba ya Mheshimiwa Rais. Nafanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 na kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, kwa ajili ya maendeleo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 “Mimi kama Mtendaji Mkuu wa Serikali, nafuatilia maagizo, maelekezo, usimamizi wa bajeti ya serikali, utendaji wa watumishi wa ngazi zote mpaka kijijini kwa kumsaidia Rais, kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango, ufanisi, gharama halisi na fedha zinafanya kazi zilizokusudiwa bila kuchepushwa. Hivyo, wachafuaji kwa makusudi wanapotosha kuwa ninapokuwa leo niko Mwanza, kesho Tanga, Lindi, Kagera, Dodoma au Rukwa, wanasema nafanya kampeni za kugombea urais, hapana. Nakuwa nasimamia Ilani ya CCM kwa niaba ya Serikali, na unaposema Serikali maana yake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeko madarakani kwa sasa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.”
Waziri Mkuu Majaliwa ameliambia JAMHURI kuwa tafsiri potofu inayopenyezwa na baadhi ya vikundi vya watu wanaotamani urais, wakiashiria kuwa mtumishi anayefanya kazi na kufuatilia kwa karibu utendaji wa serikali anakuwa anajipitisha kwa wananchi, isipodhibitiwa, Tanzania itashindwa kupiga hatua nzuri katika maendeleo: “Maana kila mtu ataogopa kufanya kazi kwa kudhani akionekana huku na kule watu watatafsiri kuwa anatafuta uungwaji mkono. Hili mimi nasema kuwa dhamira yangu ni safi, naamini halitanirudisha nyuma. Nitaendelea kufanya kazi, kuhakikisha Mama Samia anaendelea kupata mafanikio makubwa kama anavyoendelea kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa sasa.”

Majaliwa ameongeza kusema: “Nikiwa mjumbe wa Kamati Kuu nachukua fomu ya kugombea urais kwa chama gani wakati mwenyekiti wangu anagombea?  Naichukua kutoka mikono ya nani? Ananijadili nani? Na je, nitaomba kura kwa nani atakayeniunga mkono?” anauliza!!!!”
JAMHURI lilipomuuliza taarifa zilizosambaa mitandaoni na sehemu mbalimbali za vijiwe vya siasa kuwa yeye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndiye yuko nyuma ya mpango wa Shule ya Uongozi, amesema: “Huo ni kati ya uzushi na uchonganishi  unaoendelea kufanywa na watu wachache wenye nia ovu ya kutafuta madaraka kwa hila. Wanatafuta mtu wa kumsingizia wakidhani itawasaidia wao kupata wanalolitafuta. Mimi nafanya kazi ya utumishi katika nafasi yangu kwa moyo safi na kwa mujibu wa Katiba na Miongozo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/2025.   Sijawahi kuwaza na sina mpango wa kushiriki harakati zozote nje ya majukumu yangu ya msingi na maelekezo ya mamlaka. Kubwa ninaloamini, hata hao wanaopita huku na kule wakinichafua, wanapaswa kufahamu kuwa nafasi za uongozi wa watu zinatoka kwa Mwenyezi Mungu.
Ametoa wito kwa wana-CCM: “Wana-CCM ni lazima tushikamane tuilinde Katiba yetu. Tunayo mifumo na maadili ndani ya chama chetu. Tuendelee kushikamana, chama chetu kipate ushindi mkubwa kupitia Rais wetu, Samia Suluhu Hassan… sitarajii kabisa kuona mwana –CCM anachukua fomu mwaka 2025.”
 
Miradi ya maendeleo


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anasema miradi mikubwa ya maendeleo inaendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa katika Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kiwango ambacho kufikia 2025 yote yaliyoahidiwa ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM au ahadi za mgombea, yatakuwa yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
“Miradi inaendelea vizuri sana. Barabara zinajengwa, madaraja likiwamo la Busisi – Kigongo Feri yanaendelea kujengwa, mradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere unaendelea kwa kasi kubwa. Ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea kwa kasi kubwa na juzi tu, tumeshuhudia Rais Samia akishuhudia utiaji saini wa kipande cha tatu (Lot 3) kutoka Makutupora hadi Tabora, kipande ambacho ni cha msingi katika kuunganisha Reli ya Kati na mengine mengi.
“Katika afya vinajengwa vituo vya afya kila kona ya nchi hii. Elimu, nafurahi sana kuona watendaji katika ngazi ya mkoa na wilaya walivyosimamia kwa ufanisi ujenzi wa madarasa 15,000 ya shule za sekondari na madarasa 3,000 ya shule za msingi, ambayo yametokana na mkopo wa Sh trilioni 1.3 alioupata mama yetu Rais Samia. Mkopo huu umeondoa kero ya wazazi kubanwa kujenga madarasa kila mwaka na sasa wanafunzi wetu wote waliofaulu mitihani ya darasa la saba wataingia sekondari moja kwa moja bila kusubiri kama ilivyokuwa huko nyuma… kwa kweli Mheshimiwa Rais Samia anafanya kazi kubwa na nzuri na sisi wasaidizi wake, tupo kusimamia miradi hii kwa niaba yake.”
Amesema Novemba, mwaka jana kipande cha reli ya SGR kati ya Dar es Salaam na Morogoro kilikuwa kimekamilika na mkandarasi alikuwa anamalizia kipande kidogo cha kati ya Dar es Salaam na Pugu. 

“Na mimi mwenyewe nimefanya majaribio ya kupita mara mbili hadi Morogoro na Kilosa, tukapita kwa ufanisi mkubwa,” amesema. 

Alipohojiwa kwamba mbona treni ya SGR haikuanza kazi Novemba mwaka jana kati ya Morogoro na Dar es Salaam, kama ilivyotangazwa awali, akasema:
“Nchi ambayo tulikuwa tumeagiza mabehewa iliathiriwa sana na corona. Serikali yake iliweka watu wake chini ya lockdown. Kutokana na hilo, viwanda karibu vyote vilifungwa, kikiwamo hiki kinachotengeneza mabehewa ya reli yetu ya SGR. Hawakutengeneza mabehewa au vichwa vya treni kwa wakati kama tulivyokuwa tumekubaliana. Huwezi kuwalaumu, maana hata mikataba tunayoingia inakuwa ikitambua kuwa yakitokea majanga ya asili kama haya, ucheleweshwaji kama huu unaweza kutokea na ndivyo corona ilivyochelewesha mpango wetu wa kuzindua reli ya SGR haraka kama tulivyotarajia.
“Sisi kwa upande wetu reli iko tayari, tunasubiri mabehewa. Taarifa tulizonazo watu wameanza kurudi kazini huko, viwanda vimefunguliwa na utengenezaji wa mabehewa tuliyoagiza umeanza. Tunamwomba Mungu kila kitu kikienda vizuri, basi mwezi Machi, mwaka huu tutayapokea mabehewa haya na kazi itaendelea kwa kasi kubwa. Corona ni janga la asili na limetuathiri kutimiza ndoto yetu kwa wakati, ila chini ya uongozi shupavu wa Rais Samia, nakuhakikishia reli hii itakamilika na tutajenga nyingine nyingi kama ulivyosikia zikitangazwa wakati wa kutia saini kipande cha tatu (Lot 3) juzi.
Alipoulizwa juu ya ukame unaoikumba nchi mara kwa mara na kwamba uwekezaji mkubwa wa Sh trilioni 6.5 unaowekezwa katika mradi wa maji wa Bwawa la Nyerere watu wanasema ni upotevu wa fedha, maana ukitokea ukame bado nchi itakosa umeme kama inavyotokea katika Bwawa la Mtera kuishiwa maji, amesema: “Huu mgawo wa umeme tulioupata umechangiwa na mambo mengi. Kwa sasa kama nchi tunaendelea kuimarisha uwezo wa vyanzo vya uzalishaji umeme ikiwamo ukarabati wa mitambo na ujenzi wa vyanzo mbalimbali vipya ikiwamo gesi, upepo na Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo pekee litazalisha megawati 2,115.
“Hata kama maji yatapungua, umeme unaozalishwa hautashuka chini ya megawati ambazo ni mahitaji yetu kwa sasa. Tutaendelea kutumia na vyanzo vingine ikiwamo gesi, upepo, makaa ya mawe na Bwawa la Mwalimu Nyerere. Bwawa hili ni suluhisho la kudumu la matatizo ya umeme Tanzania. Umeme utakuwapo mwingi na wa kutosha, hivyo wanaowaza kuwa uwekezaji huu ni kupoteza fedha, hawaitendei haki nchi yetu. Ni vema tujivunie uwekezaji huu mkubwa unaotutoa hatua moja kwenda nyingine.”
Amesema Serikali ya Rais Samia imewaagiza maafisa wa kanda wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wanakarabati miundombinu ya umeme katika maeneo yao, kuepusha umeme kukatikatika, huku akisema mradi wa REA umelikomboa taifa kwa kufikisha umeme vijijini kwa kasi kubwa.

Chanjo na mikopo kwa nchi
 
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kasi ya uchanjaji imeongezeka nchini baada ya wananchi kupewa elimu ya kutosha, na watu waliokuwa wanapotosha juu ya ubora wa chanjo wanaendelea kushindwa kuthibitisha hoja zao. 

“Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu ya Uviko–19 kwa kushirikiana na waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya. Hatua tuliyofikia kupitia elimu ni nzuri. Tumewaeleza watu na tunawasihi watu wafuate maelekezo ya wataalamu wa afya, ambao ni madaktari katika suala hili la chanjo,” amesema.

JAMHURI limemuuliza Waziri Mkuu ana maoni gani katika sakata linaloendelea nchini la Serikali kuchukua mikopo kufanya shughuli za maendeleo, ambalo limeleta sintofahamu mwishoni mwa mwaka jana, akasema: “Mkopo wa Sh trilioni 1.3 unakwenda vizuri sana. Tuliunda Kamati ya Kitaifa, ambayo mimi ni Mwenyekiti. Tumeunda kamati za mikoa zinazosimamiwa na wakuu wa mikoa na wilaya, ambazo zinafanya kazi nzuri sana. Kufikia Desemba 31, 2021 taarifa nilizonazo halmashauri za wilaya nyingi zilikuwa zimekamilisha ujenzi wa madarasa kwa asilimia 100 na chache zilizosalia zilikuwa zimefikia asilimia 94. Kufikia Januari 15, 2022 madarasa yote yatakuwa yamekamilika na wototo wote waliofaulu watakwenda sekondari moja kwa moja bila kusubiri.”
Amesema ukopaji kwa taifa changa kama Tanzania ni jambo chanya, linaloharakisha maendeleo ya wananchi. “Mheshimiwa Rais, ameweka wazi kuhusu mkopo huu, na kila mwananchi anaona umefanya nini. Kwa mara ya kwanza kupitia mkopo huu tutajenga Shule Shikizi (Chekechea na darasa la kwanza) karibu 400 nchi nzima. Wazazi wengi wanapeleka watoto wao chekechea nyumbani kwa watu. Sasa Rais Samia amesema tuwe na mfumo rasmi. Ni sehemu ya mkopo huu inafanya mambo haya mazuri,” amesema.
Amesema mkopo huu pia utajenga miradi ya afya, kununua mashine za kisasa za tiba, kujenga barabara za vijijini, miundombinu ya wafanyabiashara wadogo na kununua mitambo ya kuchimba visima na mabwawa ya maji katika kila mkoa nchini ili kurahisisha upatikanaji wa maji kwa wananchi.
Alipoulizwa kuhusu mafanikio iliyopata Serikali ya Rais Magufuli, amesema serikali zote kuanzia awamu ya kwanza hadi ya sita zimepata mafanikio: “Zimefanya kazi kwa weledi mkubwa na mimi nimepata fursa ya kutumikia kuanzia Awamu ya Nne chini ya Rais, Dk. Jakaya Kikwete, nikapata fursa ya kutumikia katika Awamu ya Tano chini ya Rais, Dk. Magufuli, na sasa naendelea kutumikia katika Awamu ya Sita chini ya Mama Mheshimiwa Rais Samia – viongozi wakuu wameendelea kufanya nchi hii kuwa kimbilio.
 “Huwezi kukosa changamoto katika awamu zote hizi na viongozi wa awamu zote wamefanya kazi ya kutatua changamoto kadiri zilivyojitokeza. Naye Rais Samia ameanza na anaendelea vizuri, na tuna uhakika ataendelea kupata mafanikio makubwa. Muhimu kwetu Watanzania ni kuendelea kumuunga mkono kama tulivyomuunga mkono Dk. Kikwete, tukamuunga mkono Dk. Magufuli, kwa masilahi ya Watanzania.”
 JAMHURI limemuuliza anauzungumziaje mwaka 2021?
Amesema mwaka 2021 ni mwaka ambao nchi imepata changamoto kubwa ya kupoteza viongozi wa kitaifa; kufiwa na Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli akiwa madarakani. Pia kufiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akiwa madarakani, Mheshimiwa Seif Sharif Hamad, kufiwa na Balozi Mhandisi John Kijazi aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi. 

“Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema peponi.  Ni mwaka ulioweka historia ya Tanzania kupata Rais wa kwanza mwanamke, Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeapishwa Machi 19, 2021 kushika madaraka kwa mujibu wa Katiba baada ya kifo cha Rais Magufuli,” amesema.
Amesema pamoja na changamoto kubwa ya kifo cha Rais Magufuli iliyotokea, bado serikali imeendelea kufanya kazi na kupata mafanikio makubwa. “Miradi yote mikubwa kama reli, barabara, ununuzi wa ndege, ujenzi wa madaraja, barabara, Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere… Kazi inaendelea. Na kazi inaendelea vizuri kweli chini ya Mheshimiwa Rais Samia, tunayepaswa kumpongeza kwa usimamizi na uendeshaji bora kabisa wa serikali.
“Tunajua changamoto za hapa na pale zipo kama kuongezeka kwa muda katika baadhi ya miradi, ila kama nilivyosema hili limetokana na janga la corona, kwani serikali haidaiwi na wakandarasi, bali inadai kazi, imekwishawalipa wote wanaohusika katika miradi hii ya kimkakati. Tunaamini kadiri changamoto ya corona inavyopungua vifaa vitaanza kuingia kwa kasi hapa nchini, na miradi itaongeza kasi ya utekelezaji wake.
“Tumesikia mafanikio mengi tuliyopata katika mwaka ulioisha kupitia hotuba za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mwaka 2021, na sasa ametoa mwelekeo wa shughuli za serikali kwa mwaka 2022. Sisi kama wasaidizi wake kupitia mwongozo wa kila wizara uliopitishwa katika bajeti, Ilani ya CCM na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia, tumejipanga kuendelea kumsaidia kujenga Tanzania iliyo bora zaidi.
“Tunaomba wananchi waendelee kuiamani serikali yao chini ya Jemedari wao Rais Samia anayeendelea kufanya kazi vizuri, kwamba miradi yote iliyoanza miaka ya nyuma itatekelezwa na mingine mipya tayari imeibuliwa na imeanza kutekelezwa. Nawatakia heri ya mwaka mpya 2022 Watanzania wenzangu. Mungu ibariki Tanzania.”