Kwanza nianze kwa kumsalimia kaka na rafiki yangu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba. Salamu hizi ni salamu za dhati kutokana na malezi niliyopewa na walezi wangu. Shikamoo Mheshimiwa Waziri.
Mwigulu ni kaka na rafiki yangu. Mtanzania mwenzangu, mchapakazi na mwenye maono na malengo makubwa katika nchi yetu.
Kutokana na upendo mkubwa nilionao kwake, leo nalazimika kutumia ukurasa huu kumshauri kujitafakari upya katika wadhifa alionao sasa.
Watanzania wote wanatambua ya kuwa wewe ni mchapakazi na mpenda maendeleo, lakini kutokana na kile kinachoendelea Mkoa wa Pwani, nakuomba sana mheshimiwa waziri mwenye dhamana ya ulinzi wa raia na mali zetu ujitafakari kama kweli unafaa kuendelea na wadhifa ulionao au la.

Mwaka 1977, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Rais wa Awamu ya Nne, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, alijiuzulu wadhifa wake kutokana na utovu wa nidhamu uliofanywa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi Kanda ya Ziwa.
Mwinyi alichukua jukumu la kujiuzulu kutokana na kile alichokisema kuwa hawezi kukwepa kadhia iliyojitokeza kwani dhamana yake ya uwaziri imeambatana na wajibu wa jeshi hilo.
Kujiuzulu huko kumemjengea heshima ambayo katu haiwezi kufutika katika historia ya nchi yetu vizazi na vizazi.

Waziri wa mambo ya ndani ndiye kiongozi wa Jeshi la Polisi ambalo kazi yake ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Usalama wa raia wa Mkoa wa Pwani umetetereka.
Usalama wa askari polisi nao unazidi kutia hofu kutokana na mauaji yanayoendelea kutokea Rufiji, Mkuranga na Kibiti. Watanzania wanaishi kwa hofu huku wakitakiwa kuingia ndani saa 12 jioni kwa lazima.
Kibiti limekuwa eneo hatari, waziri amekuwa akishuhudia mauaji bila kuwajibika.

Kutokana na heshima uliyonayo kaka yangu Mwigulu, kutokana na uzalendo na uthubutu ulionao rafiki yangu na kijana mwenzangu. Nakuomba sana tena kwa msisitizo baba jiuzulu tu.
Mauaji yanayoendelea Mkoa wa Pwani ni moja ya kipimo tosha kuwa wizara hii imekushinda kuiongoza. Si kwamba wewe ni dhaifu ila wahalifu wamekuzidi kete, hivyo ni vyema ukajiuzulu ili kutoa nafasi kwa Rais kuweza kuteua mtu mwingine ambaye atakuja na mbinu mpya za kukabiliana na uhalifu huu na mwingine utakaotaka kujitokeza.

Siombi uhalifu uendelee kutokea nchini, bali natoa tu angalizo. Natambua uwezo mkubwa wa vikosi vyetu vya ulinzi katika kupambana na kukabiliana na uhalifu na wahalifu. Sina shaka katika hilo.
Nimelazimika kutumia ukurasa huu kukushauri rafiki yangu bila kuwa mnafiki, kwani wapo baadhi ya marafiki zetu wa karibu ambao nimewasikia wakiulizana na kukushangaa kwa kutowajibika kutokana na mauaji haya.
Bila kificho wanakusema pembeni. Wanakusema kwamba umeng’ang’ania kuendelea kuwa waziri wa usalama wa raia na mali zao wakati usalama wa raia umezorota nawe hujali kwani kama ungeonesha kujali ungeng’atuka kuonesha kwamba unakerwa na hili.
Wanakusema kwamba umebadilika na kuwa king’ang’anizi wa madaraka. Wanakusema kwamba umeshindwa kuonesha uzalendo wako uliokuwa nao hapo awali. Uzalendo uliokuwa ukiwafundisha vijana wenzio ambao wewe ndiyo shujaa wao.
Mheshimiwa, kutokana na heshima uliyonayo, nakuomba utafakari suala hili kwa kina kwani kuendelea kuongoza wizara hii ni kujipaka tope. Jiuzulu kaka. Jiuzulu uendelee kuwa safi.

Ni vyema ukafuata nyayo za baadhi ya viongozi wetu walioamua kuachia madaraka ili kulinda heshima. Naamini ya kuwa bado una nafasi ya kuonesha njia kwa vijana, njia ya kuendelea kuwa kiongozi bora bila kuwa waziri wa wizara hii.
Kuendelea kuwa waziri katika hali hii ni kujidhoofisha kiutendaji mheshimiwa kaka. Unajidhoofisha kisiasa ndugu yangu. Jiuzulu mapema na uendelee kulitumikia Taifa kupitia jimboni kwako na bungeni mpaka pale Rais atakapoona unafaa.
Kutokana na jinsi ninavyotambua kuwa wewe ni miongoni mwa viongozi vijana wenye busara, naamini ya kuwa utatafakari ushauri wangu huu na kuchukua hatua wala hutosubiri kutumbuliwa kama ilivyotokea kwa rafiki yetu mwingine niliyewahi kumpatia ushauri akaupuuzia yakaja kumkuta.
Wasalaam.

By Jamhuri