Serikali kupitia Wizara ya Habari, Sanaa na Utamaduni imemfungia msanii, Abednego Damian maarufu Roma Mkatoliki kutojihusisha na shughuli zozote za muziki kwa kipindi cha miezi sita kutokana na kukaidi kufanyia marekebisho wimbo wake wa ‘Kibamia’.

“Huyu ndugu anayeitwa Roma Mkatoliki tunampa adhabu, kwa mujibu wa katiba na kanuni ambazo zinatuongoza sisi. kwa hiyo tunamfungia kwa miezi sita. Ndani ya hiyo miezi sita hakuna kufanya kazi yoyote ya sanaa, hakuna kutoa wimbo wowote wa sanaa, hakuna kuperform kwenye tamasha lolote, na wimbo huo moja kwa moja tunaufungia,” amesema Naibu Waziri, Juliana Shonza.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Alhamisi,, Machi 1, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza ameeleza kuwa msanii huyo amewahi kupewa onyo la kubadilisha jina la wimbo huo pamoja na baadhi ya maneno yaliyomo ndani yake, lakini alikaidi na wimbo huo ukaendelea kupigwa katika vyombo mbalimbali vya habari.

Shonza ameongeza kuwa, Roma Mkatoliki amekuwa akipigiwa simu na kutumiwa ujumbe mfupi wa maanddishi ukimtaka afike katika ofisi za wizara hiyo, lakini hakutaka kupokea na amekuwa akizisoma jumbe hizo bila kujibu chochote, jambo ambalo linaonyesha kuwa anadharau wito wao.

Hivyo kutokana na kukataa wito huo, Wizara hiyo imeamua kumfungia Roma kujihusisha na shughuli za sanaa kwa muda wa miezi sita kuanzia leo Alhamisi Machi Mosi, 2018.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), imempa onyo msanii Emmanuel Elibariki maarufu Nay wa Mitego kutokana na nyimbo zake nyingi kuwa na lugha isiyo nzuri (matusi), na kuahidi kuwa atabadilika na kuzifanyia marekebisho nyimbo hizo.

Shonza alitaja baadhi ya nyimbo za Nay wa Mitego kama vile Maku Makuz na Hapa Kati Patamu.

Vile vile, Juiana Shonza ametoa onyo kwa wasanii wengine kuzingatia maadili katika utungaji wa nyimbo zao, pamoja na video, ili kujiepusha kuingia matatizoni na kuwataka kuitikia wito mara moja pale wanapotakiwa kufika kwa ajili ya mazungumzo.

“Nionye tu kwa wasanii wengine kwa mba ni vizuri unapoitwa ukaweza kufika, kwa sababu hujui unachoitiwa ni nini,” amesema.

Hatua hii imekuja ikiwa ni miezi michache tu imepita tangu Wizara hiyo, iwafungie badhi ya wasanii wa kike pamoja na ‘video queens’ kutojihusisha na sanaa kutokana na kufanya mambo yanayokiuka maadili.

By Jamhuri