Wiki jana, niliandika juu ya nafasi ya kufanya mikutano ya kidemokrasia iliyopigwa marufuku muda wa kazi, niliandika kutokana na kumbukumbu mbalimbali za ujana wetu miaka ile dahari ya mfumo wa chama kimoja, ambapo tulikuwa na hiyari ya kuchagua jembe au nyundo.

Wiki jana nilijaribu kuwakumbusha kuwa utaratibu wa Serikali yoyote duniani ni kuwaletea maendeleo raia wake na siyo kuwafukarisha kwa namna ya kuingiza siasa kuwa kikwazo kimojawapo cha maendeleo. Wanazuoni mbalimbali wamesema hata katika kiwango cha familia au kaya kama hakuna utulivu ni dhahiri kuwa maendeleo hayatapatikana.

Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka hoja mbalimbali za kisiasa kutaka demokrasia ya uhuru wa watu katika kufanya siasa utambuliwe na uheshimiwe, tumeona watu ambao ni wanasiasa na ambao si wanasiasa wakijaribu kunadi sera zao mahali walipo kwa kuanza na kulaumu uhuru wa kutumia demokrasia ya siasa.

Kwangu mimi nakubaliana na hoja zao ambazo zipo sahihi lakini labda ni suala la kukumbushana kama kuna ibara yoyote katika Katiba yetu ambayo haikinzani na hoja yao, nakubaliana na siasa na siasa ni kazi ilimradi isiwe kazi ya kutuletea umaskini au kudhoofisha mambo yanayoleta maendeleo.

Sisi ni watu wachache ambao tulipiga kura ya maoni juu ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, na wakati ule kila aliyekuwa akitoa maoni yake ya kutaka vyama vingi vya siasa, alikuwa akitazamwa kwa jicho la tatu zaidi katika mazingira ya kuonekana mpinzani.

Baadhi walikuwa wanaogopa kuchangia katika kadamnasi lakini walipopewa nafasi ya kutoa maoni yao katika makundi ya watu wachache, waliweza kujenga hoja nzito za kuwa na vyama vingi, wapo walioshauri wakati ule kwamba Katiba ya nchi nayo iangaliwe upya ili kwenda na mfumo mpya wa vyama vingi.

Kimsingi, hakuna kosa lolote ninaloliona kama tukiweza kubadili Katiba na kuruhusu watu wawe huru ya kutumia demokrasia vizuri, sisemi kwamba Katiba inakataza mikutano ya hadhara, hapana ila ina misingi ya dhati kwa Mtanzania anatakiwa afanye nini kwa wakati gani.

Nafahamu vipo vifungu vya kufanya kazi kwa mwananchi badala ya kuwa kupe, mnyonyaji na kadhalika, nafahamu uko uhuru wa mwananchi katika kushiriki masuala ya siasa, nafahamu kuna uhuru wa kupashana habari na kupasha na kupata habari, lakini kimsingi hakuna uhuru usio kuwa na mipaka.

Katika nchi zilizoendelea, ukiangalia mfumo wao wa siasa hapo awali ulikuwa na mipaka, hawakuendekeza siasa wakati wa kazi, hali kadhalika hata nchi yetu tena wakati tumetoka kupata uhuru, tuliamua siasa iwe baada ya kazi, siku hizo tulikuwa tukifanya siasa kuanzia saa kumi jioni baada ya kufanya kazi.

Leo uwanja umepanuka, siasa zinafanyika alfajiri bila kujali muda wa kazi, siasa leo ni ajira kwa watu wachache na wanafanikiwa kuwaongoza wengi ambao ni wachapakazi, siasa ni uwanja wa kutumia demokrasia ya kujieleza bila kuzingatia sheria zetu za katiba zinasemaje.

Nakubaliana na wanaodai haki ya demokrasia lakini ninahoji matumizi ya demokrasia hiyo kwa taifa maskini ambalo tunapaswa kuwajibika kwa kazi, nahofia hiki kichaka cha kulumbana kisiasa tutafika nacho wapi hata baada ya kupata uhuru kwa miaka zaidi ya hamsini.

Katika miaka ya 1960 Taifa hili lilikuwa sawa kiuchumi na mataifa kama China na  Malasyia, leo wenzetu wakitoa misaada kwa mataifa maskini wanatukumbuka kutupatia pia, leo wakitoa mikopo tupo katika orodha ya wakopaji sababu kubwa ni demokrasia ya kuongea na kutofanya kazi, sababu kubwa ni kusikiliza kila mtoa hoja na hoja yake hata kama inatupotezea muda.

Wanasiasa ndiyo waliotufikisha hapa kwa siasa zao, wameliingiza Taifa katika migogoro ya kisiasa, kisa utawala, wameliingiza Taifa katika mikataba mibovu, kisa wana maamuzi ya kiutawala, sasa tumempata kiongozi aliyetenga muda wa siasa na kufanya kazi ni vema tukafanya kazi na tuone tathmini baada ya miaka mitano.

Iwapo hatutaona mabadiliko, basi kwa kutumia siasa tena wakati huo tubadili msimamo wa uongozi na kuwapima wengine kwa miaka mitano.

Napenda siasa lakini siyo siasa hizi za kutafuta ulaji kwa migongo ya demokrasia, hata demokrasia ina mipaka. 

 

Wasaalamu, 

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri