Yah: Historia hujirudia ni laana

Nianze na salamu za pole kwa wenzetu wote, hasa Waafrika ambao wako Kusini mwa bara hili, ambao wamekumbwa na mauaji ya wenyewe kwa wenyewe kama vile wanaowaua wanatoka nje ya Afrika na hawana undugu nao, yaani leo wamesahau waliishije enzi zile za ubaguzi.

Sababu wanazozitoa ni kwamba wamekwenda kuishi huko na kufanya kazi ambazo wao walipaswa kuzifanya na kujipatia ujira ambao ungewafanya waishi maisha bora zaidi.

Maisha bora sasa kuliko kipindi cha utumwa wa makaburu. Nadhani zipo sababu zingine ambazo zitakuwa na mashiko sana mpaka kufikia hatua ya kuamua kumwaga damu kwa wenzao kutoka Afrika.

Kwa tuliozaliwa zamani kabla ya uhuru wa nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara  na kuwaona majirani zetu tulioishi nao huku kwetu wakati wakipigania uhuru nchini mwao, mtakubaliana nami kuwa tuliishi nao kama ndugu wa damu na tuliwaona kama wahitaji wa msaada wa hali na mali kutoka kwetu.

Kwa wasiojua suala la kuhakikisha wanapata uhuru lilichukuliwa kwa nguvu zote na viongozi wachache sana Afrika na wengi wao walipata maono kutoka kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Najua wapo watakaokataa, lakini huo ndio ukweli na historia itabaki kuwa hivyo hata kama itapotoshwa kwa kiasi gani, kuna kundi kubwa ambalo hata hapa nchini linaaminishwa kuwa uhuru wa nchi hiyo ulipatikana kwa juhudi zao wao wenyewe.

Jitihada za Mwalimu hazikupaswa kupotezwa kienyeji namna hiyo. Kwanza ni kosa kubwa sana kwa Watanzania kutowakumbusha wenzetu wa Afrika  Kusini, pia kutowachaji gharama ambazo tuliingia mpaka kufikia hatua ya kufifisha maendeleo yetu. Hili ni kosa letu, si lao, na kukumbusha kosa ambalo linapaswa kurekebishwa si kosa.

Sasa umefika wakati muafaka wa kuwakumbusha wenzetu kuhusu muda tuliotumia, rasilimali zilizopotea na nguvu iliyotumika kuwakomboa kutoka katika mikono ya makaburu wakati wa  ubaguzi wa rangi. Wanapaswa kulipa kila kitu ili wajue thamani ya Watanzania ambao wanamwaga damu zao.

Ni uzalendo tu uliotumika kutodai malipo ya kuwakomboa kama ambavyo mataifa mengine makubwa hufanya kwa mataifa madogo wanayoyafanyia mapinduzi kwa kigezo cha kutokuwepo kwa demokrasia halali ndani ya mataifa hayo huku wakijua kuna kuvuna mapesa baada ya mapinduzi hayo.

Linaloendelea Afrika Kusini ni historia inayojirudia. Ni kutokuwa na mwendelezo wa historia ya uhuru kwa vizazi vyao na kwa kufanya kosa kubwa tena, kamwe hali hiyo haitatengemaa mpaka kizazi hicho chenye laana kitakapokwisha na kuwa na kizazi chenye baraka kutoka kwa wananchi kwa ujumla wao na kusahau baada ya kusamehe.

Sisi tunakumbuka jinsi ambavyo tuliwachukulia kama ndugu zetu, tuliamini mipaka kupitia wakoloni na tuliamini umoja katika rangi yetu, tuliamini katika ukombozi wa nchi zote za Afrika kuwa ndicho kigezo cha uhuru wa Afrika, tuliteseka kwa ajili yao na tunaendelea kuteseka hadi leo kwa ajili yao ilhali wao hawayajui mateso yetu na wanaendelea kutuua kama wanyama.

Sielewi katika mitaala yao somo la Historia linasemaje kuhusu ukombozi wa taifa lao. Sioni jinsi ambavyo viongozi wao wanathamini jitihada ambazo taifa letu lilizifanya ili kuhakikisha wapo huru.

Inawezekana pia hata sisi tukawa tunaficha ukweli kuhusu ukombozi wao. Ninashauri sasa suala hili liwe wazi na ikibidi iandaliwe taarifa rasmi ya jinsi ambavyo tulihangaika kwa ajili yao, walinganishe matendo yao ya kikatili na huruma yetu kwa wachache wao.

Si kwa maana ya kuridhika kwa kinachoendelea huko kusini, lakini napenda nitumie neno gumu kwamba ni upumbavu kwa viongozi wa nchi hiyo kutothamini mchango mkubwa uliotolewa kwao na nchi ambazo zinaonekana kwa sasa ni wahanga, kwa kudhani kwamba wanapaswa kuhukumiwa kifo.

Ni ujinga kutowaelimisha watu wao kwamba Tanzania ni nchi ambayo tuliwalea wakati wa kutafuta uhuru na kama tungeamua kuwaua kama wao wanavyofanya, mpaka leo wangekuwa chini ya makaburu na wasingepata uhuru wao.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.