Nianze waraka wangu wa leo kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa uhai mrefu wa kuweza kuyaona mambo ya dunia hii ya awamu mbalimbali na mambo tofauti, yanayoleta changamoto katika kichwa changu.

Huwa nawaza sana juu ya vitukuu vyangu vitaionaje dunia ambayo sisi tunawaachia kwa hivi sasa, yapo ambayo natoa uamuzi sasa hivi kuwa hayo ni ngumu kudhibitika na kwamba kizazi chao kitaishi kwa staili mpya kabisa ambayo sisi tunaweza kufa bila homa iwapo tu tutaoteshwa.

Nawaza wakwe zangu vitukuu – viwe vya kike au vya kiume – itoshe tu kusema hali niionayo sasa hivi inanifanya nione kichefuchefu seuze kwa wakati huo? Sina hakika kama hata posa itakuwa ikitolewa kwa wenyewe, nawaza kwa sauti namna ambavyo watakuwa wanavaa na heshima katika jamii yenyewe, sijui wakati huo hawa dot.com watakuwa wanaonekana analogi au vipi!

Najaribu kuvuta hisia za maisha niliyoishi mimi kwa utoto wangu na tofauti iliyopo sasa kwa watoto wadogo ambao nao inawapasa kuufaidi uzee wangu, najaribu kukumbuka uhayati wa ujana wangu na urijali niliokuwa nao na kizazi cha vijana wa sasa wa kuku mayai na madhara yanayowasibu, naona kama wamepanga kuchagua lakini hawachagua kupanga.

Naangali mfumo wa uongozi enzi zetu na mfumo wa uongozi uliopo sasa na changamoto zake, haki ya kuongea na kuchagua aina ya mfumo wa siasa wa kukidhi matakwa ya wote, waliopo madarakani na wanaotaka madaraka na wale wanaoongozwa.

Nakumbuka kanuni mbalimbali za utawala wetu wa nyakati zile za siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, siasa za kufanya kazi na kujiletea maendeleo, siasa za kukataa utawala wa kimwinyi na badala utawala wa shamba la mfano, uongozi wa kuiga kutokana na matendo, uongozi wa awamu ya kujitolea.

Naangalia mfumo uliopo na matatizo ya kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo kwa maana ni kizazi cha uongozi na siyo kufanya kazi, ni kipindi cha kujadili udhaifu wa viongozi ili kuweza kupata nafasi ya kutumikia wananchi kwa faida ya matumbo, tumepanga lakini hatujachagua, ni aina ya siasa tunayofanya sasa na sijui hatima ya kizazi cha vitukuu vyetu.

Maisha yanakwenda kasi sana, miaka 60 iliyopita naona ni kama jana tu ya kuamkia leo, miaka mitano ijayo najiuliza uwezo wa kumaliza hiyo safari, watoto wa juzi miaka ya 1970 nawaona wakiwa wazee wenye kubeba uzee pasi na umri wao halisi, sitaki kukubali mabadiliko ambayo yanaleta kero badala ya ahueni.

Sitaki kusikia la mtu juu ya ushauri wa kizazi cha sasa, kizazi cha kuangali nafuu ya leo na siyo nafuu ya kesho, kizazi cha kuangalia shibe ya tumbo na siyo shibe ya maendeleo, kizazi cha kutafuta wepesi badala ya kukabiliana na changamoto, kizazi cha kutafuta suluhisho badala ya kuishi kwa amani. Hii ndiyo dunia ninayokumbana nayo sasa katika kuhitimisha nngwe yangu ya maisha.

Nashindwa kukubaliana na ukweli kiasi cha kuomba rufaa ya kutoona kinachoendelea, sitaki kuamini kuwa maendeleo ya sasa siyo kufanya kazi badala yake ni kuuziana sumu, siyo kufanya kazi badala yake ni kuwa madalali wa wazee wachache wanaofanya kazi, sitaki kuamini kuwa ni kizazi cha kuamini katika dhuluma na uonevu, kizazi cha kutojua hatima yako ya maisha.

Sitaki kuamini kuwa tunafikiria kupotezeana maisha na siyo kunufaishana maisha, sisi tunachagua kutoogopa maisha ya mtu, tumechagua kuwafanya wanandamu wenzetu kuwa bidhaa na siyo binadamu, hiki ni kipindi cha sasa na sijui kipindi kijacho cha vitukuu kitakuwaje.

Nawaza jinsi ambavyo binadamu anashindwa kumteka mbu lakini anaweza kumteka binadamu mwenziwe na kumdhuru kwa sababu za kukosa utu, ni enzi za kumwaga damu kwa lengo la kujipatia mkate wa siku, hii ndiyo awamu inayofanya nijiulize maswali mengi ya kutaka kujua awamu ya vitukuu vyangu.

Sitaki kujua wataishije lakini nikiwaangalia machozi yananitoka, kila jambo lenye heri sasa ya hatari ni jambo la kufikirisha sana kwa wakati wao, nadhani umefika wakati tukaamua kupanga na kuchagua na kuchagua ni kupanga kikawa cha manufaa kwa kizazi kijacho.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

979 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!