Marekani ni muungano wa majimbo makubwa mengi ambayo yangeweza kuwa nchi kama ilivyo kwa nchi ndogo za Afrika, lakini majimbo yale ndiyo yanayofanya taifa moja la Marekani lenye nguvu duniani kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kiteknolojia na kadhalika.

Siri kubwa ya mafanikio ya taifa lile ni muungano wa majimbo na kuwa taifa kubwa linaloweza kujitosheleza katika sekta mbalimbali. Waasisi wa taifa lile walioona mbali katika suala la muungano miaka dahari iliyopita, leo wameingia katika kumbukumbu ya kuheshimiwa kwa uamuzi wao wa hekima wakati huo.

Uingereza, taifa ambalo limetawala mataifa mengi duniani, lina muungano na visiwa vingine ili kuleta umoja wa kushirikiana katika mambo mengi yakiwamo ya ulinzi na usalama, lakini pia umoja wa kiuchumi ambao unawafanya waonekane kuwa na nguvu katika uchumi wa dunia ya leo.

Miaka kadhaa iliyopita, kundi la viongozi mahiri wa Afrika – Julius Kambarage Nyerere (Tanzania), Osagyefo Kwame Nkrumah (Ghana), Jomo Kenyatta (Kenya), Patrice Emery Lumumba (Kongo Kinshasa-DRC) na wengine, waliwahi kufikiria muungano wa Afrika na kuwa taifa moja liitwalo Afrika, ambalo lingeweza kuingia katika ushindani wa maendeleo na mataifa mengine.

Haya ndiyo baadhi ya mataifa makubwa ambayo yana maendeleo ya kiuchumi na kisiasa yaliyofikiria kuungana ili kuwa taifa moja lenye nguvu na kuweza kushindana na mataifa mengine, lakini pia kuna Japan ambayo ni nchi moja inayotokana na muungano wa idadi kubwa ya visiwa.

Nchi maskini na zenye watu wenye tamaa za kujilimbikizia mali ndizo zinazoongoza kwa kuwa na watu wenye kupinga muungano. Suala la muungano, mathalani kwa nchi yetu, limekuwa likizungumzwa sana na baadhi ya watu wasio na mtazamo wa umoja na maendeleo, viongozi ambao wapo lakini ni wanafiki wa umoja na muungano kwa dhima yake, hawa mara nyingi si viongozi wa watu bali viongozi wa nyoyo zao za tamaa.

Kuna makundi ya watu ambao wanafikiria juu ya kuvunja muungano kwa sababu ya manufaa yao binafsi na siyo kwa manufaa ya wingi wetu na maendeleo yetu, hawa ni watu wenye roho na haiba ya ubinafsi na hawapo kwa manufaa ya Taifa ila kwa manufaa ya matumbo yao.

Dhana ya muungano haiangalii ukubwa wa nchi, ni dhamira zaidi ya kimaendeleo ndiyo inayoweza kuwasukuma wananchi kuungana, dhana ya muungano ni sera ambazo zinakubalika kwa pande zote mbili, aina ya siasa na mfumo wa siasa uliopo, vinatosha kuzifanya nchi mbili zenye mtazamo wa kimaendeleo kuungana.

Muungano ni silaha ya mataifa  ambayo ni maadui wa kimaendeleo, maadui hawa wanaweza kuwa nje ya nchi au ndani ya nchi pia. Wakati tunaungana Tanganyika na Zanzibar tuliwakera maadui zetu wa maendeleo, na maendeleo si lazima yawe ya kuonekana kwa macho – inaweza kuwa maendeleo katika ulinzi na usalama au matumizi ya kushirikiana katika rasilimali zetu.

Nguvu ya muungano wetu uliopo kwa sasa haiwezi kubainika  kwa kuwa upo lakini tukitengana ni dhahiri kuwa tutaiona kasoro yake muda mfupi tu baada ya kuvunja muungano, dhima hii ya muungano ni kubwa kwetu kwa sasa japokuwa kuiona ni lazima kuwapo na jicho la tatu kwa mtu asiyejua maana ya muungano.

Huwa nafikiria kama Afrika tungeungana na kuwa nchi moja, ni dhahiri kuwa kwanza tungekuwa tunajitegemea kwa mahitaji yetu ya ndani kwa maana ya huduma za jamii na maliasili tuliyonayo, pili tungeweza kutumia rasilimali zetu kuuza nje na kuwa na amali ambayo tungetumia kwa maendeleo yetu ya Afrika.

Nafikiria uwezo wa baadhi ya viongozi wa Afrika ambao kwa sasa wapo madarakani wa kuweza kuwa na maono kama ya wale viongozi wetu waliokuwa katika fikra hizo nyakati hizo, tunakataa muungano kwa sababu ya uroho wa madaraka na kadhalika.

Wazo la kuungana Tanganyika na Zanzibar na kisha kuungana kwa nchi za Afrika Mashariki lilikuwa mwanzo mzuri wa kutupeleka katika Afrika moja, naamini muda bado tunao na inawezekana kuna viongozi wenye maono kama yale ya zamani ambao siku moja Afrika itakuwa nchi moja.

Kama mawazo ni kuwa na nchi moja ya Afrika moja, ni dhahiri kuwa ni ujinga kufikiria kuuvunja muungano wetu tulionao.

 

Wasaalam, 

Mzee Zuzu

Kipatimo.

882 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!