Yah: Naamini wengi wetu ni bendera fuata upepo

Kuna wakati niliwahi kuandika barua mahususi katika uga huu, nikijaribu kuelezea madhara ya
watu kuiga mambo na kushabikia bila kujua kile ambacho wanaiga kina madhara gani, wapo
waigaji wa mambo bila kujua labda wanakoiga wanaigiza na siyo uhalisia.
Mimi ni Mtanzania wa kuzaliwa, najivunia Utanzania wangu na ninaweza kuusema mahali
popote pale bila kuwa na haya wala soni, ni Mtanzania kwa uzawa wa bibi na babu na wote
najua nimewalaza wapi, ni Mtanzania ambaye ninaijua Tanzania kwa zaidi ya miaka sitini nikiwa
na akili timamu, ni Mtanzania niliyepigania uhuru kwa amani na tukaupata.
Ni Mtanzania mpenda mageuzi halisi, ni Mtanzania ambaye naweza nikaikosoa Serikali iliyopo
madarakani kwa kufuata misingi ya uanzishwaji wa Taifa hili, ni Mtanzania ninayejua kuwa nchi
yetu iko katika mfumo wa vyama vingi na ina taratibu zake za kufikisha ujumbe kwa mujibu wa
taratibu za vikao na mikutano.
Mimi ni Mtanzania ninayejivunia kitu kimoja tu kwa Taifa langu, nacho ni amani, najua kuwa
amani ndiyo iliyotufikisha hapa tulipo leo, najua kuwa amani ndiyo iliyotufanya wengine
wazaliwa wa zamani tukawa na kitu kiitwacho uzalendo, nafahamu pia kuwa iwapo amani
itadumishwa ni dhahiri kuwa tutapanda mbegu bora ya uzalendo kwa miaka dahari ijayo.
Naipenda nchi yangu si kwa sababu ya milima na mito, la hasha, ni kwa sababu mosi ni nchi
yangu; pili ninaishi kwa amani na furaha, naipenda si kwa sababu ni maskini lakini pia
sitaipenda kwa sababu ni tajiri lakini tukiwa hatuna amani.
Naandika barua hii, tena nikiwa niko katika dimbwi zito la mawazo, nikiangalia makaburi ya
mashujaa uchwara kwa kisingizio cha kutaka demokrasia, naandika si kwa sababu
nimehadithiwa madhara ya vita bali ni kwa sababu nina ushahidi wa kuona madhara ya vita,
najua wapo Watanzania wengi ambao hawajui vita na kama wameona basi wameona maigizo
ya vita.
Vitabu vyote vitakatifu vinazungumzia juu ya amani, watu wote wenye hekima na busara
wanazungumzia juu ya amani japo ni kweli kwamba amani inaweza ikapotezwa na viongozi
wachache wenye tamaa ya mali na madaraka.
Najaribu kuliangalia jambo hili kwa jicho la tatu zaidi naliona katika ujengaji wa hoja za kutafuta
amani kutoka kwa mzuia amani, mimi napenda mageuzi kama nilivyojitanabahisha mapema juu
ya msimamo wangu, najua nafasi ya wanasiasa katika mataifa yote, najua nafasi ya siasa
katika Taifa letu, najua dhima ya baadhi ya wananchi juu ya mustakabali wa usalama na amani
ya Taifa letu.
Mimi sipendi kabisa nguvu ya vyombo vya dola katika kuzuia haki ya demokrasia lakini pia
sipendi kabisa nafasi ya siasa katika kuchafua amani ya Taifa hili, kama nilivyosema awali
naijua Tanzania kuliko watu wengi, najua msimamo wetu kama wapigania uhuru wa Taifa hili,
najua tulikusudia kuipeleka wapi nchi hii na siko ambako naiona ikielekea iwapo wanasiasa
watatumia vibaya midomo yao.
Najua msingi wa dhana ya uongozi tuliyojiwekea, tangu tukipiga kura kwa kutumia alam za
jembe na nyumba, najua viongozi tuliwapata vipi bila kujali kabila au ukoo, dini au utajiri,
nisingependa kuona baadhi ya Watanzania wakiigeuza nchi yetu kuwa mtaji wa damu na mali
kwa mataifa mengine kwa mtaji wa wachache.
Napenda mfumo wa vyama vingi vya siasa, napenda kujenga hoja na kujibu hoja na siyo kejeli,
sipendi kusifiana mtu anapotekeleza wajibu wake lakini pia sipendi kubeza kazi nzuri
inayofanywa na mtu mwingine.

Uongozi wa nchi siyo wa familia, na uongozi wa nchi siyo wa kabila; ni nchi nzima; ni lazima
kujua kugawa rasilimali na utawala kwa watu wote, tumepata uhuru tukiwa maskini sana,
bidhaa pekee iliyokuwa ikiuzwa kwa wingi ni sisi wenyewe kama watumwa, leo tuna mali na
bidhaa, leo tupo wengi na tuna akili iweje wachache watumie akili zetu kujinufaisha?
Najua kuna watu wanakerwa na umaskini na wanatafuta mali na madaraka kwa nguvu, najua
wapo waliopo katika madaraka na pengine hawataki kuondolewa lakini jambo hilo halipaswi
kuigawa Tanzania ninayoijua mimi, Tanzania ya amani na upendo, Tanzania ya mshikamano,
Tanzania ya uzalendo, Tanzania kwanza siasa baadaye.
wasaalam
mzee zuzu