Yah: Nafasi za viongozi wasaidizi

Salamu zangu nyingi sana kama mchanga wa pwani, tena ule msafi, ziwafikie hapo mlipo, hasa nyie mlio mbali na upeo wangu wa macho. Najua mnaendelea vizuri na wengi wenu mnakumbuka mema mengi ya miaka mingi na kuyafananisha na mapya ya dunia mpya.

Naandika waraka huu nikiwa katika siha njema, lakini iliyogubikwa na mambo mengi ya maudhi katika maisha yangu, kiufupi, nina msongo mkubwa wa mawazo, hasa kutokana na namna ya baadhi ya viongozi wasaidizi wanavyoathiri watumishi wadogo kwa kutumia nafasi zao.

Naweza nisieleweke, lakini naamini wanaoelewa ni wale ambao wako katika nafasi za utumishi mahali popote, iwe serikalini au katika makampuni binafsi na wanaongozwa na baadhi ya watu ambao kimsingi nafasi walizopewa inakuwa kama ni bahati na hawakustahili kupata nafasi hizo.

Wapo kwa ajili ya kujihami muda wote na kuangalia waliopo chini kama maadui zao na si watu ambao wanastahili kupongezwa kwa kazi wanazofanya.

Wapo viongozi ambao wanaongoza mashirika na kampuni mbalimbali ambao kazi yao ni kuhakikisha kwamba kila kinachofanyika kionekane ni juhudi zao hata kama ubunifu huo si wao.

Wanapoona mfanyakazi anapata umaarufu au sifa, wapo radhi wamtafutie makosa na kumfukuza kazi, madhara yake ni makubwa kwa jamii, kwani hawatapata tena yale waliyokuwa wakipata kutoka kwa mtumishi huyo.

Suala la uongozi ni pana sana na ni watu wachache sana wanaoelewa dhana ya uongozi ni dhamana, pia watu wengi hawaamini kwamba nafasi walizonazo ni zao na wanadhani kila anayechipua yupo kwa ajili ya kunyang’anya cheo chake.

Hawa ni wengi na ndio wanaotengeneza chuki miongoni mwa watumishi na kuwafanya wanaofanya kazi kwa bidii kujiona wanyonge na wenye misongo ya mawazo kila siku, huu ndio utumishi uliotukuka siku hizi.

Enzi ya Mwalimu Julius Nyerere kulikuwa na utaratibu wa kuchunguzana sana kwa maana ya kufuatilia anayepewa dhamana hiyo ya uongozi na aina ya tabia aliyonayo. Wakati ule ilikuwa rahisi sana kutokana na idadi ya watu waliokuwepo na namna ya siasa yetu ilivyokuwa kwa maana ya ujamaa na kujitegemea.

Kipindi kile kilikuwa na maana halisi ya uongozi ni dhamana na kiongozi alionekana kuwa kiongozi bora kwa kuwashirikisha wengine kiutendaji na kufuata misingi ya sheria za kazi.

Jinsi miaka inavyokwenda kumeibuka dhana ya uongozi na elimu, wapo tunaowapa uongozi kwa kigezo cha elimu, wachache baadhi yao hawajapata kuwa na kipaji cha uongozi.

Kuongoza watu ni zaidi ya kusoma, ni kipaji na taaluma ambayo wakati mwingine inabidi isomewe na unaweza ukafaulu lakini huwezi kuongoza kutokana na namna ya maisha yako ya kujiona wewe ni bora zaidi kuliko unaowaongoza.

Sasa hivi baadhi ya viongozi wamekuwa miiba kwa watumishi wengi, nafurahi kuona wale walioko serikalini wakishughulikiwa kwa mujibu wa sheria na hiyo imepunguza ubwana mkubwa.

Sehemu kubwa kutokana na namna ambavyo serikali imejipambanua lakini kuna maeneo ambayo hayajatupiwa macho na watu wengi wanaumia na kuna mahali ambapo serikali inaweza ikawa inapoteza majukumu yake kwa taasisi hizo au wakala hizo kutokana na misimamo ya viongozi wasaidizi waliopo katika kusaidia walioko juu waweze kusonga mbele.

Viongozi wengi wamekuwa na wapambe wa nafasi zao, kutengeneza majungu na hao wanapata nafasi ambazo si zao na wanashindwa kuzitendea haki, wanakuwepo kwa sababu wana uwezo wa kutengeneza fitina mahali pa kazi na kujaza mambo ya uongo yasiyo na tija na kupoteza tija ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

Sasa hivi kujipendekeza kwa viongozi wasio na karama ya uongozi limekuwa ni jambo la kawaida, na hili ni jipu baya kwa kuwa linashusha morali ya kufanya kazi katika mashirika mengi ya umma na binafsi, wapambe wamekuwa na nguvu kuliko uongozi.

 Kwa kuwa viongozi hao wachache hawakupata nafasi ya kusomea uongozi lakini wamejaliwa kuwa na elimu kubwa, linageuka kuwa tatizo kwa watu watiifu na waadilifu katika utumishi.

Ombi langu kwa viongozi wakuu, wajaribu kupekenyua sehemu mbalimbali waone jinsi ambavyo maeneo mengine yanavyotia kinyaa kwa mambo ya ukabila, upambe, fikra binafsi, misimamo ya kijinga, kufanya kazi kwa imani za kiimla na kufanya maisha kuwa kama reli isiyopinda ghafla.

Naandika waraka huu nikiwa katika msongo wa mawazo lakini nina siha njema, sitaki kuamini kuwa uongozi ni wa mtu mmoja, bali ni pamoja na unaowaongoza.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo. 

179 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons