Nimelala usingizi wa taabu na mawazo mengi yasiyo na tija, ninawaza kesho nitakula nini, ninawaza wanangu wataendaje shule siku ifuatayo, si kwa vile nalipa ada, la hasha, kwa vile hawana kifungua kinywa, hawana madaftari wala kalamu, mama chanja ananikumbusha madeni yaliyopo mtaani kwetu, naziangalia barua kutoka sehemu mbalimbali naona nyingi zinahitaji nilipe au niingie mfukoni.

Lepe la usingizi linanipata, nahisi nitaota ndoto inayohusu maisha haya niliyonayo, nitaota kile ninachofikiria usiku huu, nawaza sana lakini sipati jibu la kutatua hali hii tete inayonikabili, sijui hatima ya kesho yangu lakini napiga moyo konde najiuliza kwani nina miaka mingapi na haya nimekutana nayo mara ngapi, nasema kimoyomoyo usiku huu nitashinda na yatapita.

Hitimisho hilo linanifanya nipitiwe na usingizi ambao unaniingiza katika ndoto ya mambo tofauti na niliyokuwa nawaza, najiona naimba wimbo wa ‘Tanzania Yetu’ na kundi kubwa la wanakijiji wenzangu hapa Kipatimo, nawaona waliotangulia mbele ya haki nikiwa nao mkabala lakini hawaongei nami, kama kundi kubwa tunakwenda mahali nisipopajua.

Tunafika katika uwanja ambao ninaufahamu uwanja wa shule yetu ya awali kabisa hapa Kipatimo, lakini leo ni shamba la mwekezaji nguli ambalo linatupa faida kubwa ya gawio, shule tumeipeleka mbali kidogo japo watoto wanakumbana na ghasia za fisi kila siku, uwanja umejaa pomoni na wananchi wanaimba kwa ari kubwa.

Hatujui nani mwenyekiti lakini kila mtu anachukua kipaza sauti na kuongea kero yake, najiuliza nafasi ikifika nitaongea nini kwa kuwa kila kitu kimeshaongelewa, nafikiria niimbe wimbo gani kutoa hamasa kwa wenzangu naona nyimbo zote zimeimbwa, najitia moyo kwamba ikifika zamu yangu nitasema ambacho hakijasemwa.

Imefika zamu yangu nimekabidhiwa kipaza sauti naanza kutetemeka siyo kwa woga ila kwa hasira ya yale niliyonayo moyoni kwa maisha niliyonayo, nashangiliwa lakini sijui kwanini, wapo wanaoimba wimbo mpya wa ‘sema baba usiogope’, na mimi nimeamua kusema bila woga nikiamini sauti yangu itasikika lakini hakuna kiongozi katika jukwaa la hapa uwanjani.

Naanza, ‘ndugu viongozi, kijiji chetu hakina maji lakini tuna bwana maji wa kijiji ambaye naye tunaongazana mtoni kuchota maji; akija kiongozi wa wilaya anatoa ripoti ya maji kimyakimya hatuelewi kasema nini, hakuna mabomba wala mitaro ya maji, tunaomba msikie kilio chetu,’ akina mama wananishangilia sana.

Naendelea, ‘ndugu viongozi kijiji chetu duka la ushirika limekufa na mhasibu wa duka tuko naye katika malalamiko ya kufilisika kwa duka la kijiji, hatuna mtu wa kumshika mkono kumuuliza juu ya duka letu, lilikuwa duka kubwa na sasa kitu cha thamani kilichobaki ni kufuli tu mlangoni,’ watu wananishangilia lakini kuna miguno ya watu wachache wakisema we mzee umepitwa na wakati, tulishaliwa siku nyingi.

Napaza sauti nasema, ‘jengo lililokuwa zahanati sasa ni bohari ya kijiji, watumishi waliondoka na utaalamu wao na dawa zao tumebaki tukiwasujudia waganga wa kienyeji kwa dawa zao na utaalamu wao kwa kukosa kwetu maarifa, wachache wanaonekana kunikubali lakini wengi wanaogopa kusema kwa sababu ya waganga tulionao mkutanoni.

Napaza sauti tena, ‘hatujafanya uchaguzi kwa muda mrefu na viongozi waliopo madarakani ni batili kwa mujibu wa sheria’, watu wote wananiangalia kuona kama ninayezugumza ni mimi, huku nikijipiga kifua nasema liwalo na liwe, potelea mbali, kiburi mwenzie jeuri, watu wengi wananizodoa kwa kusema ninyang’anywe kipaza sauti ninawakarahisha.

Napaza sauti tena, ‘haduma za jamii hapa kijijini kwetu hazipo tena, naomba zisogezwe,’ naanza kuzomewa na wananchi sisikiki tena zaidi ya kauli ya ‘rudisha kipaza sauti chetu’. Najiuliza haki ya kuongea niliyonayo imeota mbawa? Mbona nina mambo mengi ya kuongea kwa mustakabali wa kijiji changu? Naishiwa na nguvu namkabidhi jirani yangu aseme kero zake, watu wanashangilia sana.

Mwenzangu anasema, ‘jamani hapa kijijini hakuna ukumbi wa starehe,’ watu wanalipuka kwa furaha ya maoni ya mwenzangu.’ Anaendelea, ‘hapa kijijini hakuna sehemu ya kucheza mpira wala kuonesha video za mpira na sinema,’ hoihoi za vijana zinasikika.

Kwa hasira naamua kumpiga jirani yangu ambaye anatumia kipaza sauti vibaya.

Nashtuka usingizi nimempiga mama chanja ambaye sasa analia kwa uchungu, nafikiria kwanini nimempiga, kwanini nimeota ndoto hii ambayo haina uhusiano na mawazo yangu niliyolala nayo?     

Nasema ndoto yangu ya usiku wa Manani katika kirago chakavu ndiyo iliyosababishia yote haya.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.

905 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!