Kuna wakati niliwahi kumsikia Mwalimu Julius Nyerere akihutubia wananchi juu ya kulipa kodi. Katika hili alisema serikali ni lazima wawe wakali ili kila mtu aweze kulipa kodi, kodi ni kwa maendeleo ya nchi na watu wake, haiwezekeni Serikali icheke na walipakodi na walipakodi waichezee Serikali na kufanya watakavyo.

Serikali ni kama baba katika familia, iwe ikisema wengine wanasikia na kutekeleza kila kilichosemwa. Hii ni kwa nia njema kabisa ili matunda ya Serikali yapatikane kwa kada zote – masikini na matajiri, watu wote wanufaike iwe vijijini au mijini, iwe wazee au watoto, iwe aliyelipa kodi kihalali na asiyelipa kodi kihalali.

Wakati Mwalimu alipokuwa anahutubia, kuna mambo ambayo aliyalenga. Nchi hii siyo ya Ujamaa na Kujitegemea, tena ni nchi ya soko hurua, ni nchi ya uchumi mikononi mwa wafanyabiashara, ni nchi ambayo usipokuwa kiongozi makini, nchi inaweza kuongozwa na wafanyabiashara kwa namna wanayotaka wao.

Tumewahi kushuhudia ukiritimba uliojitokeza katika nishati ya mafuta ambapo watu wachache walihodhi biashara hiyo na kutaka kufanya watakavyo, walikuwa wakiongoza mustakabali wa bei, walikuwa na uwezo wa kuamua kulipa kodi ama la, kwa namna moja waliweza kuongoza nchi kwa matakwa yao hadi Serikali ilipoingilia kati angalau tukaanza kuona mambo yakiwa nafuu.

Siku za hivi karibuni tumeshuhudia nguvu ya wafanyabiashara katika sekta mbalimbali, wapo hata waliodiriki kuieleza Serikali kwamba iwapo haitafanya watakavyo wao basi watafanya mgomo baridi, naamini katika mgomo huo waathirika wakubwa watakuwa wananchi kwa kukosa huduma.

Serikali yoyote ambayo ni legelege itawasujudia wafanyabiashara ili iweze kuendelea kuwapo madarakani bila kashkash, lakini ukweli unabaki palepale kuwa itaelekezwa majukumu ya kiutendaji na wafanyabiashara, hicho ni kitendo cha kuidhalilisha dola ambayo inaongozwa na kiongozi aliyechaguliwa na wananchi.

Hivi sasa bado kuna wafanyabiashara wanaoibipu Serikali yetu kuona kama inaweza kuwasikiliza, wanataka Serikali iwasikilize na wao wafanye watakavyo, wanataka kuona Serikali ikishindwa kutoa huduma na kudhibiti baadhi ya mambo, wanataka wajidhihirishie uwepo wao, wanataka wasujudiwe, wanataka wasikilizwe. Ni wajibu wa Serikali makini kuwa macho na hawa watu wachache wenye kuleta madhara kwa siku zijazo.

Mheshimiwa Rais, ni vizuri ukajua kuwa kila kiongozi anajaribiwa kwa staili yake, wewe watakujaribu kwa staili yako na hatimaye wanaweza kuyumbisha utawala wako, wanaweza kutumia ujanja wa kuminya baadhi ya mianya midogo ambayo inawaathiri wananchi, wanaweza wakatumia ujanja wa kuwarubuni viongozi wenye uchu wa mali na kuiyumbisha Serikali yako.

Wito wangu; usimuonee haya mtu yeyote katika utekelezaji wa majukumu yako. Kama ni sukari hakikisha unawadhibiti kwa kosa la uhujumu uchumi, ni makosa kutumia nguvu ya fedha kuwanyanyasa watu wengine, sitaki kuamini kuwa sukari ina mipaka kwa wafanyabiashara kuinunua kama ilivyo kwa mbolea kwa maana ya ruzuku.

Hawa wamekubipu katika sukari lakini jiandae katika bidhaa na huduma nyingine kama mafuta. Ukiweza kuwadhibiti katika jambo dogo kama sukari, nakuhakikishia ‘watanyooka tu’ na hakuna atakayecheza na Serikali. Serikali inapaswa kuheshimiwa na kuogopwa hasa na wahujumu uchumi, wezi, mafisadi na wengineo.

Serikali inapaswa kuwa macho na wanaoitakia mabaya, iwapo mtu atataka kufanya atakavyo mpe kifungo cha maisha katika biashara yake, aende akalime, aone ni maumivu kiasi gani kusubiri huduma kwa ridhaa ya mtu baki.

Naamini walioficha sukari hawajui uchungu wa kukosa sukari, naamini hawana uzalendo na Taifa hili, naamini ni mamluki wanaofanya hivi kukukomesha ili uonekane huwezi kazi, naamini ukiwachukulia hatua za dhati kabisa watanyooka tu na kuwa watu wema. 

Haiwezekani mtu anunue sukari yote kiwandani halafu aamue yeye muda wa kuuza kwa bei anayotaka, huku ni kuichezea Serikali. Ukiangalia kwa undani lazima kuna namna ya ukiritimba ambayo imetengenezwa ili mnufaika awe mwenye kuinunua kutoka kiwandani na hapo ukifuatilia kuna namna ambayo ipo kwa maslahi binafsi na siyo Taifa. Kiufupi, kuna watu wanabipu kutaka kujua nguvu ya Serikali.

 

Wassalaam,

Mzee Zuzu,

Kiaptimo

1016 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!