Inawezekana nimeandika pia barua za kukurupuka wiki nyingi tu zilizopita, lakini dhambi hiyo hainiondoi kwenye kutazama wengine wanafanyaje katika maisha yao. 

Mara nyingi mtu hajioni kilema chake isipokuwa kilema cha mwingine, na katika hili huwa tunaona vilema vidogo na kusahau ulemavu wetu mkubwa. Narejea maneno matakatifu kwamba toa boriti katika jicho lako ndipo uweze kuona na utoe banzi katika jicho la mwenzio.

Kwa falsafa hii naomba nikiri kwamba nina boriti lakini hainizuii kumshauri mwenye banzi atoe ili nimuone vizuri. Haya ndiyo maisha ya kawaida ambayo ninajua wengi wetu, nikiwamo mimi, tunahusika katika kujadili na kusema mambo madogo ya watu bila kujitazama sisi wenyewe kwanza kama tupo sawasawa.

Naandika waraka wangu wa leo nikiwa na mambo mengi kichwani, hasa kutokana na majibizano mengi ambayo huwa yanajitokeza kila linapoibuka jambo ambalo wakati mwingine hatupaswi kulijadili sana kama mtazamo wa mtu mmoja tu. Tumekuwa kikosi kazi cha kukurupuka mno kwa mambo ya mpito.

Taifa letu linahitaji akili nyingi katika kipindi hiki cha kuelekea uchumi wa kati, hatuhitaji sana vijiwe nongwa kwa ajili ya kutazama boriti na banzi kwa wengine lakini tunahitaji kutazamana na kuongozana njia wote ili tufike tuendako. Kitu nilichojifunza, watu wengi wanapenda kufanya uchambuzi wa kina, tena kwa uhasi zaidi kuliko wao kutoa mawazo yao ili yachambuliwe.

Hali hii inaweza ikawa ni aina mpya ya ugonjwa ambao unaweza usijue tiba yake ni ipi. Mathalani siku chache hizi kumeibuka mjadala wenye hoja za ajabu sana katika suala la watumishi wa idara fulani. Mjadala huo umeinamia katika kigezo kimoja tu bila kuzingatia vigezo vingine, na kibaya zaidi ni pale ambapo tunatengeneza mjadala ambao hauwezi kutusaidia kitu katika kipindi ambacho tunapaswa kujadili kuhusu viongozi waliopatikana na wanaoendelea kujinadi kwa siku zijazo katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Nadhani tufike mahali tukubali kuwa kama taifa tunaongoza kwa miluzi mingi ya uwindaji maendeleo ya kutupeleka uchumi wa kati huku tukijua wazi kwamba hatufanyi kazi kwa jasho na wala hatufikirishi vichwa vyetu kwa mambo makubwa na ya msingi.

Taifa letu sasa hivi tumechagua vipaumbele vya kimajungu zaidi badala ya vya kimkakati. Sioni yakizungumzwa mambo ambayo yanaweza kutuvusha hapa tulipo na badala yake naiona mijadala na hoja za kimajungu katika kila jambo ambalo tunapaswa kuingiza miguu kwa ajili ya pato letu.

Ni kweli kwamba tuna wasomi wengi ambao ni chachu ya maendeleo yetu. Lakini pia ni kweli kwamba elimu yao haijaanza kutumika katika kulisaidia taifa. Yawezekana wamegubikwa na kundi kubwa la watu ambao hawajasoma kiasi cha kushindwa kujibu hoja zao. Lakini pia ni kweli kwamba hata hao wasomi ambao taifa limewekeza kwa miongoni mwao wapo ambao wameamua kuweka rehani vyeti na kuanza kujibizana na hawa wasiosoma. Tofauti yao labda itakuwa lugha lakini si mawazo.

Taifa letu linahitaji kupita katika reli za kimaendeleo na si katika njia ya mkato ambayo inaelekezwa kwa mdomo wa mtu aliyeko kitandani. Taifa linahitaji maarifa tuliyowekeza kwa wasomi ili waweze kufanya kazi na si siasa. Taifa linatakiwa kuacha siasa ifanyike lakini uamuzi mgumu ufanyike kitaalamu. Kama taifa hapa miluzi imekuwa mingi hadi tunampoteza mwindaji katika harakati za kupata kitoweo.

Watanzania tuna muda mwingi wa kujadili vitu vidogo na kuvikuza, na isivyo bahati vitu hivyo tunavyojadili havina tija kwa taifa. Hilo la kwanza. La pili, Watanzania tunapenda kukosoa zaidi hata jambo jema kwa kuamini kwamba kwa kufanya hivyo tunatumia vizuri demokrasia yetu ilhali tukijitukanisha wenyewe katika macho ya wanaoona kwa kina.

Sisi wengine ndiyo siku zetu za kuishi zipo mlangoni. Tunaangalia nyie wasomi wanasiasa wanaharakati na wananchi mtazamo wenu katika maendeleo ya taifa ambalo tulipigania uhuru wake kwa nafasi yetu na kuwaachia taifa salama likiwa huru ili muliendeleze. Siamini kama taifa litaendelea kwa maneno mengi ya kubishana vitu ambavyo ni dhahiri.

Pokeeni salamu zangu na laana inawasubiri kwa mtindo huu. Laiti tungelijua kizazi chenu na aina ya maisha mliyochagua labda tusingetoa damu na jasho ili tujitawale. Nikiangalia makaburi ya mashujaa wa uhuru najihisi mpweke niliyebakia, wenzangu wapambanaji walitangulia.     

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri