Japo ni vigumu kukubali maelezo ya sasa kutoka katika kizazi kipya, nina kila sababu ya kuwasimulia maisha halisi ambayo sisi tuliishi kwa wakati wetu, hasa nyakati za nguo moja na sabuni za foleni katika duka la ushirika au la kijiji.

Leo dunia imebadilika sana. Kuna bomba kila mahali, kuna nguo lukuki, kuna mafuta ya kupaka, kuna usafiri, pia kuna unyunyu wa kila aina.

Inawezekana nikawa nimegusa jambo dogo sana katika ujio huu, lakini niseme kitu kwamba suala la ujio wa wageni limetufanya tujue wajibu wetu katika baadhi ya mambo ya msingi. Mathalani, kuishi kwa matumaini makubwa na kujikasirisha bila sababu ya msingi, bali uvivu wetu.

Nimefurahi baada ya kusikia kwamba wageni wetu wamepokewa vizuri katika viwanja vyetu vya ndege. Sikufika huko mjini, lakini sifa zimefika huku Kipatimo. Sikufika kwa sababu sitaki kutia aibu, lakini taarifa nilizonazo nasikia ukumbi ulinoga na mambo yalifana kuanzia maonyesho hadi malazi – achilia mbali mapokezi ya kihistoria.

Sikuwahi kufikiria juu ya usafi kama ni sehemu muhimu ya kumfanya mgeni afurahie mahali, lakini nilijiuliza mara kadhaa ninapokwenda katika nyumba safi huwa najisikiaje? Na je, katika nyumba zetu zile chafu chafu huwa najisikiaje? Kimsingi huenda jambo la usafi wengi hawakulielewa katika maelezo ya kwanza, lakini wazoefu tulielewa.

Usafi haukumaanisha kuoga na kuvaa nguo safi, ulimaanisha mbali sana. Lugha tunavyoitumia kwa wageni wetu, ukarimu ambao unatokana na adabu ya lugha, usafi wa taarifa rasmi na hasa katika mambo mengi ya kusifia na uzalendo kwa taifa letu, na usafi wa tabia mwanana kwa wageni wetu badala ya uchafu wa tabia za kijinga.

Usafi wa mambo yahusuyo taifa kama kioo cha kuitangaza nchi yetu, tuna nini ambacho kitafurahisha macho yao katika utalii, siasa, uwekezaji, utamaduni na yote yanayoendana na hayo; usafi katika kuzuia mambo ya wengine hasa ambao utamaduni wetu na wao umetutofautisha, mambo ya ushoga na kukiuka haki za binadamu.

Inawezekana kuna mahali tulipitiwa. Hilo liwe funzo na tulirekebishe mapema ili tusirudi tulikokosea. Huu uwe mwanzo wa kuendeleza utamaduni wa kuwa wasafi si katika kuoga na kuvaa nguo safi tu, bali katika mambo yote yanayopaswa kuwa wazi kama vile katika maeneo wageni wanaanza kukutana nayo, iwe uwanja wa ndege au katika mipaka yetu.

Ile tabia ya miaka ya nyuma ya uzalendo na upendo kwa wageni wetu tuirejeshe. Suala la kuiga tabia ambazo si zetu na kuichafua sura ya nchi lisiwe kipaumbele. Tuonyeshe kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani na thamani yetu ya kuzitafutia uhuru baadhi ya nchi ibaki kuwa na maana na watuheshimu wakati wote.

Lazima tupongezane kwa wote waliokutana na wageni na kuwatendea haki ambayo Watanzania tuliwatuma watuwakilishe, na hata wale ambao watapokea vijiti vya kazi wasipokee majukumu peke yake, bali wapokee na ukarimu ambao ndio taarifa kamili ya taifa analoingia mgeni.

Sasa wageni wameondoka. Haimaanishi ndiyo tuwe wachafu tena katika maeneo yetu hasa yale ya jamii. Wageni wameondoka haimaanishi ndiyo hotelini tuwe na majibu ya ovyo kwa wateja kwa kuwa si wale ambao tulijipanga kujipambanua tabia zetu, wageni wameondoka tusibadilishe wapokea wageni kuanzia uwanja wa ndege, hotelini na hata madukani.

Tulichokifanya wakati wa ugeni ilikuwa ni kusafisha njia ili tuweze kuwaonyesha wenzetu sisi ni wakarimu kiasi gani. Tulichokifanya ni kuwakaribisha warudi tena waone wanyama wetu na vivutio vingine. Tulichokifanya tuna matarajio ya kuwaona tena wakija na wawekezaji mbalimbali katika sekta nyingi ili taifa lipate mapato na wananchi wapate ajira.

Wapo watakaokataa kuwa na mawazo yangu, lakini ukweli ni ule ule kwamba lazima tukubali usafi na ukarimu ni nguzo ya maendeleo kwa kila mtu, iwe binafsi au taifa. Nimependa usafi japo ninahofia hali itakuwaje kwa wale wenzangu na miye wanaooga siku ya safari.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

101 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!