Kuna watu wanaona kama maisha yamekuwa magumu kupitiliza, mimi nawaunga mkono kwamba maisha ya sasa ni shughuli pevu kwelikweli kutokana na ukweli wa mabadiliko ya sera. Tulianza kwa kushangilia hotuba mbalimbali za viongozi na matamko ambayo baadhi yetu hatukuelewa kwamba tunarudi Tanzania ambayo ilikuwa imepotea.

Leo hii kila kaya, kila kona na kila mtu wimbo ni mmoja tu kwamba maisha ni magumu. Kwangu mimi sijawahi kuwa na maisha mepesi, hivyo najaribu kutumia fursa hii kufanya utafiti ambao kimsingi siyo rasmi sana na kwa kuwa halijumuishi maeneo tofauti unaweza kuwa utafiti wa kikanda, huko kwingine nitapokea taarifa ya mdomo na kuiingiza katika utafiti wangu.

Nimependa kufanya utafiti ambao mimi nimo katika hali ya kawaida kuwa nayo, nimependa utafiti kwa kuwa ninaofanya nao utafiti hawawezi kunidanganya, wanaweza kujieleza kwa vinywa vyao na pia wanaweza kujionesha pasi na shaka ukweli ulivyo.

Maisha ni magumu kwa mujibu wa maelezo yao, lakini ukiwauliza yameanza lini kuwa magumu jibu ni moja tu wakiilaumu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani na kuanza kutekeleza sera za ‘hapa kazi tu’, maisha ni magumu kwa sababu baadhi ya mambo yaliyokuwa yakifanyika awamu nyingine sasa ni kama hadithi unayofanya kumbukumbu tu lakini kiuhalisia huwezi kukutana nayo tena.

Utafiti wangu umejikita katika mambo madogo madogo ya uswahili ambako wahenga walisema kuna vituko, na utafiti huu ningelipenda hii Serikali ya Awamu ya Tano iupokee kama hadidu rejea za kufanyika kazi vizuri zaidi katika kuboresha maisha na uwajibikaji kwa ujumla wa Tanzania mpya ijayo, iwapo tu malengo iliyojiwekea yatakamilika.

Mosi, kwa hali ya kawaida huku uswahilini ratiba ya mlo imebadilika sana, badala ya milo mitatu ya kusuasua sasa ni rasmi imekuwa miwili ya kusuasua na iwapo hali itaendelea kukaza zaidi na hakika unaweza kuwa mlo mmoja wa kusuasua, lakini upendo katika ndoa umeimarika zaidi kuliko awamu nyingine zilizopita.

Pili, utafiti wangu umebainisha kuwa vijitabu vidogo vya hesabu za mapato na matumizi sasa vinatumika ipasavyo, vitabu hivi vinatunzwa vizuri na kufuatilia matumizi zaidi kwa familia nzima, mapato ya waume yapo wazi kwa wenza wao japo kwa mbali mapato ya wanawake yanaukakasi kidogo kukamilika kujulikana rasmi hasa hela ya mchezo.

Utafiti unaonesha kuwa wanaume wengi hivi sasa wanajua gharama za vitu vidogovidogo, hili ni jambo jema kwa familia kwa kuwa kuna ushirika wa lazima kukabiliana na ugumu wa maisha, ile misemo ya kijingajinga uswahilini imekwisha sasa kuna adabu na kuna uwajibikaji.

Utafiti bado unaonesha kuwa kule kubweteka na kutembeleana kusikokuwa na lazima kumeanza kudhibitiwa na baadhi ya familia, urafiki wa kula na kulala umekwisha, ushoga wa kusogoa muda wa kazi haupo tena, ukarimu wa kutoa bila kuzingatia haupo.

Utafiti unaonesha kuwa suala la kubana matumizi limeshika kasi, watu hawawashi taa ovyo kabla ya giza na suala la kucheza na chenchi halipo tena, thamani ya shilingi mia ipo katika familia, matumizi ya anasa kama kuoga maji moto, kupaka kucha rangi, kununua sare za sherehe, kuwa na mboga mbadala, kunywa bia, maji ya chupa, na soda kwa ujumla wake hayapo tena.

Utafiti unaonesha kuwa watu wengi wanafuatilia mambo ya siasa na kuona jinsi wanasiasa wanavyoweza kupunguza makali ya maisha yao, watu wengi hawaangalii tamthilia badala yake wamejikita katika taarifa za habari na kadhalika.

Bado naendela na utafiti wangu lakini kikubwa nilichogundua ni mabadiliko ya kimaisha kwa Watanzania ambao hawakuwa tayari kubadilika kabla ya awamu ya tano kuingia madarakani. Ombi langu rasmi ni kwamba mabadiliko ni muhimu sana lakini kasi nayo tuiangalie maana inaweza ikaathiri maisha ya wavivu na kuamua kuingia katika matendo maovu.

Naangalia namna ya vipato huku uswahilini na jinsi mianya hiyo inavyokatwa, hizi baa zinazofungwa kila siku, hizi ofisi zinazofungwa kila siku, hizi sheria mpya za bodaboda, kudai risiti, kuzuia viroba n.k., ni mtihani mwingine kwa familia za uswahilini.

Naendelea na utafiti usio rasmi.

 

Wasaalam

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1139 Total Views 5 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!