Nakumbuka siku moja mkuu wa kaya alisema atahakikisha rasilimali za Watanzania zinarudi mikononi mwa Watanzania. Wapo waliokebehi kauli hiyo lakini wapo walioelewa kuwa atajaribu kwa kipindi chake na wapo walioapiza kuwa huyu jamaa akisema jambo anamaanisha.
Mpaka leo mimi sijajua niangukie upande gani, japokuwa kimuhemuhe ninachokiona ni kwa baadhi kusemea mbali kwamba spidi anayoenda nayo inaweza ikakwama kwa sababu waliofanya mambo mengi ya hovyo ndiyo waliopo juu ya sheria sasa na wakati huo.

Baadhi ya watu walio ndani ya nchi na nje ya nchi wanapongeza hizi jitihada, wanaopongeza ni wale ambao wanajua kuwa taifa lolote lina wananchi ambao kwa pamoja wanatakiwa kula matunda ya faida ya taifa lao, nakubaliana na wote wenye dhana hii ya kufaidi au kuumia kama taifa.
Leo nimeona ni vema nikashika kalamu na kutoa ushauri wangu kwa mkuu wa kaya kwa nia njema, najua siyo lazima atekeleze na kupokea maoni yangu lakini ikimpendeza siku moja akumbuke niliwahi kutoa ushauri na autumie.
Taifa letu limeingia katika giza nene la maisha magumu kwa watu wote, wapo ambao ugumu huu ulikuwa jambo la kawaida tangu wakizaliwa katika familia duni na wapo ambao sasa wanaanza kujua ugumu wa maisha maana yake ni nini, sisi wachache ambao hatukuwa wateule tulizowea maisha magumu tukiamini kwamba siku moja kabla hatujaifungia macho dunia tutafaidi matunda ya uhuru wetu.

Mheshimiwa mkuu wa kaya, kwanza tupo pamoja katika sakata hili la kujiletea maendeleo na kuweza kujitegemea, naamini katika misimamo yako na ninaamini unachofanya kwa dhati ya moyo wako, sina hakika kama umetokea katika familia duni ama la, ninachoamini ni kwamba ukubwani uliingia katika kundi la watu wasioomba chumvi na pia katika kundi la milo mitatu.
Najua lengo lako ni lipi, kwanza utii wa sheria na kwamba hayuko aliye juu ya sheria, hili nakumbuka tangu enzi za TANU lilikuwa ni lengo tulilojiwekea kama Watanganyika huru wakati huo, tulisema kila Mtanzania ana haki na mali za taifa ni sehemu ya umiliki wake na hatutabaguana kwa rangi, kabila, elimu, wala kipato. Hiyo ilikuwa ni nadhiri yetu tuliyojiwekea kwa nia ya kuliendeleza Taifa.

Miaka michache ilipofika na hasa baada ya kuhakikisha tumejenga shule za kutosha kwa watoto wetu na baada ya kuanzisha viwanda vya kutosha tukasema uchumi wa Taifa letu utategemea kilimo na ufugaji, kwa hakika kila mtu atakumbuka jinsi ambavyo kama taifa tulivyoingia kwa nguvu katika kilimo na kuanzisha maazimio ya kutosha ya kilimo.
Hatukuwahi kufikiria kwamba madini na kodi ni sehemu ya mapato ya Taifa hili, tulisema kilimo na viwanda ni ukombozi kwa Taifa letu, Taifa lilikuwa na wasomi wachache sana wengi wetu tulisoma ngumbaru jioni saa kumi baada ya kilimo cha kufa na kupona, kilimo hiki cha wakati huo hakikuwahi kumwacha mtu salama kwa cheo chake au mali yake.

Ulipoingia madarakani ulianza kuchukua hatua kali kwa baadhi ya watendaji wako, ulichukua hatua kali kwa baadhi ya wakwepa kodi na wanaolidhulumu Taifa kwa namna moja ama nyingine, katika utekelezaji wa azima hiyo kuna watu ambao kwa namna moja ama nyingine waliguswa na sakata hili na bado wengi wetu tunaguswa na sakata hili la kuwadhibiti wachache ambao waligeuza Taifa hili kuwa shamba la bibi.
Una kazi nzito yenye nia njema lakini isivyobahati inafanyika katika mazingira magumu na hatari kwa watu wengi ambao kimsingi hawakuwa na hatia yoyote wakati ule wa ufilisi wa Taifa letu, wapo ambao waliajiriwa na hao na wapo ambao walikuwa watumwa kwa hao kutokana na kuweza kushika njia za kiuchumi ambazo sasa unazirudisha kwa wenye kaya.

Najua unajua kuwa watu wengi wanapata adhabu ambayo hawastahili lakini ni lazima tupite huko ili tujue tunatokea wapi, najua unajua manung’uniko ya walio wengi juu ya maisha yalivyo magumu na lengo lako ni kutaka kuyafanya maisha bora kwa watu wote.
Maisha ni magumu sana huku, mimi na baadhi ya wazee wenzangu sasa tumekata tamaa, tunaona kama tutafunga macho bila kuona matunda ya Taifa letu, tulipigania uhuru, tukapigana na vita ya maradhi, ujinga na umaskini, tukapigana vita ya miezi kumi na nane, tukapigana na vita ya mateso ya ufisadi, siasa majitaka na sasa vita yako ya kuturudisha katika mstari.
Chonde chonde mkuu wa kaya legeza kidogo ili nasi tufe tukiwa tunahema, tumebakiza siku chache sana za kuishi lakini pia waliotufikisha hapa wanajulikana kamata hao peke yao. Nakutakia kazi njema na huruma ikutangulie.

Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo.

By Jamhuri