Yah: Wazazi wahuni tukizeeka itakuwaje?

Nimepata barua na arafa nyingi kutoka kwa wasomaji wa uga huu kuhusu madhara ya kufuga uhuni wa ujanani mpaka kuutumia uzeeni. 

Kimsingi si kweli kwamba nilikuwa ninataka watu ambao ni vijana wa leo waje wautumie ujana wao uzeeni, hapana, bali ilikuwa kuuona ujana wa leo katika uzee wa kesho.

Najua kwamba nimepitwa na wakati, lakini pia ninajua kwamba teknolojia imetamalaki sana leo, lakini pia ninajua kwamba vyote hivyo vimekuja na vimeukuta utamaduni wetu, tatizo linaanza pale ambapo tunataka mambo ya kigeni yapoteze mila na desturi zetu.

Katika waraka wangu nilijaribu kukumbuka maneno ya hekima ambayo tulikuwa tukipewa kila iitwapo jioni ya siku hiyo, tulipewa mawaidha mbalimbali ambayo hayakuhusu wakati huo peke yake bali yalihusu mpaka wakati huu nikiishi bila babu na bibi.

Katika chakula chetu cha jioni nilifunzwa namna nzuri ya kula mbele za watu, nilifunzwa namna ya kushiriki chakula cha pamoja, sikupakuliwa nile peke yangu hata pale nilipokuwa ninaumwa, na vivyo hivyo nilifunzwa namna ya kula na mgonjwa au asiyejiweza, nilikuwa ninatengenezewa upendo kwa wenzangu pia kufundishwa kuacha tabia za kuwa mnyimi.

Babu na bibi walijua wajibu wao kwangu juu ya maongezi yangu na tabia kwa ujumla, kwa ufupi walinilandisha na wana wao ambao ndio wazazi wangu, nilijisikia fahari kila ninapopongezwa kwa jambo la kishujaa lakini pia nilijisikia mnyonge kila ninapohukumiwa kwa kosa nililolifanya.

Zamani ni zamani na labda ndiyo sababu watu wengi hawapendi zamani, zamani kila mtu aliyekuzidi umri alikuwa baba au kaka bila kujali kama mnafahamiana ama la, kila mtu alikuwa na mamlaka ya kukufundisha pale ulipokosea, tulipokosea huko mbali tulitandikwa.Mtandikaji haikumlazimu kumjua mzazi wako lakini alipohitaji kumuona alifanya hivyo na alipewa shukurani na mzazi kisha mtandikaji anapoondoka unaanza upya kupokea stahiki yako ya adhabu kwa kosa lililotolewa adhabu tayari, leo nasikia hiyo ni kesi ya polisi.

Tumefikia hapo kwa sababu wazazi wengi wa leo ndio kile kizazi cha hovyo kilichoingia katika malezi yasiyo ya utamaduni wetu, ndio wazazi wenye tabia za hovyo wakiamini malezi ya mtoto wanapaswa kuyafanya wao wenyewe na si jirani, watoto wana vibali vya kuporomosha matusi na mtu mzima hauna haki ya kumkanya.

Hiki ndicho kizazi ambacho kimeasi maadili yetu na kuleta utamaduni mpya ambao unapotosha watoto wengine na kudhani kwamba kuanza kuangalia picha za utupu ni haki, kubaka ni haki, kutukana ni haki, kupora ni ujanja, kutapeli ni akili, kutofanya kazi ni wajibu na kudai demokrasia ya kuvunja maadili ni sehemu ya maisha yao.

Kizazi hiki ndicho kitatoa wazee wenye busara katika miaka michache ijayo, ndicho ambacho kinaweza kutoa ushauri wa maana iwapo kuna tatizo, kizazi hiki ndicho kililelewa na kizazi cha hovyo na kisha kikapatikana. Ninachelea kusema ni kizazi kisicho na wazazi wanaoishi pamoja, ni kizazi cha watoto yatima wenye wazazi walio hai.

Najua kwamba kila mtu angependa kuona mwanae yuko katika mikono salama ya jirani, lakini si dunia ya wazazi wa leo, kila mzazi angependa kuona watoto wanacheza pamoja mtaani lakini si watoto wenye malezi tofauti ya leo, malezi ya usasa wa kipumbavu.

Imani imekwisha baina ya mtu na mtu, hakuna tena imani baina ya mtu na jirani yake, leo kimefika kipindi ambacho hata ndugu wa kawaida ni vigumu kumwachia watoto, haya ndiyo maendeleo ambayo mimi ninayaona tunayakaribisha kwa mikono miwili.

Najaribu kufikiria jambo dogo la malezi linavyobomoa utamaduni wetu na bado watu hawaoni athari kubwa tuiletayo kwa kisingizio cha maendeleo, maendeleo gani ni suala jingine kwa sababu walioendelea ndio wanaotusaidia kuzitunza familia zetu zinazoparaganyika kwa kisingizio cha maendeleo.

Ifike mahali tujiulize, sisi wazazi tukizeeka itakuwaje na haya mambo yetu ya kihuni? Au hata wahuni wakizeeka nao wana busara zao? Nini matokeo ya wahuni wakizeeka? Au ndiyo tutasingizia chanjo zimetuathiri na si ujinga wetu wenyewe?

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.