Kuna wakati natamani niandike waraka wangu kama ule wa zamani, kwa kutumia lugha yetu, lakini naona kama dunia ya leo imebadilika kiasi kwamba hampendi mambo mengi zaidi ya mambo, vipi? Huwa sipendi salamu hizi.

Leo nimeamka nikiwa na hisia tofauti kabisa, nikaamua kukuandikia Mheshimiwa Rais wangu waraka huu ambao naamini una upendo na unajua nataka kusema nini, lengo si kukukumbusha, la hasha! Ni kuwakumbusha wengine walio chini yako juu ya suala la amani na furaha kwa wenye ualbino.

Kwa kumbukumbu zangu za uhakika, suala hili uliwahi kulizungumzia na ninajua kwamba lilikugusa sana na Watanzania wengine liliwagusa vivyo hivyo, na matokeo yalianza kuonekana dhahiri kwa kupitia baadhi ya hukumu na tahadhari inayochukuliwa kwa wenzetu wenye ualbino.

Mheshimiwa Rais, jambo hili limetugusa sisi wenye uelewa wa chini na wenye imani za kishirikina, baadhi yao ni wafanyabiashara wakubwa na viongozi wengine ambao kwa namna moja wana imani potofu juu ya binadamu wenzao.

Hivi karibuni tumesikia matukio ya watoto wadogo wakifanyiwa ukatili, inauma sana, naamini vyombo vya sheria havitalifumbia macho jambo hili kama ambavyo wenzetu walivyotafutwa na wenye imani potofu kwa miaka mingi sasa. Napenda kutamka kitu lakini, nahisi nitakuwa nimevunja na kuibagaza Katiba yetu ya nchi, lakini elewa hivyo, nilitaka kusema hivyo bila kuzingatia maelekezo ya Katiba yetu.

Ningependa kuendelea kusikia kauli yako ya kupinga mambo haya kila wakati na hasa katika mikutano yako ya hadhara ambayo unaifanya mara kwa mara. Hili suala la kuamini watoto wadogo na wenzetu wenye ualbino ni sehemu ya mafanikio yao halikubaliki hata kidogo kwa jamii iliyostaarabika.

Narudi kwako Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, najua una mambo mengi unayofuatilia, inawezekana hili pia ni kipaumbele chako, kwako sioni shida sana kushauri kwamba ifike wakati tuamue kuunda tume kabisa ya kutokomeza waganga wa jadi ambao wengi wao ni matapeli wakubwa.

Sioni soni kutamka bayana kwamba tumeanzisha kampeni maalumu ya kutajana huku mitaani kwa watu ambao tunadhani wana tabia hizo ili ikiwezekana tusaidie vyombo vyako vya dola kuwakamata na kutoa ushahidi.

Kuna tatizo kubwa la ushahidi wa mambo haya, lakini nikwambie kwamba Watanzania hawa wamekuwa na tatizo kwa sababu watu wengi tuliowatuhumu wanaachiliwa ama kwa dhamana na kuingia tena mitaani wakiwa na makandokando yale yale, wanatuogofya na kututisha kiasi cha kutufanya tuogope kwenda kutoa ushahidi mahakamani.

Tumekuwa tukiishi kwa hofu mitaani na watoto wetu, tumekuwa tukiishi kwa wasiwasi na wenzetu wenye ualbino, kisa, wapo wenye imani zao na tunawatazama kama watu wasio na hatia, tunapata taabu sana ambayo wengine wasiofikwa na masahibu haya hawawezi kuelewa tunasema nini.

Mheshimiwa waziri, naomba upokee waraka wangu na uufanyie kazi iwapo itakupendeza, katika majukumu yako mengi hili pia liweke katika vipaumbele vyako, sisi tuliotangulia miaka tunaogopa kuulizwa siku ya kiama tuliitendea nini jamii ya wenye ualbino na watoto wadogo.

Nawaandikia waheshimiwa wabunge waraka huu, naomba mpokee kama mnavyopokea miongozo, jambo hili ni hatari sana kwa mustakabali wa maisha ya mnaowawakilisha huko bungeni. Nawaombeni mpitie mikataba mbalimbali ya haki za binadamu na muangalie ipi ambayo haijasainiwa na sababu zake ni zipi, inauma sana.

Nakuandikia IGP si kwa sababu hufanyi kazi, nataka kukukumbusha yaliyotokea Njombe na Simiyu na ikikupendeza angalia mafaili ya watuhumiwa wa mauaji ya wenye ualbino nchi nzima ili uone ni watu wangapi wamekamatwa na wangapi wamehukumiwa kwa idadi ya kesi zilizopo. Naujua ugumu uliopo lakini nalijua sekeseke lako na hasa hili la hapa jirani Kilwa hivi karibuni. Ukiamua utalimaliza mara moja.

Nawaandikia ‘ma-RPC’ wote nchini, ikiwa mtashindwa kupata namna ya kutulinda, basi ombeni msaada kwa wengine, wote tuna haki ya kuishi na kwenda popote tutakako, ni haki yetu ya msingi kuwa huru na tukiwa na amani.

Nawaandikia viongozi wa dini, wanasheria, asasi zote, mzazi, Mtanzania mwenzangu, rafiki yangu, ndugu na wanangu wote. Najua mnajua nilichoandika, najua mnawajua wanaofanya ukatili huu, sasa tuseme inatosha na hatua stahiki tuzichukue, tukisema hapana itawezekana, imani potofu za kishirikina zinaweza kufutwa kwa kuelimishwa elimu dunia na elimu ahera.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri