Yaliyojiri mkutano wa EU, AU Ubelgiji

Na Nizar K Visram

Wakuu wa nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU) walikutana mjini Brussels, Ubelgiji, Februari 17 na 18, mwaka huu. 

Viongozi 40 wa nchi na serikali za Afrika na viongozi 27 wa Ulaya walikutana katika mkutano wa kilele wa EU na AU ambao hufanyika kila baada ya miaka mitatu; hii ikiwa ni mara ya sita. 

Lengo la mkutano lilikuwa kuleta mageuzi katika uhusiano wa Ulaya na Afrika. Kaulimbiu ilikuwa; ‘Maono ya Pamoja Kuelekea 2030’.

Mageuzi haya yanatarajiwa kuletwa kwa kubuni mipango ya uwekezaji katika nyanja kama Uviko-19, mabadiliko ya tabia nchi, usalama na utawala bora. 

Viongozi wakazungumzia mada kadhaa kwa minajili ya kuanzisha miradi mbalimbali katika nyanja zote. Pia walialikwa wataalamu na washauri.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambaye ni Mwenyekiti wa EU, alisema chini ya uongozi wake uhusiano wa EU na Afrika utapewa kipaumbele kwa sababu umekuwa ukisuasua. 

“Wakati sasa umefika kuleta mageuzi,” anasema Macron. 

Mkutano wa tano kama huu ulifanyika jijini Abidjan, Ivory Coast, Novemba 2017, kisha mkutano wa sita ukapangwa kufanyika Novemba 2020, lakini kutokana na mlipuko wa Uviko-19 ukaahirishwa hadi majuzi.

Mwaka jana EU ilitangaza mpango kabambe wa uwekezaji wa kimataifa (Global Gateway), lengo likiwa kuwekeza dola bilioni 341 ifikapo mwaka 2027.

Rais wa Tume ya EU, Ursula von der Leyen, alitembelea Senegal akakutana na Rais Macky Sall ambaye ni Mwenyekiti wa AU. Ursula akatangaza kuwa chini ya mpango huu hatua ya kwanza ni kuwekeza dola bilioni 170 barani Afrika. 

Haya yalizungumzwa katika mkutano wa Brussels, ndipo kila nchi ikawa inavutia kwake. Wachambuzi wanasema kitu kimoja ambacho hakikuonekana ni AU kuwa na msimamo na mkakati wa pamoja kama jumuiya uliowekwa mbele ya EU.

Mpango huu wa Global Gateway umebuniwa na EU kukabiliana na China ambao tayari wana mpango wa uwekezaji wa kimataifa (Belt and Road). 

Hata Marekani nayo imeingia katika ushindani kwa kubuni mpango wake wa uwekezaji unaoitwa ujenzi wa dunia bora (Build Back Better World).

Jitihada hizi za EU kuimarisha uhusiano na Afrika zinakabiliwa na changamoto kadhaa. Mshindani mkubwa wa EU barani Afrika ni China ambayo mwaka jana ilikutana na wakuu wa Afrika mjini Dakar (Senegal). 

Mkutano huo uliitwa ‘Ulingo wa Ushirikano wa China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation – FOCAC)’.

Leo China ni mshirika na mkopeshaji mkubwa barani Afrika. Mwaka 2020, EU ilikuwa inaongoza katika biashara na Afrika, ikifuatiwa na China. Leo China inaongoza na EU ni ya pili.

Mradi wa ‘Belt and Road’ ni mtandao wa mawasiliano na usafirishaji unaounganisha China na nchi 138 duniani, kuanzia Italia hadi Saudia na Cambodia, ukijumuisha miradi ya bandari, reli, barabara na daraja, umeme na kadhalika.

EU haikabiliwi na China pekee bali kuna washindani wengine. 

Nchi nyingine ambazo zimekuwa zikikutana na wakuu wa Afrika ni Marekani, Japan, Uingereza na Uturuki. Saudi Arabia nayo inaandaa kukutana na watawala wa Afrika.

Urusi inapanga mkutano wa kilele na Afrika mwishoni mwa mwaka huu. Urusi tayari inatuma Afrika askari wake wa kukodiwa wanaojulikana kama ‘Wagner Group’. 

Hawa wanapambana na wana-jihad walioko Sahel, Afrika ya Kati na Msumbiji. Nchini Mali majeshi ya Ufaransa yamefukuzwa na nafasi yao imechukuliwa na Wagner. Hili pia lilizungumzwa katika mkutano wa kilele. 

Afrika inawavutia wawekezaji na wakopeshaji wa duniani kwa sababu uchumi wake unakua kwa haraka. Hivi sasa uchumi wake unashika nafasi ya nane duniani na ifikapo mwaka 2063 utapanda na kufikia nafasi ya tatu. 

Maana yake uchumi wetu utazishinda nchi kama Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na India.

Ni vizuri wakuu wa Afrika wakatambua ukweli huu, kwani wengi wao wakikutana na wakuu wa EU na kwingineko huwa wanafikiria jinsi ya kupata ‘misaada’. 

Ndiyo maana huko Umoja wa Mataifa (UN), kwa mfano, inapokuja kupiga kura dhidi ya ubaguzi (ukaburu) wa Israel, nchi za Kiafrika hugawanyika kwa misingi ya ‘misaada’ ambayo ndiyo huamua jinsi ya kupiga kura na wala si msimamo au itikadi. Kwa wengine hii ndiyo ‘diplomasia ya kiuchumi’.

Mfano mwingine ni kikundi cha G-20 kinachokutanisha nchi takriban 20 kwa lengo la kuamua sera za kisiasa, kibiashara na kiuchumi duniani. Ni nchi moja tu ya Kiafrika (Afrika Kusini) mwanachama wake, wakati Ulaya na Marekani ya Kusini zina wanachama wasiopungua watatu kila moja. EU inaingia kama jumuiya wakati AU haimo. 

Mwaka 2016 China ilipokuwa mwenyekiti wa G20 lilipitishwa azimio la kuendeleza viwanda Afrika. Mwaka uliofuata Ujerumani ikashika hatamu na likapitishwa azimio la kuwekeza katika Afrika. 

Mwaka 2021 chini ya uongozi wa Italia likaanzishwa jopo la washauri kuhusu Afrika.

Uamuzi wote huu huchukuliwa na G20 wakati Afrika ikiwa na usemi mdogo sana. Hilo jopo la Afrika lilikuwa na wajumbe 12 kutoka nje ya G20, likiongozwa na mwenyekiti asiye Mwafrika. 

Wanajopo waliokuwa na nguvu zaidi ni kutoka IMF na Shirikisho la Nchi Tajiri (OECD). Afrika ilipewa nafasi ya kupokea ushauri.

Ndiyo maana unakuta katika uchumi wa dunia nzima hisa ya Afrika ni chini ya asilimia nne tu. Wakati ulimwengu  umekumbwa na Uviko-19 Afrika imepokea asilimia tatu tu ya dozi zote zilizozalishwa duniani. Huu ndio mfumo wa kimataifa unaotawaliwa na mataifa tajiri katika vikao vyao kama G20, Davos, IMF na Paris Club.

Suala la Uviko–19 lilizungumzwa huko Brussels. Nchi kama Afrika Kusini zilitaka kuzalisha chanjo kwa ajili ya Afrika lakini EU ilikataa kuruhusu kwa sababu wao ndio wavumbuzi na ndio wenye hakimiliki. Wanachotaka ni Afrika iendelee kupokea misaada ya dozi kutoka kwao.

Hii ilimkwaza sana Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini naye akasema:  “Tumewaomba waondoe kwa muda hakimiliki zao ili nasi tuweze kuzalisha chanjo lakini wamekataa. Wanataka tuendelee kutegemea makombo kutoka kwao.”

Profesa Lorenzo Kamel wa Chuo Kikuu cha Bologna, Italia, anayefundisha historia ya ukoloni na ukoloni mamboleo, amesema wakati tunazungumzia maendeleo katika Bara la Afrika ni lazima tuangalie jinsi Bara la Ulaya linavyoendelea kulinyonya Bara la Afrika:

“Sehemu kubwa ya fedha zinazotokana na maliasili ya Afrika kama dhahabu, mafuta, gesi na kadhalika zinachukuliwa na kampuni za Ulaya na Marekani na kuwekwa katika benki za siri huko kwao. 

“Utafiti uliofanywa na Panama Papers umedhihirisha kuwa kuna kampuni takriban 1,400 ambazo zinatorosha fedha kutoka nchi maskini duniani. Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema Afrika inapoteza dola bilioni 50 kila mwaka.”

Ripoti moja inasema EU imesaini mikataba 10 ya uvuvi katika bahari za Afrika. Ili walipe mrabaha meli za uvuvi zinatakiwa ziwasilishe thamani ya samaki wanaovua. Wanachofanya ni kupunguza thamani ili kukwepa tozo. Nchini Senegal walisema ni dola milioni 11 kumbe ni milioni 19. Nchini Guinea-Bissau walisema milioni 5 badala ya milioni 8.6

Wakati huohuo meli za uvuvi kutoka nchi nne za EU – Ugiriki, Italia, Ureno na Hispania – zimekuwa zikivua katika bahari za Gambia na Guinea ya Ikweta bila kibali cha serikali. Meli 19 kutoka EU zilikuwa zikivua wakiwa na vibali bandia.

Suala hili lilitetwa mbele ya Bunge la EU. Wabunge walitakiwa wapige kura kuzuia ruzuku kwa meli hizo za kitapeli lakini azimio halikupita.

Maswali kama haya yalitakiwa yaibuliwe na kuhojiwa na AU katika mkutano wa Brussels badala ya kuzungumzia misaada tu. Afrika ilitakiwa ipinge nchi za EU kutoa ruzuku kwa meli zinazoendelea kupora samaki wa Afrika bila kibali na bila mrabaha.

 [email protected]

0693 555373