Yanga imeanza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mlandege katika mchezo wa kundi B, uliopigwa uwanja wa Amaan Zanzibar.
Ushindi wa Yanga umepunguza kasi ya Mlandege ambayo ndiyo vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi zao sita, na Yanga wanapanda hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi tatu mabao mawili ya kufunga.
Kiungo mshambuliaji Juma Mahadhi ndiyo amefunga mabao yote mawili katika dakika za 6 na 36, na kurekebisha makosa yake ambayo amekuwa akiyafanya hata kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza.
Mlandege ndiyo waliouanza kwa kasi mchezo huo na kufanya mashambulizi makali kwenye lango la Yanga na lakini mabeki wa Yanga walisimama imara na kuondosha hatari hizo langoni mwao.
Yanga ilijikuta ikipata pigo sekunde ya 53, tangu kuanza kwa mchezo baada ya beki wa Yanga na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kugongwa kichwani na mshambuliaji wa Mlandege na kupoteza fahamu jambo lilisababisha benchi la timu hiyo kufanya mabadiliko yasiyo ya lazima kwa kumuingiza Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Mchezo huo uliendelea kwa Mlandege kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Yanga, lakini mipira yao mingi ilikuwa ikiishia kwenye miguu ya mabeki wa Yanga ambao walikuwa makini wakimlinda kipa wa Ramadhani Kabwili.
Yanga ilizinduka baada ya kuusoma mchezo huo na kufanikiwa kuandika bao lake la kwanza dakika ya 6, mfungaji akiwa Mahadhi aliyemalizia mpira wa kichwa uliopigwa na Pius Buswita kufuatia krosi nzuri ya beki wa kulia Ramadhani Kessy..
Bao hilo lilionekana kuwazindua Mlande na kuongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Yanga lakini washambuliaji wake Khamis Abuu na Ally Mkenya walishindwa kuzitumia vilivyo nafasi walizopata.
Mahadhi aliiandikia Yanga bao la pili dakika ya 36, safari hii akipokea pasi ya Papy Shishimbi aliyeunganisha krosi ya Haji Mwinyi ambaye katika mchezo huo alionekana amepoa kuliko ilivyokuwa kawaida yake.
Pamoja na jitihada za timu ya Mlandege kupambana kutaka kusawazisha mabao hayo zilionekana kushindikana na kufanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa nyuma mwa mabao hayo mawili.
Kipindi cha pili Mlandege walikianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kufuatia machozi dakika ya 47 mgfungaji akiwa Omary Makame aliyepokea pasi nzuri ya Mohamed Abdallah.
Bao hilo liliiongezea kasi Mlandege na kuendelea kupiga presha kwenye lango la Yanga lakini ulinzi ulikuwa makini na jitihada za washambuliaji hao kuonekana kupotea
Yanga ilizinduka tena na kuanza kufanya mashambulizi kwenye lango la Mlandege ambapo katika dakika ya 65 Buswita alipoteza nafasi nzuri baada ya kupenyezewa pasi nzuri na Rafael Daud.
Dakika ya 70 kiungo Papy Kabamba Tshishimbi alipoteza nafasi ya wazi baada ya shuti alilopiga akiwa ndani ya eneo la hatari kudakwa na kipa wa Mlandege Masoud Kombo.
Katika dakika ya 86 wachezaji Endrew Vicent wa Yanga na Omary Makame wa Mlandege walitolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia kutaka kupigana wanjani na baada ya tukio hilo mchezo uliendelea kwa timu zote kushambuliana.
Yanga ilifanya mabadiliko matatu kwa pamoja ambapo iliwatoa Daud, Tshishimbi na Mahadhi na nafasi zao kuchukuliwa na Emmanuel MartinSaid Bakari na Yohana Nkomola ambao kiasi fulani waliongeza presha kwa wapinzani wao Mlandege.
Hadi dakika 90 za mpambano huo zinakamilika Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mlandege

1919 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!