Kikosi cha Yanga
Kikosi cha Yanga
Kikosi cha Majimaji

 

Kikosi cha Yanga leo kinatarajia kusafiri kuelekea Mkoani Songea kucheza na Majimaji katika mechi yao ya kesho Jumapili ya 16 Bora ya Kombe la FA.

Yanga inakwenda Songea ikiwa ni siku moja tu tangu iliporejea kutoka Victoria, Shelisheli ambako ilikwenda kucheza na St Louis mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako walitoka sare ya bao 1-1.

Hata hivyo, Yanga imesonga mbele katika michuano hiyo ya Afrika kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1, kwani katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam ilishinda bao 1-0.

Yanga ilitinga hatua ya 16 bora ya Kombe la FA baada ya kuiondoa Ihefu FC ya Mbeya kwa penalti 4-3 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema: “Tunaondoka kesho (leo) saa 4:00 asubuhi kwenda Songea na ndege ya Air Tanzania (Bombardier) baada ya mazoezi.

“Lengo la kusafiri na ndege ni kuhofia wachezaji wetu kupata uchovu wa safari kwani Songea ni mbali na kama tukitumia basi wachezaji watachoka na kushindwa kucheza kwa ufanisi.

“Ratiba inatubana kiukweli, angalia jana (juzi) timu ilirejea saa nne usiku ikitokea Shelisheli na leo (jana) tulifanya asubuhi mazoezi mepesi kwa muda mfupi kwa hofu ya kuwachosha wachezaji wetu.

“Baada ya mazoezi tunawapumzisha wakijitayarisha kwa ajili ya safari ya kesho (leo) asubuhi tutakaposafiri saa nne asubuhi, utaona ni jinsi gani ratiba inavyotubana na kushindwa kufanya maandalizi ya kutosha.”

Saleh alisema majeruhi wa timu hiyo wanaendelea vizuri akiwemo Juma Mahadhi aliyeugua ghafla homa akiwa Shelisheli na yupo katika msafara utakaoenda Songea

“Wachezaji wengine kama (Donald) Ngoma, (Amissi) Tambwe, (Thabani) Kamusoko na (Obrey) Chirwa wenyewe bado wanaendelea na matibabu,” alisema Saleh.

 

By Jamhuri