Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewatoa hofu wapenzi wa michezo nchini kwa kusema kuwa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kuwa mwanachama wa Shirikisho la Mpira wa miguu barani Afrika hakuwezi kudhoofisha uhusiano mzuri uliopo kati ya TFF na ZFA.

Akizungumza na JAMHURI, Rais wa TFF, Jamal Malinzi, mara baada ya kurejea nchini akitokea Addis Ababa nchini Ethiopia, ambako alishiriki katika uchaguzi wa CAF, amesema kimsingi Watanzania hawapaswi kuwa na wasiwasi juu ya jambo hilo.

Malinzi amesema Watanzania wanachohitaji ni kuona maendeleo yanapatikana linapokuja suala la michezo, kwa hiyo maendeleo hayawezi kukwamishwa na vitu vidogodogo.

“Kila Mtanzania mpenda michezo hapa nchini, hana budi kuipongeza hatua hii iliyofikiwa na wenzetu wa ZFA, kwani itasaidia kuinua kiwango cha soka Visiwani na Tanzania kwa ujumla,” amesema Malinzi.

Amesema ZFA haikuanza leo kuomba kuwa miongoni mwa wanachama wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kama wengi wanavyodhani.

Malinzi amesema, TFF kwa kushirikiana na ZFA wanatarajia kuandaa mchakato wa kuhakikisha ZFA inakuwa mwanachama wa FIFA katika siku za usoni baada ya ZFA kupata uanachama wa CAF.

“Kwa misingi ya undugu tulio nao kati yetu na wenzetu wa Zanzibar, hatuwezi kuwa na wasiwasi kwa sababu ZFA wamekuwa wanachama wa CAF, badala yake itaongeza kuudumisha undugu wetu,” amesema Malinzi.

Mkutano Mkuu wa 39 wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, ulikubali na kupitisha  ombi la Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kuwa mwanachama  wake.

Kwa hatua hiyo, Zanzibar inakuwa nchi ya 55  mwanachama wa Shirikisho hilo wa kujitegemea, hali ambayo inaweza kuwa kichocheo kikubwa  cha kukuza mchezo wa soka na michezo mingine kisiwani humo.

“Umefika wakati wadau wa soka ni lazima wakubaliane na mapinduzi yanayotokea kila kukicha ndani ya mchezo huu, vinginevyo tutajikuta tunabaki nyuma,” amesema Malinzi.

Amesema, ipo mifano ya nchi nyingi ambazo zimeungana na nchi nyingine lakini ni wanachama wa Shirikisho la Soka la Duniani (FIFA). Mfano ni nchi zilizo chini ya Malkia wa Uingereza lakini zimeendelea kuwa imara.
%

914 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!