IMG_4376 copyKampuni ya Utalii ya Leopard Tours inayotajwa kuwa kubwa kuliko kampuni yoyote kwenye tasnia hiyo hapa nchini, inakabiliwa na tuhuma za ukwepaji kodi.

Pamoja na ukwepaji kodi kupitia mishahara ya waajiriwa, nyaraka zinaonesha kuwa Leopard Tour yenye makao yake jijini Arusha, imekuwa ikiwaachisha kazi wafanyakazi bila kufuata taratibu za kisheria.

Pigo la karibuni kabisa liliwakumba madereva 45 ambao ni sehemu ya madereva zaidi ya 280 walioajiriwa katika kampuni hiyo inayoendeshwa na Zuher Fazal.

Aidha, wafanyakazi wengine walifukuzwa kazi wiki iliyopita kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutoa siri za kampuni kwa Naibu Waziri, kwa waandishi wa habari na kwenye mitandao ya kijamii. Miongoni mwa waliofukuzwa ni wafanyakazi wa mapokezi.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Kazi na Vijana, Anthony Mavunde, katika ziara yake ya ghafla katika kampuni hiyo mapema mwezi huu, alipewa taarifa nyingi za upotoshaji.

Kati ya taarifa hizo ni zile zilizohusu mishahara ya watumishi ambako msemaji wa Leopard Tours, Joel Mmbaga, alimweleza Naibu Waziri Mavunde kwamba mishahara ya watumishi wa kampuni hiyo ni kati ya Sh 150,000 na Sh 300,000 kwa mwezi. 

Uchunguzi wa kina uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kuna tofauti kubwa kwenye mikataba ya ajira; na hati ya malipo kwa wafanyakazi wa Leopard Tours. Kilichoandikwa kwenye mikataba si kile kinacholipwa na kuoneshwa kwenye hati ya malipo ya wafanyakazi ya kila mwezi.

“Nadhani Fazal anadhani kuwa hii Serikali ni sawa na zile zilizopita, Leopard Tours imesema kuwa inawalipa mishahara wafanyakazi wake kati ya Sh 150,000 na Sh 300,000. Hii siyo kweli kabisa, tunaweza kuthibitisha hilo kwa sababu sisi guides tunalipwa kati ya dola 500 (Sh milioni 1.09) na dola 1,000 (Sh milioni 2.18) kwa mwezi,” amesema mmoja wa wafanyakazi wa Leopard Tours.

Chanzo cha habari kinasema ujanja huo unatumiwa na Leopard Tours kama njia ya kukwepa kodi na pia kuwapunja wafanyakazi kwenye michango yao inayopaswa kupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Kisheria, mtumishi anayelipwa chini ya Sh 170,000 kwa mwezi, kodi yake serikalini ni sifuri. Kwa maana hiyo, wafanyakazi wa Leopard Tours kwa kuonesha kuwa wanalipwa Sh 150,000 hii ina maana baada ya makato ya NSSF ya Sh 15,000 wanabakiwa na Sh 135,000.

Amekuwa akiwasainisha karatasi za Sh 150,000 na huku akiwalipa kati ya dola 500 na dola 1,000 za Marekani. Kisha hata hizo alizowasainisha alikuwa hapeleki NSSF. Ndiyo maana ukifuatilia wale madereva zaidi ya 40 aliowafukuza mwaka 2014 na ambao walikwishafanya kazi Leopard Tours kwa miaka 20 wengi walioenda NSSF walikuta kuna kati ya Sh 600,000 na Sh 1,000,000 tu.

“Tulipoenda NSSF tuliambiwa kuwa ‘jamani tajiri yenu ni mkorofi sana hakuna wa kushindana naye shukuruni Mungu hata kwa hicho kidogo mlichopata’. Haya ni maneno ya mtu wa Serikali. Anajua namna wakubwa wa Serikali walivyowekwa mfukoni,” kinasema chanzo chetu.

Wakati wa ziara yake, Mavunde aliambiwa Mhasibu Mkuu, Mmbaga analipwa Sh 500,000 lakini imebainika kuwa kama dereva analipwa dola kati ya 500 na dola 1,000; Mmbaga anacholipwa ni kikubwa zaidi. Kuna madai kwamba Mmbaga analipwa dola 4,000 za Marekani (zaidi ya Sh milioni 8) kwa mwezi.

“Tumefanya kazi zaidi ya miaka 10 Leopard Tours na hakuna asiyejua mshahara wa Mmbaga, maana wote mshahara tunauchukulia sehemu moja kwenye dirisha maalumu na unasaini, kwa hiyo tunajuana vizuri mishahara yetu. Huo ndiyo ukweli na si kama alivyomdanganya waziri kwamba analipwa Sh 500,000,” amesema mmoja wa wafanyakazi aliyeomba jina lake lihifadhiwe.

Ukweli kuhusu wanacholipwa madereva wa Leopard Tours umebainishwa kwenye kesi ambayo baadhi ya madereva walimfungulia Leopard Tours katika Idara ya Kazi- kesi ya Honesty Kessy na wenzake 2 dhidi ya Leopard Tours: CMA/ARS/ARB/44/2015; kesi ya Hashimu na Humud Magoma dhidi ya Leopard Tours -CMA/ARS/ARB/76/2015; na kesi nyingine na 78 ya mwaka 2015.

Katika kesi hizo, Mahakama iliitisha mikataba halisi ya kazi ya wafanyakazi wa Leopard Tours na ikabainika kuwa wanalipwa kuanzia dola 500 kwa mwezi.

Akitoa maelezo kwa Mavunde, Mmbaga alimweleza kuwa Leopard Tours haina Meneja Rasilimali Watu (HR); hali iliyomshitua Naibu Waziri huyo.

Hata hivyo, katika kesi ya Honesty Kessy na wenzake 2 dhidi ya Leopard Tours CMA/ARS/ARB/44/2015, kwenye kiapo Mmbaga alijitambulisha kuwa ndiye HR wa kampuni ya Leopard.

Aidha, kwenye barua ya Zitta Lumato, aneyadai mishahara yake tangu Desemba, 2014, Mmbaga amejitambulisha kama HR wa Leopard Tours. 

 

Wageni wanafichwa? 

Kuna taarifa kuwa siku ambayo Naibu Waziri alizuru Leopard Tours, baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, raia wa kigeni walifichwa kwa kuwa hawana vibali vya kufanya kazi nchini. Miongoni mwa watumishi hao ni mwanamke raia wa Malawi ambaye JAMHURI inalihifadhi jina lake kwa sasa.

Mwanamke mwingine raia wa Senegal, naye anatajwa kuwapo kwenye kampuni hiyo, akiwa anaishi na kufanya kazi zinazotajwa kuwa zingeweza kufanywa na Watanzania.

“Amepewa nyumba ya kuishi hapo hapo Leopard Tours ghorofani ambako anaishi na familia yake na watoto ambao kampuni ya Leopard Tours inawalipia shule ya St. Constantine, Arusha,” kimesema chanzo chetu.

Taarifa zilizopatikana wiki iliyopita zilisema mwanamke huyo ameonesha nia ya kuacha kazi.

“Kuna Meneja Karakana. Huyu ni Mshelisheli, amepangishiwa nyumba Njiro. Kuna walinzi wa karakana raia wa Nepal. Kazi yao ni kufungua geti tu na kufunga ila wanalipwa vizuri, wamepewa nyumba bure hapo hapo karakana. Hatuna hakika kama hawa watu wana vibali vya kufanya kazi nchini. Lakini unaweza kujiuliza, sheria gani inaweza kuruhusu mgeni aajiriwe kwa kazi za ulinzi wa karakana! Kwa namna mambo yalivyo sasa katika Serikali hii ya Awamu ya Tano, hawa walinzi wanaweza kutoroshwa,” kimesema chanzo chetu.

 

Kesi ya madereva 45

Madereva 42 wa Leopard Tours waliachishwa kazi mwaka jana, tuhuma kuu dhidi yao ikiwa kwamba waliwasilisha ofisini stakabadhi zilizoghushiwa kuonesha waliwapeleka watalii katika eneo la Olduvai Gorge.

Kwa upande wao, madereva waliozungumza na JAMHURI wanakanusha vikali madai hayo wakisema waliwapeleka watalii sehemu hiyo, na hakuna malalamiko kutoka kwao kuwa hawakufikishwa huko.

“Ofisini walisema hatuwapeleki watalii Olduval Gorge na badala yake tunaghushi stakabadhi. Hili ni jambo la kushangaza kwa sababu kabla ya kuanza safari sisi na wageni hupewa ratiba ya safari na vituo vyote. 

“Kama humpeleki mgeni sehemu iliyoandikwa kwenye ratiba ataandika malalamiko ofisini. Waulizeni wapi kuna hayo malalamiko? Hayapo,” anasema mmoja wa madereva waliofukuzwa.

Dereva huyo anaungwa mkono na wenzake (majina tunayahifadhi kwa sasa) wanaosema uamuzi wa Leopard Tours kuwafukuza ulitokana na kudorora kwa biashara ya utalii duniani, na kwa maana hiyo wakaona wapunguze idadi ya wafanyakazi.

“Hakuna stakabadhi za kughushi, walichofanya ni kupunguza wafanyakazi kutokana na kudorora kwa utalii. Wakaona watupunguze sisi lakini ili tusilipwe stahiki zetu, basi waseme tumeghushi stakabadhi,” kimesema chanzo chetu. 

Kwa sasa JAMHURI inahifadhi baadhi ya nyaraka zinazohusu madai hayo kwa kuwa suala hilo kwenye ngazi ya uamuzi ya vyombo vya sheria. 

 

Madereva waliotimuliwa kwa mbinu hiyo ni:

1: Anthony Milinga

2: Godwin Makundi

3: Jurgen John

4: Lawrence Mosha

5:  Micky Molobere

6: Mosses Anderson 

7: Noeli Elifuraha

8: Oswald Fabian

9: Ramadhan Kanyenga

10: Sabastian Edward

11: Saleh Rashid

12: Salum Said

13: Samson Kisamo 

14: Simon Matei

15: Wilbard Azaria

16: Yahaya Muruma

17: Ciryl P. Cyril

18: Emmanuel Urio

19: Gilbert Munisi

20: Joseph Sirikwa

21: Joseph Sarwat

22: James Ringo

23: John Boris

24: Munir Said

25: Mosses Charles 

26: Maxi Mbise

27: Nuru Mangula

28: Onesmo Peter

29: Peter Shampula

30: Rodrick Ndemfoo

31: Victor Mkulia

32: Vicent Fares

33: Tuhery Mawala

34: Charles Minja

35: Frank Mollel

36: Hashim Abdulrahman

37: Humud Magoma

38: Honesi Kessy

39: Didmus Joseph

40: Samuel Simon 

41: Silva Justine 

42: Saad Zuber

43: Iddi Abdul

44: Juma Sumbi

45: Joseph Ngwenya

 

Aidha, imebainika kuwa uongozi wa Leopard Tours ulimnyang’anya leseni yake ya udereva dereva Salva Justine pamoja na vyeti halisi vya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) tangu mwaka 2014. Hadi wiki iliyopita, Justine alikuwa hajarejeshewa vitu hivyo, hali iliyomfanya akose kuomba kazi sehemu nyingine. 

 

Naibu Waziri Mavunde anena

Mavunde amezungumza na JAMHURI kuhusu ziara yake katika Leopard Tours na sehemu nyingine mbalimbali mkoani Arusha.

“Lengo ni kuhakikisha tunatekeleza matakwa ya kisheria kwa kuhakikisha waajiri wote wanatekeleza sheria za kazi na za ajira kwa wageni.

“Nilipita maeneo tofauti – viwandani, ofisi za ujenzi, sehemu mbalimbali na nikamalizia Leopard Tours. Ilikuwa ziara ya kushitukiza, na kwa kweli niseme hatukupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wafanyakazi.

“Nilibaini mambo mengi, lakini kubwa ni tofauti kubwa sana ya kile wanacholipwa wafanyakazi mwisho wa mwezi na kinachoandikwa kwenye ‘payroll’. Nilibaini kuwa Serikali inapoteza mapato mengi sana. NSSF wanapata hasara.

“Nikaagiza TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wafanye ukaguzi wabaini kwa nini mishahara inayolipwa ni tofauti kabisa na iliyoandikwa kwenye mikataba,” amesema Mavunde.

Alipoambiwa na JAMHURI kwamba wapo wafanyakazi na waliowahi kufanya kazi Leopard Tours ambao wako tayari kuisaidia Serikali, Mavunde alisema: “Nawakaribisha kabisa. Naomba waziwasilishe moja kwa moja kwangu, au kwa kupitia utaratibu maalumu nitakaowapa.

“Naomba walete taarifa maana katika hali ya kawaida huwezi kukubali kuwa dereva amzidi mshahara mhasibu.”

Naibu Waziri akaongeza: “Sitaki kuwalaumu waandishi wa habari, lakini nadhani wanapaswa kuandika mambo makubwa yanayoibuka wakati za ziara hizi. Kuna mambo makubwa sana.”

 

Msemaji wa Leopard Tours azungumza 

Msemaji wa Leopard Tours, Mmbaga, alipotafutwa na JAMHURI mwishoni mwa wiki hakuwa tayari kuulizwa maswali.

“Kwa sasa tunavyoongea mimi niko barabarani, nilikuwa ofisini kweli tangu saa mbili, lakini sasa napiga mwendo naelekea Usa River. Niko mwendo kweli kweli,” alisema.

Alipoombwa apigiwe simu baadaye akishafika huko anakoenda, alijibu: “Hapana, ninachoenda kufanya huko siwezi kwenda na kula na watu kwenye vishughuli vidogo vidogo vya kifamilia, siyo muda mwafaka. Nitafute kesho asubuhi…sasa hivi nakimbia maana ndugu zangu wamenialika wanataka tukae pamoja, sasa nimechelewa.”

Kwa upande wake, mmiliki wa Leopard Tours, Fazal, alipotafutwa naye alikataa kuzungumza na mwandishi wa JAMHURI.

Alisema: “Leo Jumapili, naomba nipumzike tafadhali. Kwa saa moja nimepata masimu ya waandishi wa habari mpaka nimechoka sasa hivi, naomba tafadhali. Mmbaga ndiye msemaji, na leo ni Jumapili sote hatupo kazini. Mmbaga ndiye mzungumzaji wa kampuni, siyo mimi. Naomba Mmbaga azungumze tafadhali.”

6590 Total Views 2 Views Today
||||| 3 I Like It! |||||
Sambaza!