Nianze kwa kumpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk. Maulid Madeni, kwa kusaidia umma kutambua ukweli wa kile nilichokiandika kwenye safu hii toleo lililopita.

Dk. Madeni amezuru maeneo mbalimbali ya jiji hilo na kubaini wafanyabiashara zaidi ya 500 walioamua kuwatumia wamachinga kuuza bidhaa zao, huku [wafanyabiashara] wakidai wamefunga biashara kwa kukosa wanunuzi.

Kwa maelezo yake, amebaini udanganyifu mkubwa kwa wafanyabiashara ambao huwapa wamachinga bidhaa wawauzie,  kisha jioni hukusanya hesabu. Wafanyabiashara 500 wamefunga maduka wakidai kuwa hali ya biashara ni mbaya. Hawa ni tone tu kati ya wafanyabiashara zaidi ya 5,000 katika jiji hilo.

Nampongeza kwa dhati kabisa Dk. Madeni. Uamuzi aliouchukua unapaswa kuigwa pia katika majiji na miji yote nchini. Hii ndiyo aina ya uongozi inayotakiwa. Kulialia tu kama anavyofanya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kwamba imekuwa kazi ngumu kukusanya fedha kutoka kwa wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi, si suluhu ya matatizo.

Wafanyabiashara wamebuni utaratibu wa kuwatumia wamachinga kukwepa kodi. Hili halina ubishi. Fikiria, kama Arusha pekee wafanyabiashara zaidi ya 500 wamebainika kukwepa kodi kwa njia hiyo, ni fedha kiasi gani zinazopotea kwa miji, majiji, mikoa na taifa zima?

Njia pekee ya kudhibiti haya mambo ni kama nilivyoshauri; na anavyofanya Dk. Madeni. Ni kuhakikisha wamachinga wanatengewa maeneo ya biashara ili iwe rahisi kuwatambua. Wale wa kutembeza njiti za meno na soksi mitaani si tatizo kubwa kwenye uchumi. Tatizo ni hawa wanaouza vitu vya mamilioni huku wakikwepa kutumia EFDs kwa kigezo kwamba ni wamachinga.

Pili,  kuwatengea maeneo kutasaidia kuiweka miji yetu kwenye mpangilio wa kistaarabu. Leo Arusha ni kama uwanja wa fisi! Hata watalii hawaoni raha tena kupita kwenye mitaa na barabara za Arusha. Ni kero. Sidhani agizo la Rais John Magufuli lililenga kuvuruga mpangilio wa miji na majiji.

Naamini lililenga kuwapa nafuu wamachinga ili wajipatie vipato kwa njia nzuri. Agizo lake linapaswa litafsiriwe vizuri ili kuendelea kulinda na kutunza mandhari ya miji yetu. Hizi barabara nzuri zinazojengwa kila uchao zitakuwa hazina maana endapo zitaendelea kuvamiwa na wachuuzi na kuziba kabisa njia za waenda kwa miguu na watumiaji wengine.

Kama nilivyosema awali, nia ya Rais Magufuli kuhusu wamachinga ni njema, lakini endapo utaratibu hautawekwa mapato ya nchi yataendelea kushuka. Maendeleo ya nchi yanaletwa na kodi. Nani atalipa kodi kama wenye kustahili kutumia EFDs wote wengi wao wameamua kuwatumia wamachinga? Ashakum si matusi, mfanyabiashara gani mjinga atakubali kuwa na EFD wakati anaona kuna fursa ya kutoitumia kwa kujigeuza kuwa mmachinga?

Migahawa na hoteli ni maeneo mengine yanayoingiza fedha kwenye halmashauri, taasisi za umma na serikali. Kuna kodi za pango, kodi za OSHA, Zimamoto, usafi, afya, kodi za mapato, NSSF na nyingine nyingi.

Bahati mbaya mambo sasa yanafanywa kiholela mno. Kina mama wanapika vyakula nyumbani. Wanajaza kwenye ndoo na kwenda kuviuza mijini kwenye watu wengi. Wanapanga ndoo za vyakula hadi mbele ya migahawa na hoteli. Kwa kuwa wao hawalipi kodi yoyote, chakula wanachouza Sh 1,500 au 2,000; kwa hotelini kinauzwa Sh 4,000 au wakati mwingine Sh 5,000.

Kwa sababu hawa kina mama ntilie hawabanwi kwa kodi zozote, chakula wanachokiandaa hukikoleza kwa vikolombwezo vingi. Utakuta dagaa, maharage, nyanya chungu, bamia kidogo, mchuzi wa nazi, nyama iliyookwa na kadhalika.

Kwa kufanya hivyo, mtu anayehitaji chakula hawezi kuingia hotelini kulipa Sh 4,000 au 5,000 na kuacha chakula kitamu zaidi ya hicho kinachouzwa kwa Sh 1,500 au Sh 2,000.

Kwa haraka haraka tunaweza kushangilia kuwa kina mama na baba ntilie hawa wanasaidiwa kujipatia riziki ili wayamudu maisha yao. Hilo ni kweli. Lakini kwa upande wa pili hali hii si ya kushangiliwa, kwa sababu wenye hoteli ambao ndio wenye EFDs na walipa kodi, biashara zinakufa. Matokeo yake wengi wanafunga na kuajiri kina mama ntilie. Athari zake ndizo hizi za ukosefu wa mapato kutoka kwenye migahawa na hoteli.

Kusema hivyo simaanishi kuwa hawa mama na baba ntilie wapigwe marufuku, la hasha! Hilo haliwezekani asilani. Ninachopendekeza ni kuwa kundi hili kwa sababu lina wateja wengi, litengewe maeneo maalumu kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake. Wakishakuwa na eneo, walipe kodi kulingana na biashara zao. Potelea mbali hata kama watalipa Sh 200 kwa siku. Muhimu hapa ni kuweka utaratibu wa kila Mtanzania ajione ana haki na wajibu wa kulipa kodi. Tuone ni kwa namna gani tunapunguza huu u-bure bure wa kila huduma kwa Watanzania. Unatulemaza.

Jambo la kuangalia ni kuzuia aina zote za manyanyaso au uonevu wa watendaji wa serikali.

Kuwaweka sehemu maalumu ndugu zetu hawa, mbali ya kusaidia kuchangia mapato ya halmashauri, kutasaidia kulinda afya za wateja na wasio wateja. Wataalamu wa afya watahakiki afya zao. Kutakuwa na vyoo. Ilivyo sasa kila anayetaka kuuza chakula au kinywaji, anauza hata kama anaumwa TB. Hii ni hatari.

Wasomaji wetu wamenipigia simu na wengine wameniletea ujumbe mfupi wa maandishi wakiunga mkono mwito nilioupeleka kwa Rais Magufuli kuhusu miji yetu. Wameniomba nisichoke kulisemea jambo hili kwa sababu ni la kiungwana na linalenga kuifanya miji yetu iwe katika hali inayovutia.

Kama nilivyoshauri wiki iliyopita, kuruhusu biashara na uchuuzi viendeshwe kwa mfumo huria, usio na udhibiti wowote ni hatari kwa mustakabali wa usalama wa jamii yetu. Mtu akiachwa afanye anachotaka mahali fulani kwa muda mrefu, siku ya kumwondoa kutakuwa na mapambano. Atapinga kuondolewa, maana ataamini anaonewa.

Leo hii hawa ndugu zetu walioachwa wauze vyakula na bidhaa nyingine popote wanapotaka, siku ya kuwaondoa itakuwa ‘vita’, na kwa kuwa hakuna vita isiyokuwa na madhara, watu wataumizwa, mali zitaharibiwa na chuki ya wananchi kwa dola itaibuka.

Leo kuna lawama anazobeba Rais Magufuli kwa sababu wapo waliozilea. Anapochukiwa na watu waliolihujumu taifa hiyo haina maana yeye ndiye aliyewalea. Wapo waliowafikisha hapo. Anapambana na mfumo uliolelewa na baadhi ya watangulizi wake. Lawama za baadhi ya watu walioathiriwa na upanuzi wa barabara ya Ubungo – Kibaha zipo kwa sababu watu walipovamia na kujenga kwenye hifadhi ya barabara waliachwa. Hao waliowaacha walifanya hivyo ama kwa uzembe, au kwa huruma na kutaka wapendwe. Matokeo yake yule anayewarejesha kwenye utaratibu anaonekana mbaya. Huko ni kumwonea.

Vivyo hivyo, endapo leo naye ataruhusu wamachinga watamalaki kila mahali kwa sababu ama za kisiasa, au huruma ya kibindamu, atakayekuja baada yake atakuwa na wakati mgumu kurekebisha hali hiyo. Zitatumika nguvu na fedha kufanya kazi ambayo wala isingehitaji gharama zote hizo. Kwa kulitafakari hilo ndiyo maana tunashauri uwepo mfumo endelevu wa namna ya kuweka mambo kama taifa la watu wanaokusudia kuishi kistaarabu.

Mara zote Rais Magufuli amependa kushauriwa; na ni kwa kutumia busara hiyo tupo tulioona ni vizuri tukamshauri kwa haya tunayoona yanaweza kuwa na athari huko tuendako. Tunayasema haya ili kuona nchi inaongeza mapato kupitia kwa wafanyabiashara ‘walioasi’ na kuamua kujiita wamachinga kwa lengo la kukwepa kodi. Lakini pia utitiri huu wa umachinga usiwe unasababishwa na ubabe wa TRA kwenye makadirio ya kodi. TRA wanapaswa pia kuwa waungwana.

Pia kutenga maeneo kwa wamachinga kutasaidia kuweka mfumo mzuri wa mipango miji inayovutia wageni na wenyeji. Mwisho, nampongeza kwa dhati Dk. Madeni kwa kuikoleza hoja yangu kwa vitendo. Sote tuna wajibu wa msingi wa kushiriki kulijenga taifa letu kwa vitendo badala ya kulalamika tu.

1983 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!