Wiki iliyopita Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) walitangaza kuruhusiwa kutoka hospitalini mtu wa mwisho aliyekuwa ameambukizwa Ebola, ugonjwa hatari ambao umeua maelfu ya watu barani Afrika. 





Mgonjwa wa mwisho kuugua Ebola akitoka wodini katika mji wa Beni wiki iliyopita.

Hiyo ni moja ya dalili za kuonyesha kuwa ugonjwa huo, ambao umedumu kwa miezi 17, sasa umedhibitiwa. Lakini wataalamu watalazimika kusubiri kwa siku kadhaa ili kujiridhisha kuwa ugonjwa huo umeondoka kabisa.

Mwandishi wa kujitegemea, Emmanuel Freudenthal, aliishi katika mji wa Beni, ambao upo katika kitovu cha eneo lililokuwa limeathirika sana. Katika kipindi alipoishi hapo, amebaini kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola umewalazimisha watu kubadili mfumo wao wa maisha.

Mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya Ebola hayakuja bila ya kuwa na vikwazo. Mathalani, mara kadhaa kumekuwa na mivutano ambayo wakati mwingine ilihatarisha kuibuka kwa mapigano kati ya watoa huduma za afya na jamii za watu walioathirika kwa ugonjwa huo.

Mwezi uliopita mathalani, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka – Médecins Sans Frontières – liliwaondoa kwa muda wataalamu wake katika maeneo yaliyoathirika kutokana na misuguano na wenyeji.

Freudenthal amerekodi vituko kama hivyo na vingine vingi kuhusiana na Ebola. Mwandishi huyo aliingia Beni Julai mwaka jana katika kipindi ambacho hali ya ugonjwa huo ilikuwa mbaya sana. Lengo lake kubwa lilikuwa ni kuona ni kwa nini wenyeji wamekosa kuwaamini wataalamu wa afya walioletwa kuwasaidia kupambana na ugonjwa huo.

Anasema lengo lake lilikuwa ni kuona hali ilivyo kwenye maeneo yaliyoathirika, si kufahamu hivyo kupitia simulizi za wananchi ambao walikuwa wameathirika kwa ugonjwa huo.

Simulizi ya mwandishi

Asubuhi, muuguzi ananichoma sindano ya kinga ya Ebola ya majaribio. Inauma sana. Ni baada ya kuchomwa sindano hiyo ndipo daktari ananieleza mimi na wengine wakiwamo wataalamu wa afya na baadhi ya wanajamii kuwa tumepatiwa chanjo ya Ebola, na kuwa tunaweza kuona madhara kidogo.

Na kweli naanza kuona madhara ya sindano hiyo. Nashinda siku nzima nikiwa kitandani kwa maumivu ya mwili na asubuhi ya siku iliyofuata ninalazimika kuendelea kupumzika. Lakini baadhi yetu wana bahati, kwani hawasumbuliwi na maumivu hayo.

Chanjo iliyotengenezwa na Kampuni ya Merck niliyokuwa nimepatiwa ilikuwa bado kwenye majaribio, ni moja kati ya chanjo mbili zinazojaribiwa nchini DRC. Moja kati ya masharti kabla mtu hajapatiwa chanjo ni kupewa taarifa zote kuhusiana na chanjo na yeye kukubali kwa hiari kupatiwa chanjo hiyo. Huu ni utaratibu ambao Shirika la Afya Dunaini (WHO) limeutoa.

Malumalu, mwalimu wa saikolojia ambaye aliwekwa kwenye karantini kwa siku tano wakati alikuwa hajaambukizwa Ebola.

Taarifa hizo zinapaswa kuhusisha ufafanuzi wa madhara ya kinga hiyo na baadaye wahusika wapewe fursa ya kuuliza maswali na wakishakubali ndipo wapatiwe chanjo hiyo.

Lakini kabla ya kupatiwa chanjo hiyo sikupewa maelezo yoyote kuhusiana na madhara yake au taarifa nyingine.

Nilipofika kwenye kituo cha chanjo, niliulizwa jina langu, ambalo linapitiwa na watu kadhaa. Mwishoni, ninaambiwa nisaini fomu ya kukubali, ambayo ninaambiwa nitaisoma baadaye, kama nikipata muda.

Hata kujaza fomu lilikuwa ni zoezi gumu. Inabidi nirejee utaalamu niliokuwa nao wakati ninasoma darasa la awali kukamilisha ujazaji wa fomu. Wakati fulani mtu anayenisimamia kujaza ananiambia kuwa herufi zangu hazisomeki vizuri. Ninapomaliza kuandika ‘M’ mbili za jina langu, msimamizi ananiambia niondoe herufi ya mwisho kwenye jina.

Baada ya kukamilisha jina langu linasomeka: EMMANUEL FREUDENTHA. Hakukuwa na nafasi kwenye fomu kwa ajili ya herufi ya kwisho ya jina langu!  Baadaye ninapigwa picha ambayo inabandikwa kwenye fomu kwa kutumia pini.

Ninashangaa ni Wakongo wangapi ambao wamepatiwa chanjo hii? Wanajisikiaje baada ya kutendewa hivi? Kwanza, wamelazimika kubadili utaratibu wao wa maisha ya kila siku baada ya mlipuko wa Ebola. Sasa, juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo nazo zinawaletea utaratibu mpya wa maisha ambao hawajauzoea.

Hata hivyo, ninashukuru kuwa nimepatiwa chanjo hii, ambayo, kwa mujibu wa taarifa zilizopo, inaanza kufanya kazi baada ya siku kumi.

Wakati nikisubiri siku hizo kumi, wakati ninapata staftahi hotelini kwangu, ninaanza kushangaa kuhusiana na usalama wa chakula ninachopatiwa. Ni watu wangapi wameigusa ndizi iliyomo kwenye mlo wangu? Vipi kuhusu mkate?

Sijui iwapo mpishi wa hoteli hajaambukizwa ebola na atafariki dunia. Sijui iwapo aliandaa chakula changu baada ya yeye kuambukizwa.

Niliamua kuwasiliana na WHO katika ofisi yao ya Geneva na kuomba wanipatie maelezo ya ufafanuzi kuhusiana na utaratibu mzima wa kumpatia mtu chanjo hiyo. Ofisa habari aliponipigia, nilimwambia kuwa watu wanapatiwa chanjo hiyo bila kukubali, wengi wameniambia hivyo. Ananijibu kuwa hao watakuwa hawajaelewa, kwani wakati mwingine raia wa DRC wanakuwa wagumu kuelewa maelekezo wanayopewa.

Ninamwambia kuwa hata mimi nilipatiwa chanjo hiyo bila kufuata utaratibu ambao wameuweka.

Kwa upande mwingine, mwakilishi wa WHO ananiambia kuwa shirika hilo limetekeleza mengi ya matakwa ya jamii ya watu wa DRC. Kukubali kwa jamii husika kupatiwa chanjo hiyo kilikuwa kinatajwa kama kikwazo kikuu cha utoaji wa chanjo, ambayo inaaminika kuwa ilikuwa muhimu kukomesha janga la Ebola.

Ninataka kuona kwa nini jamii inapinga juhudi za kupambana na ugonjwa huu ambao unaua watu wengi. Hiyo inamaanisha ni lazima niongee na watu ambao wameathirika kwa ugonjwa huu. Najua hilo linaongeza uwezekano wa mimi kuambukizwa, pia kujikuta katikati ya vurugu baina ya pande hizi mbili, hasa watu wakiambiwa kuwa nami ni mmoja wa wataalamu wa kupambana na Ebola ambao wanawaona kama adui zao.

Siku chache baadaye ninaifuata timu ya wataalamu wa WHO mjini Beni wakati wakitoa awamu nyingine ya chanjo kwa wenyeji. Tupo katika msafara wa magari kadhaa, baadhi yakiwa na watu wawili tu ndani yake, akiwamo dereva. Tunapotea.

Baadaye tunafanikiwa kufika tunakokwenda, lakini si pale tulipokusudia kwenda. Ni kazi ngumu kutafuta eneo katika mji ambao hauna vibao vinavyoonyesha majina ya mtaa. Baada ya kuzunguka katika barabara ndogo kwa muda, tunafanikiwa kufika tulipopakusudia.

Mahema yanawekwa haraka haraka, bila kuzungumza na watu waliokuwa wamesimama pembeni wakiangalia.

Watu wachache kwenye timu yetu wanaanza kuzungumza kuhusu mgonjwa wa Ebola aliyefariki dunia katika eneo hilo na kulazimisha wao kuja kutoa chanjo hiyo ili kuwakinga watu ambao walikaribiana naye. Kila mtu aliyekuwa karibu aliweza kulisikia jina la mgonjwa, kazi yake na alikuwa anaishi wapi.

Siku chache kabla, katika siku yangu ya kwanza Beni, nilibaini jinsi Ebola inavyoharibu uhusiano wa watu. Siku hiyo nilikwenda kwenye makao makuu ya kampeni ya kupambana na Ebola. Nilipofika, kama kawaida, nikanyoosha mkono wangu ili kumsalimia Dk. Gaston Tshapenda, ambaye kila mtu alikuwa anamuita Dk. Gaston, akasita kuupokea mkono wangu. Lakini baadaye akanipa mkono tukasalimiana. Hapo ndipo nikabaini kwa mara ya kwanza kabisa kuwa hata utaratibu huu wa kawaida wa kusalimiana hautumiki tena katika maeno haya.

Katika maeneo ambayo yameshambuliwa na ugonjwa huu watu hawakupaswa kukaribiana na salamu zilikuwa si kwa kushikana mikono kama ilivyozoeleka, bali kwa ishara. Kuosha mikono kwa maji yaliyowekewa dawa ni jambo la kawaida kila mara unapoingia au kutoka katika jengo.

Dk. Gaston ni mcheshi sana, ambaye anazungumza Kifaransa akichanganya na Kiingereza, lugha ya pili aliyojifunza ambayo anamudu kuizungumza. Ananiandikia barua ya utambulisho kuonyesha kuwa nimepewa ruhusa ya kuripoti masuala ya Ebola. Lakini kuna makosa, barua hiyo ni kwa ajili ya mwandishi mwingine wa habari!

Barua kama hiyo inamruhusu mwandishi wa habari kufanya kazi Beni kwa muda wa siku tatu au nne. Waandishi wengi hawapendi kukaa muda mrefu katika maeneo haya yenye Ebola ingawa mtu mmoja ananiambia yeye atakaa hapa kwa siku tano.

Ninaambiwa kuwa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu pia husaidia kuandaa masuala ya itifaki kwa baadhi ya waandishi. Masuala hayo ni pamoja na usafiri wa anga, uhamisho na mahojiano.

Dk. Gaston anajitahidi kuangalia na hatimaye anaipata barua yangu. Anajaribu kuichapisha lakini wakati huu printa inaleta matatizo, ikionyesha kama kuishiwa wino. Kwa sababu hakuna mtaalamu wa masuala ya IT hapa, Dk. Gaston anaamua kuirekebisha printa yeye mwenyewe. Anatoa kifaa kinachotunza wino na kukitikisa. Lakini ungaunga wa rangi ya pinki unamwagika kutoka kwenye kifaa hicho na kusambaa katika shati lake. Anajifuta na kurudisha kifaa hicho kwenye printa. Baadaye anachapisha barua yangu na kunikabidhi.

Ninapoipokea barua hiyo moyoni mwangu ninawaza jinsi alivyojitolea kufanya kazi katika aneo ambalo miundombinu, kuanzia printa hadi barabara, ni mambo yasiyotabirika.

Mazishi

Wiki chache kabla sijafika DRC, gari lililokuwa limebeba wataalamu wa kupambana na Ebola lilichomwa moto. Abiria walifanikiwa kujiokoa kuchomwa moto na kundi la vijana. (Hadi mwishoni mwa Disemba mwaka jana, WHO ilisema kulikuwa na mashambulizi 390 dhidi ya vituo vya afya mwaka mzima.)

Nikiwa nimeambatana na msaidizi wangu, Yassin Kombi, ambaye ni mwandishi wa habari anayeishi maeneo haya, tukatembelea eneo la jirani ambako gari lilichomwa moto ili niweze kuzungumza na waendesha bodaboda.

Wananieleza kwa ukali kuwa Ebola si ugonjwa bali ni biashara. Hali ni tete kidogo lakini tunapoanza kuzungumza, wanaamua kunieleza na kufafanua kilichotokea.

Tunapanda kwenye bodaboda zao na wanatupeleka katika shule ya sekondari iliyoko jirani kuzungumza na wanafunzi waliokuwa wametawanywa kwa risasi zilizopigwa na polisi kama njia ya kuwazuia wasihudhurie mazishi ya mwenzao aliyefariki dunia kwa Ebola. Wanafunzi hao walikuwa wameomba jeneza lifunguliwe ili waweze kuuona mwili wa rafiki yao.

Siku iliyofuata ninaamua kuhudhuria mazishi ya mtu aliyefariki dunia kwa Ebola. Ninakwenda huko nikiwa nimeambatana na maofisa wa Wizara ya Afya wanaoshughulikia mazishi ya watu wanaofariki dunia kwa Ebola na ninazungumza nao tukiwa njiani.

Wananiambia kuwa kazi yao ni ya hatari sana. Mmoja ananisimulia jinsi alivyolazimika kuhama sehemu aliyokuwa anakaa baada ya jirani zake kubaini kazi aliyokuwa anaifanya. Anasema kila usiku watu walikuwa wakirusha mawe nyumbani kwake na watoto wake wanaanza kuishi kwa wasiwasi. Amehamia mbali, na watoto wake sasa wanalazimika kutembea kilometa saba kwenda shuleni.

Anasema: “Jirani zetu wanaamini kuwa tunakula mikate iliyochovywa kwenye damu ya waliokufa kwa Ebola. Wanaamini kuwa sisi ni sehemu ya mpango mzima wa kutumia Ebola kufanya biashara na tunafanya mipango wenzetu wafe. Hiyo ndiyo hatari inayotukabili.”

Zamani alikuwa mwalimu na ninapomuuliza kwa nini asirudie kazi yake yenye usalama, anajibu: “Hapana. Hapana. Hapana! Ni kazi isiyo na kipato. Lakini ugonjwa bado upo, tunawezaje kuacha kupambana nao?”

Kwa kazi hii analipwa kama dola 300 za Marekani kwa mwezi lakini anatarajia kulipwa dola 450 za Marekani kama bonasi kutoka kwa WHO.

Mbele ya gari letu kuna gari jingine ambalo limebeba jeneza likiwa limefungwa msalaba. Nyuma yetu, katika gari jingine dogo, kuna ndugu na jamaa wa marehemu. Wanakwenda kumzika mtoto wa mwaka mmoja.

Tunapokaribia makaburi, timu ya wazikaji inazidi kupata wasiwasi. Tunapofika, wanashuka kwenye gari na kuzika haraka haraka. Mazishi yenye heshima ni jambo ambalo limesahauliwa katika maeneo haya kutokana na uhasama uliopo.

Baba wa mtoto analia. Ninaomba ruhusa ya kumpiga picha na anasema hajali. Ananiangalia, kisha anaangalia nyuma yangu. Mwanamke mzee amejilaza ardhini, analia. Wasichana wawili nao wmejikunyata ardhini karibu nao wanalia, wakiomba Mungu.

Wazikaji wanapomaliza kufukia kaburi, wazazi wanapanda miti juu ya kaburi na msalaba nao unawekwa.

Pembeni, mtu mmoja anawakaripia wazikaji: “Mbwa nyie.”

Dakika 15 baada ya kuanza, mazishi yanakuwa yamekamilika. Ninampa baba wa marehemu kadi yangu ya anwani iwapo angependa kuwasiliana nami baadaye ili kupata picha nilizopiga.

“Niifantie nini hii?” anauliza huku akiusukuma mkono wangu.

Tunarudi kwenye magari haraka haraka na mtu mwingine anafoka tena: “Mbwa nyie.”

Maisha yabadilika

Siku chache zilizofuata ninajaribu kuangalia maisha ya mtu ambaye ameambukizwa Ebola. Nataka kujua jinsi wanavyoshughulikiwa kuanzia wanapofika hospitalini, matibabu hadi wanapoma.

Ninatembelea kituo kilichowekwa na Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) ambacho kinaendeshwa na Wizara ya Afya. Ninawatafuta wagonjwa ambao wamewekwa kwenye karantini lakini ninaishia kukutana na mwalimu wa saikolojia, Malumalu, ambaye aliwekwa kwenye karantini kwa siku tano lakini hatimaye akabainika kuwa hajaambukizwa.

Nilipofika kituoni nilishuhudia mgonjwa akiwa amebebwa kwenye pikipiki. Kwa kuwa hakukuwa na nafasi ndani, analazimika kulala chini nje ya kituo.

Baada ya muda gari lenye wataalamu wa afya linafika na wanapotaka kwenda kumpima wanagundua kuwa hawana baadhi ya vifaa vya kujikinga. Wanaamua kuwasubiri wenzao.

Wanapofika, gari linasogea karibu na mwanamke huyo lakini mlango wa nyuma wa gari unagoma kufunguka.

Mlango unapofunguka, wafanyakazi wawili wanambeba na kumpandisha kwenye gari la tatu na kumpeleka kwenye kambi nyingine ili akafanyiwe vipimo.

Baadaye ninafahamishwa kuwa aliachiwa baada ya siku tatu kwa sababu hakuwa na Ebola.

Ninapozungumza na wafanyakazi wanaopigana na ugonjwa huu wananieleza kuwa kazi yao imetawaliwa na vurugu kutoka kwa wenyeji. Kunakuwa na vurugu kuanzia kwenye kuwaweka watu kwenye katantini mpaka kwenye maeneo ya makaburi ambako mazishi hufanyika.

Wananiambia kuwa kuna wenzao ambao wameshawahi kuuawa katika vurugu hizo.

Siku nyingine ninamtembelea mganga wa kienyeji anayeishi nje ya mji. Anajigamba kuhusu idadi kubwa ya watu walioambukizwa Ebola ambao ameshawatibu na kupona. Anasema wakati fulani wafanyakazi wa afya walikuja ili kuwachukua wagonjwa wa Ebola aliokuwa anawatibu, wakakimbia.

Ninapozungumza naye, mawazo yangu yanazunguka nikihisi kuwa kuna uwezekano mmoja wa wagonjwa wake alikuwa amekaa kwenye kochi ambalo na mimi nimelikalia hivi sasa. Kwa muda wa siku 21 nilizokuwa hapo, kila mara nilikuwa na wasiwasi wa kugusa vitu kwa sababu sikuwa na uhakika ni wapi wadudu wa Ebola wanaweza kuwa wameachwa. Ukweli ni kuwa Ebola ilikuwa ni tishio kubwa, ingawa wakati mwingine unaweza usilione kwa macho.

Emmanuel Freudenthal ni mwandishi wa habari wa kujitegemea anayeishi Nairobi, Kenya.

By Jamhuri