Tutarajie maskini wengi kumfuata Rais Magufuli

Kitendo cha mama mjane ‘kuvamia’ mkutano na kuwasilisha kilio chake kwa Rais John Magufuli, kinapaswa kuwafumbua macho viongozi na watumishi katika mamlaka za utoaji haki nchini.

Si wajibu wetu kuhukumu kutokana na yale yaliyozungumzwa na mjane huyo, lakini itoshe tu kusema mamlaka za utoaji haki nchini zinapaswa kujitazama upya ili kuwatendea haki wananchi.

Tunayasema haya, si kwa tukio hilo pekee, bali ni kutokana na ukweli kwamba kwa kazi yetu ya habari, tumekuwa tukipokea malalamiko mengi mno ya wananchi wakilalamikia uonevu na kutotendewa haki katika ngazi mbalimbali.

Hapa tunaomba tuwe wazi kwa kusema kuwa sehemu zinazolalamikiwa zaidi ni Polisi, Mahakama, ofisi ya DPP na sasa kwa baadhi ya mawakili. Kesi nyingi zimekuwa zikivurugwa katika ngazi ya ushahidi ambako baadhi ya polisi wasio waaminifu wameshiriki kuvuruga ushahidi na hivyo kusababisha wananchi wanyonge wapoteze haki zao.

Katika Mahakama, pia maskini wamepoteza haki zao kwa sababu ya kitu kinachoitwa ‘technicalities’. Hapa ni pale ambako mtu hupoteza kesi kwa mambo kadhaa, likiwamo la kifungu fulani cha sheria kunukuliwa kwenye shitaka lisilohusika. Bunge linapaswa kutazama namna ya kurekebisha jambo hili ili wananchi wapate haki zao.

Wapo mawakili wanaolalamikiwa kwa kushirikiana na upande wa pili katika kesi wanazosimamia. Hayo huyafanya kwa kuacha ‘nyufa’ fulani fulani ambazo baadaye huudokeza upande wa pili wazitumie na matokeo huwa mteja wake kupoteza kesi. Haya matukio yapo mengi.

Yule mjane aliyemfuata Rais Magufuli, alifanya hivyo kwa ujasiri wake. Wapo watu wengi wenye malalamiko ya aina hiyo, lakini hawana namna ya kumfikia.

Endapo vyombo vya utoaji haki havitabadilika na kuanza kutenda haki, tutarajie kuona watu wengi zaidi wakitumia staili ya yule mama mjane kuwasilisha vilio vyao kwa viongozi wakuu.

Wakati umefika kwa mamlaka zinazohusika kuwawajibisha watumishi na watendaji wanaofanya makusudi, au uzembe kuchelewesha au kupoteza haki za wananchi.

Hali ilivyo sasa, ni kama kumtendea haki mwananchi ni jambo la hisani. Kama watumishi na watendaji wa aina hiyo hawaogopi binadamu wenzao, basi ni vizuri wakamwogopa Mungu.

Watu wanaoonewa, wanaodhulumiwa na wanaoyumbishwa katika kupata haki zao ni wengi mno nchini mwetu. Hii si hali nzuri kwa ustawi wa nchi yetu.

1741 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons