Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jumla ya Sh milioni 600 zitaokolewa baada ya watoto 40 kufanyiwa kupasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Shirika la Muntada Aid la nchini Uingereza.

Gharama ya upasuaji kwa mtoto mmoja ni Sh milioni 15 ndani ya nchi ambapo nje ya nchi ni Sh milioni 30.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Richard Kisenge amesema upasuaji huo umeanza Aprili 20 ,2024 ambapo tayari watoto 24 wamekwisha fanyiwa upasuaji huku lengo likiwa ni kufikia watoto 40.

“Tangu tarehe 20 taasisi yetu ilipata wageni kutoka Uingereza walikuwa wanakuja wakati taasisi ilikuwa hali ya chini kwa upasuaji wa moyo hawa wametupa historia kubwa wamesaidia kufundisha madaktari wetu na watoto zaidi ya 500 wamefanyiwa upasuaji.

Dk Kisenge ameseme wataalamu hao ni muungano wa madaktari mbalimbali kutoka Canada, Uholanzi,Misri na Uingereza na wamependa kuja hapo kutokana na miundombinu iliyoboreshwa na serikali na rasilimali watu.

“Serikali hivi karibuni imetoa Sh bilioni tano kusomesha madaktari katika ubingwa bobezi hawa wakija wanataka kuona miundombinu mizuri na hawa pia wamekuja na vifaa vya gharama ya Sh bilioni 1.5 wamekuja navyo na wametuachia kuwasaidia wenzetu,”ameeleza.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Moyo kwa watoto Dk Sulende Kubhoja amesema katika kila watoto 1,000 wanaozaliwa wenye matatizo ya moyo ni watoto nane mpaka 10.

Meneja wa miradi wa Shirika la Muntada Aid,Kabir Miah amesema wanafanya kazi Afrika katika nchi mbalimbali na hasa sehemu ya afya ambapo mradi huo unaokoa maisha ya watoto wanaoteseka na magonjwa ya moyo

By Jamhuri