Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Kibaha

MEI 9 mwaka 2024 Tanzania imezindua kampeni ya awamu ya pili ya “Mtu ni Afya” baada ya ile ya kwanza kutamatika kwa mafanikio makubwa kutokana na baadhi ya magonjwa yaliyokuwa yakiwasumbua wananchi takribani miaka 50 iliyopita kudhibitiwa na mengine kutokomezwa.

Katika kampeni hiyo ambayo imezinduliwa rasmi na Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango,wilayani Kibaha mkoani Pwani inakusudiwa kumalizika mwaka 2030 ikiwa imelenga kupambana na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanadaiwa kusababisha aslimia 33 ya vifo vya wananchi.

Baadhi ya magonjwa yasiyo ambukiza ni pamoja na Saratani,shinikizo la damu (presha),Kisukari, Upofu,Pumu, Ulevi, magonjwa ya akili,Madonda ya tumbo,Majereha,Karisi ya meno na hata selimundu.

Hakika Serikali inastahili pongezi katika hilo,kwa sababu msingi mkuu wa maisha ya mwanadamu yoyote hapa duniani ni afya, haijalishi ni tajiri au maskini.

Kama tunavyofahamu taifa lolote linaloendelea linahitaji kuwa na watu wenye Afya,nguvu,akili, maarifa,heshima na lenye wasomi wenye fikra chanya, wachapakazi na wenye uzalendo wa kuipambania nchi yao.

Waziri wa afya,Ummy Mwalimu, akiwahamasisha wananchi kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyo ambukiza.

Rais wa 44 wa Marekani,Barack Obama, aliwahi kusema “Mabadiliko hayawezi kutokea kama utasubiri mtu mwingine au muda frani”.

Hali kadhalika,nukuu ya aliyewahi kuwa rais wa Afrika kusini,Nelson Mandela inasema “Matendo bila dira ni kupitisha muda tu,dira bila matendo ni ndoto za mchana, lakini dira pamoja na matendo vinaweza kubadili dunia”.

Pamoja na mambo mengine,makala hii imejikita kuzungumzia changamoto ya ugonjwa ya Kisukari na shinikizo la damu ambapo magonjwa hayo mawili yanatajwa kuwa miongoni mwa 10 yanayoongoza kwa kusababisha vifo vingi nchini.

Kwa vile Serikali yetu imeonyesha dira ya wapi tunapopaswa kuelekea katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo, kinachosalia ni utekelezaji kwa vitendo kuelekea 2030 lengo likiwa ni kupunguza au kuyatokomeza kabisa.

Licha ya kwamba magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaendelea kuua watu duniani pote,nchini kwetu bado kuna baadhi ya watu hawana kabisa uelewa wa magonjwa hayo ambayo baadhi yake yanatokana na mfumo wa maisha na mengine yakiwa ni ya kurithi.

Dkt. Faustin Kamugisha,aliwahi kusema Ukibadili unachokiona unabadili unachokizalisha, maana yake kubwa ni kwamba unapotaka kutoka sehemu fulani kwenda nyingine piga kwanza picha ya akilini kisha anza kuitekeleza picha hiyo katika uhalisia.

Hata katika kitabu kitakatifu cha Biblia Mithali 29:18 ” Pasipo maono watu kuangamia”. Kumbe ni muhimu kuwa na maono ya kuaminika,kuyapanga vyema kisha kuyatekeleza.

WANANCHI WANAJUA NINI KUHUSU MAGONJWA HAYO

Neema Paschal,mkazi wa Sofu Picha ya ndege anasema hajui ugonjwa wa kisukari husababishwa na nini licha ya kwamba anafahamu madhara yake.

“Ukweli sijui kisukari unasabishwa na nini,nachokijua ni kuwa huo ni ugonjwa ambao ukiupata hauponi haraka na husababisha kifo”anasema.

Magreth Mathias,mkazi wa magereza Kibaha anadai ugonjwa huo husababishwa na watu kutumia sukari na chumvi mbichi kwa wingi na kwamba hali hiyo huwakumba baadhi ya watu na wengine hulazimika kutembea na sindano za kujidunga.

“Miaka ya 1982 niliwahi kumshuhudia Babu yangu alikuwa na sindano ya kujidunga, hali hiyo ilikuwa ikimkuta sehemu yoyote hata akiwa mtaani akishaona dalili za mwili kukosa nguvu anachomoa haraka sindano yake anajichoma kwenye paja” anasema Magreth.

Aidha anaeleza kuwa hajawahi kwenda hospitali kupima ili kutambua iwapo ana ugonjwa huo au hapana kwa kuwa hajawahi kuhisi dalili katika mwili wake.

Makamu wa Rais Philip Mpango,akizungumza na wananchi wa Kibaha kwenye uzinduzi wa kampeni ya Mtu ni Afya awamu ya pili.

Seleman Mohamed,mkazi wa Maili moja ni miongoni mwa wagonjwa wa shinikizo la juu la damu(High blood pressure) ambapo anasema amefanikiwa kuishi na changamoto hiyo kwa zaidi ya miaka 15 huku akitumia dawa na kuzingatia masharti ya madaktari.

Anasema ugonjwa huo humsumbua sana mtu hasa anapokuwa amekwazika, na wakati mwingine akiwa kwenye msongo wa mawazo na kwamba ni vyema kupata muda mwingi wa utulivu wa nafsi.

“Presha ni ugonjwa hatari sana,kwanza unaweza kukuua wakati wowote na ni ugonjwa usiopenda uwaze vibaya kwa muda mrefu,na unapohisi hali yako haiko sawa ni vizuri kuwahi kwenye huduma za afya maana wale wamesomea namna ya kumsaidia mgonjwa badala ya kukaa tu nyumbani” anasema Mohamed.

Sospeter Kalembo,anasema awali kabla hajatambua kama anasumbuliwa na presha alitumia gharama kubwa kwenda kutibiwa kwa waganga wa Jadi akiamini analogwa na jirani zake kutokana na ushindani wa kibiashara.

Hata hivyo ukweli wa mambo ulijidhihirisha baada ya vipimo vya kitaalamu kubaini changamoto ya ugonjwa wa shinikizo la damu, ambapo alianza kuzingatia masharti ya madaktari kwa kupunguza kula vyakula vyenye wingi wa chumvi,sukari,vyakula vya wanga na kuanza kufanya mazoezi kila asubuhi na jioni.

“Namshukuru sana Mungu naendelea vizuri,awali kabla ya kufuata masharti ya madaktari hali yangu ilidhoofika sana kiasi cha kukata tamaa ya maisha,maana niliamini katika kulogwa kumbe ni ugonjwa kama magonjwa mengine” anasema Kalembo.

Kwa mantiki hiyo unaweza kukubaliana na msemo wa mwanafalsafa wa kifaransa na mshindi wa tuzo ya Nobel mwaka 1927 Henry Bergson, kwamba ” Jicho linaona kile ambacho akili iko tayari kuelewa”.

HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA CHATO

Kwa mujibu wa daktari bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya rufaa ya Kanda Chato, Dkt. Liberius Libent,angalau jamii imeanza kupata uelewa juu ya magonjwa yasiyoambukiza ukilinganisha na miaka ya nyuma.

“Zipo sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha kuonekana magonjwa hayo yanaongezeka kila kukicha duniani kote na kusababisha vifo,ukitazama hapa kwetu Tanzania kama zilivyo nchi nyingine wananchi wanaishi maisha ya kisasa zaidi tofauti na enzi za babu na bibi zetu.

Kumbuka zamani hapakuwa na vyombo vingi vya usafiri ukilinganisha na sasa,kwahiyo watu wa zamani muda wao mwingi waliutumia kutembea kwa miguu pasipo kujua kama wanadhibiti baadhi ya magonjwa hayo, vilevile walipendelea kula vyakula vya asili pasipo kuvikaanga kwa mafuta mengi” anasema Dkt. Libent.

Hata hivyo anasema katika uchunguzi wa afya kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya figo na moyo kwenye hospitali hiyo, inaonyesha takribani aslimia 98 ya watu hao walianza kuugua shinikizo la damu(presha) pamoja na kisukari.

Anaishauri jamii kujiepusha na ulaji zaidi wa vyakula vya wanga,Mafuta,sukari na chumvi na kwamba wajenge tabia ya kuchunguza afya zao mara kwa mara kabla na baada ya kuugua badala ya kukimbilia kwa waganga wa Jadi kwa imani za kishirikina.

“Tunaishauri sana jamii kuepuka ulaji usio na maana hasa vyakula vya viwandani, maana wanajihatarishia afya zao na kutumia fedha nyingi kwaajili ya kujitibia pia wanaigharimu pesa nyingi serikali kununua madawa na vifaa vya uchunguzi, hata hivyo tunaendelea kusisitiza sana katika mazoezi”.

“Ni vema watu watambue kuwa lishe bora huchangia kwa kiasi kikubwa kuzuia magonjwa yasiyoambukiza,watu watumie kwa wingi mboga za majani,matunda, ndizi za kupika na nafaka zenye jamii ya mizizi na mikunde”anasema Dkt. Libent.

DALILI ZA UGONJWA

Anataja dalili za Ugonjwa wa kisukari kuwa ni Kukojoa mara kwa mara, kusikia kiu kali,kuhisi njaa sana, kuchoka mwili,kupungua uzito pasipojitihada zozote za kupunguza hali hiyo,maambukizi kwenye njia ya mkono ambapo mtu hupata maumivu makali wakati akiokoa.

Huku dalili za Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ikiwa maumivu kifuani, mpapatiko wa moyo,kusikia kizunguzungu na kuhisi baridi kali mwilini.

Pia Dkt. Libent anataja madhara yatokanayo na Ugonjwa wa kisukari kuwa ni, kupoteza uwezo wa macho kuona(upofu), matatizo ya figo, maumivu makali kifuani, Kiharusi (kupooza),Vidonda, kuharibika Neva, kufa ganzi,kupata uhanithi kwa wanaume (kushindwa kudindisha),kuzimia au kupoteza fahamu,kuharisha pamoja na kifo.

Ambapo madhara ya shinikizo la damu (presha) ni kupooza mwili, kuchanganyikiwa, kupoteza uwezo wa macho kuona,kutembea kwa taabu, maumivu makali ya kichwa,kuzimia, mimba kuharibika kwa baadhi ya wajawazito pamoja na kifo.

Dkt. Libent, anaishauri serikali kuendelea kutenga fedha za kutosha ili kuwawezesha wataalamu na wadau wengine wa maendeleo kutoa elimu kwa jamii ili waweze kubadili mtindo wa maisha na kujiepusha na visababishi vyaagonjwa hayo ambayo bado ni tishio kwa jamii.

MPANGO MKAKATI WA AFYA

Waziri wa afya, Ummy Mwalimu,anasema mpango mkakati wa serikali ni kuhakikisha inadhibiti na kutokomeza magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa jamii ili kuwa na watu wenye afya bora kwa ustawi wa taifa.

Sambamba na hilo, ni kuhamasisha jamii katika masuala ya lishe inayozingatia misingi ya afya,kuushughulisha mwili mara kwa mara,kutoa mafunzo na kusimamia watumishi wa afya ya jamii pamoja na kuwaongezea uelewa wataalamu wa tiba za jadi ili kuwa na ufanisi kwa wagonjwa.

Kutokana na hali hiyo, serikali kuanzia mwaka 1973 ilizindua rasmi kampeni ya mtu ni afya lengo likiwa ni kupambana na adui maradhi na kuhakikisha wananchi wanaishi salama na kujiletea maendeleo.

“Kuanzia mwaka 1973 serikali ilianza kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti na kuboresha huduma za afya nchini na kupunguza ama kutokomeza baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza baada ya uhuru wa Tanganyika ambapo serikali iliamua kupambana na adui maradhi,umaskini na ujinga.

MAKAMU WA RAIS

Kwa mujibu wa Makamu wa rais Dkt. Philip Mpango, mwaka 1980 ugonjwa wa kisukari ulikuwa kwa kiwango cha aslimia moja ambapo kwa sasa umefikia aslimia tisa, wakati ugonjwa wa shinikizo la damu awali ulikuwa aslimia tano ukilinganisha na sasa aslimia 25, jambo ambalo ni hatari kwa afya za wananchi.

Aidha katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ambukiza, mwaka 1973 serikali ilianzisha kampeni ya Mtu ni afya ambayo pamoja na mambo mengine ilionyesha matokeo makubwa ikiwa ni pamoja na kutokomeza ugonjwa wa Ndui.

Dkt. Mpango anasema kutokana na mafanikio ya awali,serikali imeamua kuzindua awamu ya pili ya kampeni hiyo ambayo itahusisha ushiriki wa wananchi wote kwa kuzingatia mitindo bora ya maisha,kufanya mazoezi,ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni bora za usafi wa mazingira.

Kwa mujibu wa Mwongozo wa taifa wa Chakula na Ulaji, ulioandaliwa na Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la umoja wa Mataifa(FAO) unakusudia kuongeza matumizi sahihi ya Chakula mchanganyiko katika kaya,kuhamasisha kupunguza matumizi ya Chumvi,Sukari na Mafuta,Kuhamasisha usafi wa mazingira yanayotumika kuandaa chakula kwa kuboresha afya na lishe kwa jamii.

NINI KIFANYIKE

Baadhi ya wadau wa afya wanapendekeza nguvu kubwa ielekezwe kwenye elimu kwa umma,kuanzia ngazi ya kaya,kijiji,Kata,Tarafa,wilaya,mkoa na Taifa kwa Ujumla.

Vikao vya kikanuni na mikutano ya hadhara kuanzia vitongoji,vijiji,kata na wilaya viweke kipaumbele cha kuzungumzia masuala ya kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Kliniki za Baba,Mama na Mtoto zitumike kutoa elimu ya mtindo bora wa maisha ,na namna jamii inavyopaswa kujilinda dhidi ya ugonjwa wa kisukari na shinikizo la juu la damu.

Wataalamu wa afya wawezeshwe ili kuyafikia makundi hatarishi katika jamii ikiwemo, mashuleni, vilabu vya pombe,Migahawa, wauzaji wa vinywaji vyenye wingi wa sukari na msisitizo wa matumizi sahihi ya chumvi.

Wataalamu wa saikolojia na Madaktari wa Afya ya akili washirikishwe katika kampeni hiyo kwa lengo la kutoa elimu ya kuepuka msongo wa mawazo,na changamoto ya magonjwa ya akili.

Jamii ihamasishwe kulima na kutumia vyakula vya asili yakiwemo matunda na mboga za majani kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya.

“Kujali afya ya vizazi vyetu ndiyo uhakika wa kesho ya taifa letu”