Mei 15, 2024, Afisa Tarafa wa Tarafa ya Katerero iliyoko Bukoba Mkoani Kagera Bwanku M Bwanku amefika Kata ya Mikoni kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa pamoja na kusikiliza na kutatua kero ya Mwanamama Shakila Elius na aliyekuwa mumewe wa zamani.

Baada ya kusikiliza na kutatua mgogoro wa Bi. Shakila, Gavana Bwanku akiambatana na Mtendaji wa Kata ya Mikoni Bi. Anna Mwiru alifika Shule ya Sekondari Karamagi kukagua miradi miwili ya Ujenzi wa madarasa matatu na ofisi vyenye thamani ya milioni 75 pamoja na kukagua Ujenzi wa vyoo matundu 8 vya milioni 14 shuleni hapo.

Mkuu wa Shule hiyo Bwana Diocles Hanta alimpitisha kwenye miradi yote hiyo huku Gavana Bwanku akisisitiza ubora, ufanisi, thamani ya fedha na uharaka ili wanafunzi waanze kunufaika na dhamira njema ya Rais Samia kuboresha sekta ya elimu ambayo Serikali ya Rais Samia imeendelea kutoa bila malipo ambapo shule hiyo pia inapata fedha kila mwezi, kuboresha miundombinu, kuajiri walimu wapya na kadhalika.