Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa siku 90 kwa Hospitali na taasisi zote za afya kuhakikisha wanaweka miundombinu sahihi ya kuhifadhi na kuteketeza taka zitokanazo na huduma ya afya kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya mazingira na kanuni zake kwa kuacha utupaji wa taka hizo hovyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 16,2024 jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa NEMC, Hamad Kissiwa amesema ukiukwaji wa matakwa ya sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake juu ya usimamizi na utupwaji wa taka hatarishi zitokanazo na huduma ya afya unapelekea uharibu wa mazingira lakini pia kuleta maambukizi ya magonjwa mbalimbali.

Akizitaja taka hizo hatarishi zinazotokana na huduma ya afya ni pamoja na madawa yaliyotumika , taka zenye mgando wa damu, sehemu za mwili wa binadamu zilizoondolewa sababu za magonjwa mbalimbali taka zenye viambukizi vya magonjwa,vitu vyenye nchi kali na zinginezo.

“Taasisi za huduma ya afya kufuata sheria ya mazingira na kanuni zake pamoja na miongozo ya wizara ya afya tahadhari tunatoa kwa yeyote anaeyejishughulisha na shughuli hizi kuacha mara moja utupaji wa taka hizo ovyo ndani ya siku 90 kuweza kujisajili kwenye wizara husika ili kupata utaratibu mzuri wa kupata vibali maalum vya usimamizi wa taka hizo,”amesema Kissiwa.

Amesema taka hizo ni hatarishi kwa afya ya binadamu, viumbe hai na mazingira kama hazitaratibiwa na kusimamiwa ipasavyo ili kuzuia na kudhibiti athari hizo zitokanazo na taka zenye madhara zitokanazo na huduma ya afya.