Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Iringa

Waandishi wa habari nchini wameshauriwa kuripoti habari zilizo sahihi ili kuepuka taharuki ikiwemo suala la kuripoti habari za dawa na vifaa tiba ambalo lipo chini ya Mamlaka ya dawa na vifaa tiba nchini (TMDA).

Hayo yamebainishwa leo Mei 16, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba wakati akifungua kilichowakutanisha wahariri na waandishi wa habari kutoka Dodoma, Singida, Iringa na Dar es Salaam.

RC Serukamba amesema kuwa TMDA haiwezi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila ya ushirikiano wa waandishi wa habari kupitia vyombo vyao mbalimbali hapa nchini .

“TMDA haiwezi kufanyakazi peke yake bila ya ushirikiano wa vyombo vya habari, hivyo ushirikiano huo mtaweza kushirikisha wananchi na pia kuelewa matatizo yaliyopo katika jamii yanayohusiana na usalama na ubora wa bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA.

“Kutokana na ushirikiano huo mtakuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha kwamba sheria ya dawa na vifaa tiba sura 219 inatekelezwa na wadau wote kwa ufanisi.’’ amesema Serukamba.

Aidha, akitumia nukuu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu. Julius Nyerere, kuhusu kuripoti habari sahihi amesema;

‘’Raia wanahitaji taarifa sahihi na zenye kuaminika katika wakati sahihi. Vivyo hivyo kwa wafanyabiashara kwenye masoko hata na Serikali, [mwisho wa kunukuu kauli ya Nyerere aliyoitoa akizungumza na waandishi wa habari ]’’ amesema Serukamba.

Aidha, amesema kuwa, waandishi wa habari ‘leo’ mmealikwa katika kikao kazi hiki ili mkasaidie kupunguza taharuki, kwa kuhakikisha kwamba mnazingatia kupata taarifa sahihi kutoka katika vyanzo sahihi.

Hata hivyo amewapongeza TMDA katika mambo makubwa inayokabiliana nayo hususani uwepo wa dawa duni na dawa bandia.

“Ni matumaini yangu mtaweka mikakati ya pamoja juu ya kuimarisha udhibiti wake pamoja na udhibiti wa matangazo ya bidhaa husika ili wananchi wapate taarifa sahihi na kuweza kufanya uchaguzi wa bidhaa zenye usalama na ubora wa afya zao.’’ amesema Serukamba.

Aidha, Serukamba ameviomba vyombo vya habari kuelimisha umma kuachana na matumizi ya dawa duni na bandia ambazo zimekuwa zikiripotiwa uwepo wake hapa nchini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo amesema kuwa TMDA inafahamu umuhimu wa sekta ya habari nchini hivyo wataendelea kushirikiana na vyombo vya habari.

Amesema kuwa, TMDA imefanikiwa kuweka mifumo mizuri ya udhibiti wa dawa ambayo imehakikiwa na shirika la Afya Duniani (WHO).

Dk Fimbo amesema kuwa, wanafanya kazi kubwa na kwa ufanisi kwa kufuata mifumo iliyokuwepo, ambapo amesema maabara iliyopitishwa na WHO yenye hadhi ya [WHO Maturity L-3].

“Nisema tu, tunafahamu sekta ya habari ni muhimu. Na Kazi yetu kulinda afya za jamii,
Jamii kuifikia katika kuipasha habari ni pamoja na kutumia Vyombo vya habari kuwafikia wananchi wengi” amesema.

Ameongeza kuwa TMDA imekuwa ikizunguka kila Kanda kukutana katika vikao kazi hivyo na wahariri na waandishi kwa kutoa mada mbalimbali za watalaama, lakini pia kutoa tuzo kwa waandishi wa habari wanaoripoti habari za mamlaka hiyo.

By Jamhuri