Waziri wa Afya Ummy Ali Mwalimu (Mb.), amewasilisha Bungeni mpango wa Wizara na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na maeneo ya kipaumbele ambayo wizara itajielekeza nayo kwa mwaka 2024 -2025.

Sisi, ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Afya Dk Elizabeth Sanga tumeisikiliza na kuchambua bajeti ya Wizara ili kuona kwa namna gani bajeti ya Wizara ya Afya inaakisi mahitaji, matarajio na matamanio ya wananchi.
Uchambuzi wetu Umebaini.

Ufinyu wa bajeti ni tatizo linaendelea mwaka hadi mwaka, bajeti ya afya imeendela kuwa chini ya asilimia 3 ya bajeti ya taifa kwa miaka mitatu mfululizo. Mwaka 2001 nchi wanachama wa Umoja wa Afrika walisaini makubaliano ya bajeti ya afya kuwa asilimia 15 ya bajeti ya Taifa kwa nchi zao. Kwa kiasi hiki cha bajeti ya Wizara ya Afya, lengo la bajeti ya afya kufikia makubaliano ya Abuja bado ni ndoto.

Uchambuzi wetu umebaini kuwa kiwango ambacho kupokelewa bado ni ndogo sana mwaka wa fedha 2023/24 fedha za maendeleo zilizopokelewa ni asilimia 59 tu ya fedha zote zilizoidhinishwa, vilevile asilimia 41 bajeti iliyoidhinishwa mwaka 2023/24 ilitegemea fedha kutoka nje.

Hata hivyo, tunaona kuwa Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayotumika imepitwa na wakati, haiendani na Mpango mkakati wa tano wa sekta ya afya 2021/22 -2025/26.
Haya ni maeneo 10 ya uchambuzi wetu. kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Hatua za kupambana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza haziridhishi
Idadi ya watu wenye magonjwa yasiyoambukiza imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, magonjwa ya shinikizo la juu la damu na kisukari yameongoza katika idadi ya watu waliokwenda kupata matibabu kwenye vituo vya kutoa huduma za afya.

Watu wenye kisukari na shinikizo la juu la damu ni takriban asilimia 30 ya wagonjwa wote wenye magonjwa yasiyoambukiza waliofika kwenye vituo vya kutoa huduma za afya kupatiwa huduma. Magonjwa haya yanaweza kuzuilika au kutibiwa kwa gharama ndogo yanapogundulika na kutibiwa mapema.

Aidha, huduma ya uchunguzi wa magonjwa yasiyombukiza kwenye zahanati na vituo vya afya bado hairidhishi. Mfano, huduma za uchunguzi wa saratani zinazoongoza kwa wingi nchini kama saratani ya tezi dume, shingo ya uzazi na saratani ya titi haukidhi mahitaji na ni gharama kubwa kwa mwananchi mwaka 2023-24 wanawake 278406 walipata huduma ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, ambao ni asilimia 1.6 tu ya wanawake wote walio kati ya umri wa miaka 15 -64.

Pia, Asilimia 30 ya watoto wana udumavi na asilimia 59 wana upungufu wa damu, asilimia 42 ya wanawake walio kwenye umri wa kuzaa wa watu wana upungufu wa damu. Kuendelea kuwepo kwa idadi ya magonjwa sugu ya upungufu wa damu na kushindwa kutatua changamoto ya ukosefu wa lishe bora kwa watoto na kina mama wajawazito ni moja ya athari mbaya za huduma duni ya afya katika ngazi ya msingi.

Kuna gharama kubwa za kutibu magonjwa yasiyoambukiza yaliyofikia hatua mbaya, kwenye hospitali za rufaa. Kumekuwa na ongezeko kubwa la fedha inayolipwa na NHIF kugharamia magonjwa yasiyoambukiza kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kutoka Shilingi Bilioni 24.4 sawa na asilimia 12 ya fedha zote zilizolipwa na NHIF mwaka 2015/16 hadi Shilingi Bilioni 137.8 au asilimia 19 ya pesa yote iliyolipwa mwaka 2023/24. Asilimia 30 ya watoto wana udumazi na asilimia 47 wa watu wanaukosefu wa damu (anemia).

Kuendelea kuwepo kwa idadi ya magonjwa sugu ya upungufu wa damu na kushindwa kutatua changamoto ya ukosefu wa lishe bora kwa watoto na kina mama wajawazito ni moja ya athari mbaya za huduma duni ya afya katika ngazi ya msingi.

ACT Wazalendo, tunaitaka serikali iweke kipaumbele kwenye kuongeza ubora wa huduma kwenye ngazi za zahanati na vituo vya afya badala ya kuwekeza zaidi kwenye huduma za rufaa.

Upungufu mkubwa wa miundombinu ya Afya unazorotesha huduma.
Pamoja na ongezeko la ujenzi wa vituo vya huduma za afya, Idadi ya vituo vya kutoa huduma ya afya bado haikidhi mahitaji ya umma. Pia kuna upungufu wa miundombinu kama vile vitanda vya kulaza wagonjwa, vyumba vya kujifungulia wajawazito, vyoo na vifaa vya kunawia mikono, viteketezi taka, huduma za maeneo ya wagonjwa kusubiri huduma, maabara za kiuchunguzi na vyumba vya upasuaji. Pia, vituo vingi vya huduma za afya vina ukosefu wa miundominu msingi kama vile maji safi, na umeme.

Nchi yetu ina mzigo maradufu wa magonjwa, yaani magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza. Idadi ya watu wenye magonjwa yasioyoambukiza inazidi kuongezeka nchini Kwa kipindi cha July 2022 hadi March 2023, silimia 67.6 ya wagonjwa wote wa nje walienda kwenye zahanati na vituo vya afya kupatiwa matibabu. Hii inamulika umuhimu wa kugharamia mfumo bora wa huduma ya afya ya msingi kama suluhisho la kupambana na kuzuia na magonjwa yasiyoambukiza na ya kuambukiza.

Sera ya kuwa na zahanati kila Kijiji na kituo cha afya kila kata, haijatekelezwa kwa maeneo yote. Idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya afya nchini vilivyosajiliwa ni 12266. Kati ya hivyo, Hospitali ni 444 Vituo vya Afya ni 1187, Zahanati ni 8062 na kliniki ni 970, 1603 ni vituo vinginevyo, maeneo ya mijini yakiwa na vituo vingi vya kutoa huduma ya afya kuliko vijijini. Kati ya vituo 112266 vituo vinavyomilikiwa na serikali ni 7375 tu sawa na asilimia 60 ya vituo vyote, zahanati za serikali ni 5719 tu. Taarifa za serikali zinaonyesha kuna jumla kata 3956 na vijiji 12,319 nchi nzima.

Idadi iliyopo ya vituo vya huduma za afya haitoshelezi mahitaji ya watanzania. Aidha, Ripoti ya CAG ya mwaka 2022-2023 inaonyesha uchelewashaji wa kukamiika kwa ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya uliogharimu Sh bilioni 13.5, na upotevu wa takriban Sh bilioni 5 kutokana na sehemu za afya zilizokamilika lakini hazitumiki.

Gharama za kukosa huduma bora za afya kwenye ngazi ya zahanati na vituo vya afya ni kubwa, eneo la kinga ya magonjwa limeathirika kwa kiasi kikubwa na kusababisha hasara. Matumizi holela ya dawa pasipo ushauri wa wataalamu wa afya ni hatari kwa wagonjwa, mfano usugu wa dawa za antibiotiki umefikia 56%, kutokana na matumizi holela ya dawa hizo.

ACT Wazalendo tunaiitaka serikali kuongeza bajeti ya huduma za afya hasa kwenye ngazi ya zahanati na vituo vya afya. Bajeti ya sasa ya wastani wa alisema 2.5 ya bajeti ya Taifa haiendani na mahitaji ya wananchi. Pili, kuimarisha usimamizi wa fedha dhidi ya ubadhilifu. Aidha wote waliohusika na matendo ya matumizi mabaya ya fedha kama ilivyoainishwa kwenye Ripoti ya CAG wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi usiokidhi viwango
Upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya. Vituo vya kutoa huduma za afya vinaendelea kukabiliwana na uhaba wa raslimali, kama mazingira duni ya kazi, na uhaba wa dawa na vifaa tiba. Uwekezaji wa ujenzi wa vituo vya huduma za afya unapaswa kwenda sambamba na jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma ya afya kwa wananchi.

Upatikanaji wa dawa kwenye huduma za afya ngazi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za halmashauri bado hauridhishi, aidha maboresho ya upatikanaji wa dawa hayaendani na ongezeko la wafanya kazi wa afya wenye uwezo wa kutoa dawa hizo kwa wagonjwa, mfano uwepo wa aina 3 za dawa za shinikizo la juu la damu, kwenye zahanati zote lakini kuna upungufu mkubwa wa wahudumu wa afya wenye ujuzi wa kutoa hizo dawa kwa wagonjwa.Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, kuna tatizo kubwa la hospitali za Rufaa za Mikoa kununua za vifaa tiba vyenye gharama kubwabila kuvitumia kama ilivyokusudiwa, baadhi ya sababu zilizotajwa ni kukosa majengo yanayohitajika kufunga vifaa hivyo na ukosefu wa wataalamu wenye ujuzi wa kuvitumia.

Pamoja na ufinyu wa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, ripoti ya CAG kwa miaka mitatu mfululizo 2022-2023 imeonyesha hasara kubwa iliyotokana na dawa ambazo muda wa matumizi yake ulikwisha ambazo hazikuwa zimeteketezwa. Sambamba na mapungufu hayo, vifaa vya matibabu na dawa vilivyolipiwa vyenye thamani kubwa vilichelewa kupelekwa kwenye vituo vya kutoa huduma za afya,

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuongeza bajeti na usimamizi wa bajeti kwa ajili ya usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwenye vituo vya huduma za afya hasa kwenye ngazi ya hospitali za halmashauri, zahanati na vituo vya afya. Pili, kuiwezesha Bohari ya Dawa (MSD) kufanya kazi zake kwa uhuru na kuiwajibisha. Tatu, Serikali ihakikishe dawa zilizoisha muda wake zinateketezwa kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha kanuni za uagizaji na matumizi ya dawa vinazingatiwa.
Upungufu wa Watumishi wa afya katika hospitali za umma,

Uhaba wa watumishi wa afya katika vituo vya afya umekuwa ni tatizo sugu na la muda mrefu hali inayopunguza ufanisi wa wafanyakazi na kupunguza ubora wa huduma za afya kwa wananchi. Juhudi za kuongeza watumishi wa Sekta ya Afya haziendani na kasi ya ukuaji wa idadi ya watu nchini. Hadi kufikia mwezi Machi 2024, Sekta ya Afya ilikuwa na jumla ya watumishi wa afya wapatao 126,925 ambao ni sawa na asilimia 36 tu ya watumishi 348,923 wanaohitajika katika sekta ya afya. Kati yao idadi ya madaktari na wauguzi ni ndogo zaidi.

Idadi ya chini kabisa ya wafanyakazi wa afya yaani madaktari, wauguzi na wakunga waliosajiliwa inayohitajika ili kuweza kutoa huduma ya afya ya msingi kwa jamii ni wafanyakazi 2.5 kwa watu 1000. Hadi kufikia Machi, 2024, Jumla ya madaktari 39133 wamesajiliwa na Baraza la madaktari Tanganyika, ikiwa ni idadi ya madaktari 0.5 kwa kwa watu alfu moja.

Aidha kuna tatizo la mgawanyiko wa wafanyakazi wa afya, zahanati na vituo vya afya vijijini na maeneo ya pembezoni vikiwa na uwiano mdogo zaidi wa idadi ya wafanyakazi wa afya na wagonjwa kulinganisha na hospitali na vituo vya vingine vya huduma za afya vilivyopo mijini.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kutumia njia endelevu za kuandaa na kuajiri wahudumu wa afya ili kimarisha huduma za afya kwenye ngazi zote za vituo vya huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha madaktari, wauguzi na wakunga kufanya kazi kwenye maeneo ya vijijini. Pili, wahudumu wa afya wanatakiwa kupewa mafunzo ya mara kwa mara (Refresher course) ikiwemo, mafunzo ya huduma kwa wateja, mafunzo ya huduma za dharura na uwajibikaji ili kuongeza ufanisi kwenye kazi zao.

Kukosekana kwa matumizi ya mfumo wa Tehama ngazi ya afya ya msingi

Kuna tatizo kubwa la kukosekana kwa matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa rekodi za kitabibu (electronic c medical records kwa kifupi EMR) na mfumo bora wa kuthibiti taarifa za afya (health management information system yaani HMIS) kwa ujumla. Bajeti ya Tsh bilioni 2 iliyowekwa kwenye kugharamia mfumo wa TEHAMA ni ndogo sana kulinganisha na umuhimu wake.

Mfumo bora wa TEHAMA unawezesha wafanyakazi kwenye vituo vya huduma za afya kukusanya, kudhibiti na kuchanganua taarifa za wagonjwa na mahitaji yao kwa wakati, kwa usahihi na ufanisi ili kuhakikisha wanafuatilia hali zao za afya na kuwapa huduma bora.Lakini mfumo huu pia unawawezesha wasimamizi wa huduma za afya kupata taarifa sahihi mapema, za mahitaji ya wagonjwa kwenye vituo vya huduma za afya, kutathmini na kutumia taarifa hizo ili waweze kufanya maamuzi sahihi.

Mfumo wa kielektroniki unatumia gharama ndogo kuliko mfumo unaotumika sana wa kukusanya na kutunza data kwa madaftari, ambapo kila eneo la kitabibu likiwa na daftari lake yaani register mfano wagonjwa wa nje, watoto, wajawazitok, wazazi nk. Mfumo wa makarasi ni mfumo duni wenye mapungufu mengi ikiwa ni pamoja na kukosa taarifa sahihi za mahitaji ya vituo vya afya kwa muda mwafaka.

Mfumo wa kielektroniki bado haujawekwa kwenye vituo vingi vya afya nchini. Aidha, wafanyakazi wengi wa afya hawajapata mafunzo ya kutumia mfumo wa kielektroniki.

Kwa mujibu wa tafiti za hivi karibuni takribani 18% tu ya vituo vya afya ngazi ya msingi nchini vinaweza kutumia data zinazokusanya vituoni kupanga uendeshaji wa vituo na kuboresha huduma za afya. Na vituo vya afya ngazi ya msingi vyenye uwezo wa kukusanya rekodi za kitabibu zilizojitosheleza ni asilimia 9 tu. Hii ni moja ya sababu kubwa inayosababisha mfumo mbovu wa usimamizi na ukadiriaji wa mahitaji ya vituo vya afya.

Usimamizi usiofaa, unafungua milango ya ubadhirifu wa fedha mfano malimbikizo ya madeni. Adhari nyingine za kukosekana kwa mfumo bora wa kukusanya taarifa na kutoa taarifa ni kushindwa kudhibiti uendeshaji wa bima ya afya, kukosekana kwa mawasiliano ya moja kwa moja baina ya vituo vya afya na bohari ya madawa na maeneo mengine na changamoto nyingine zinazosababisha huduma duni za afya.

ACT Wazalendo, tunaitaka serikali kuondokana na mifumo ya karatasi na kuweka mifumo ya tehama kwenye vituo vyote vya afya. Serikali iongeze bajeti ya kuimarisha mfumo wa TEHAMA katika kutoa huduma za afya.

Kufilisika kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeshindwa kutatua tatizo la ugharamiaji wa bima ya afya licha ya kuwepo kwa matabaka ya uanachama wa mfuko. Mfuko huu hauna fedha za kutosha kuwahudumia wanachama wake. NHIF umekuwa ukiendeshwa kwa hasara kwa miaka takribani mitano mfululizo.

Hasara hii imetokana kukosekana kwa njia bora za kuthibiti na kuendesha mfuko na matumizi mabaya ya fedha. Serikali haijatoa maelezo yoyote kuhusu kulipa deni kubwa la sh bilioni 208 inayodaiwa na NHIF, deni hilo linasababisha mzigo mkubwa wa kifedha, deni hili ni takribani 33% ya makusanyo ya NHF kwa mwaka 2023 -2024 .

Aidha uwekezaji wa fedha za mfuko ili kuzalisha faida hauna tija. Mapato ya mfuko wa NHIF yatokanayo na uwekezaji yamepungua kutoka asilimia 9 mwaka 2022-23 hadi asilimia 5.7 mwaka 2023-24. Karibia mapato yote ya NHIF yanatokana na fedha za michango ya wanachama.

Hasara za mwaka hadi mwaka zimepelekea Serikali kuchukua hatua mbali mbali kuunusuru Mfuko, Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuondoa bima zote za gharama nafuu za VIKOA, kudhibiti huduma zinazotolewa kwa kuweka vifurushi vya kujiunga vyenye gharama na huduma zinazotofautiana, ambapo wanachama wanaolipia zaidi hupata huduma zaidi, kupandisha gharama za uanachama, kupunguza mafao kwa huduma zenye gharama kubwa kama magonjwa ya moyo, saratani, ini, sukari na huduma za operesheni za uzazi, kuzuia matumizi kwa baadhi ya hospitali na kuondoa bima ya afya ya bei nafuu kwa watoto yaani TOTO Afya.

Juhudi hizi zinapelekea kuongeza mzigo kwa mwananchi kwa kumtoza mwananchi gharama zaidi na kupunguza mafao anayopata mwananchi anapoumwa. Wananchi hawapaswi kutumika kulipa gharama za maamuzi mabovu ya Serikali.
ACT Wazalendo katika Ilani ya Chaguzi 2020 tuliahidi kuhakikisha suala changamoto za afya kuwa historia “Serikali ya ACT Wazalendo itafanya yafuatayo; Itaboresha mfuko wa Bima ya Afya kwa kuunganisha na mifumo ya Hifadhi ya Jamii, ili kila Mtanzania anapochangia hifadhi ya jamii awe anapata huduma ya Afya moja kwa moja. Kwa mfumo huu, mfuko wa Bima ya Afya utaweza pia kupata fedha kwa wakati na kulipa watoa huduma kwa wakati. Bima ya Afya ni haki ya kila Mtanzania.”

ACT wazalendo tunapendekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iwe na Fao la Matibabu, mwanachama wa Mifuko hiyo awe moja kwa moja mwanachama wa NHIF. Pili, Bodi na Menejiment yote ya NHIF ibadilishwe, Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote uandikwe upya kuzingatia mapendekezo ya ACT wazalendo na sheria mpya ya NHIF itungwe ili kuimarisha mifumo ya huduma za Afya nchini.

Mfumo usiofaa wa kugharamia huduma za afya.

Tangu Serikali ilipoanza kutekeleza sera ya uchangiaji wa huduma muhimu kama vile za Afya na Elimu kutokana na sera ya urekebishaji wa uchumi na soko huria, mwanzoni mwa miaka 1990, kumeongeza pengo kubwa la wenye nacho na wasio nacho katika kupata huduma za afya.

Upatikanaji wa huduma bora za afya kwa sehemu kubwa unategemewa na uwezo wa mwananchi kununua huduma hiyo badala ya uzito wa ugonjwa wenyewe. Jitihada za Serikali katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa usawa zinazuiwa na gharama kubwa na mifumo mibovu ya kuunganisha nguvu za wananchi ili kupanua wigo na uwezo wa Serikali kugharamia huduma.

Takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2022 zilizotolewa Juni 2023, zinaonyesha kuwa mwaka 2022 jumla ya Watanzania milioni 43 walikuwa wagonjwa kwenye Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati Nchi nzima. Hii ina maana kuwa takriban asilimia 69 ya Watanzania walihitaji huduma za afya mwaka 2022.

Na zaidi ya 70asilimia ya wagonjwa walikwenda kwenye vituo vya afya ya msingi kutafuta huduma za afya. Katika nchi ambayo huduma za afya zinahitajika kwa kiwango hiki suala la Afya linapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa sana. Kitendo cha Serikali kujiondoa kwenye kuhudumia raia wake kwenye afya kwa namna yoyote ni kuumiza wananchi wake.

Mfumo wa sasa wa ugharamiaji wa huduma za afya umeachwa kwenye mabega ya mwananchi aidha kwa kutumia pesa taslimu au kwa kupitia mfumo wa Bima ya Afya. Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya Afya, takriban asilimia 15 tu ya watanzania wote ndiyo wanaonufaika na huduma za bima ya afya.

Mfuko wa NHIF kwa sasa unahudumia asilimia 8 tu ya Watanzania wote, huku asilimia 7 wanahudumiwa na Bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa (CHF) na bima za binafsi. Hata hivyo wanachama hai wa iCHF (kaya 22,000) ni asilimia.

Wote ni mashahidi namna watu wanavyopoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu, Ndugu wa marehemu kuzuiwa kuchukua maiti katika hospitali kutokana na marehemu kuwa na deni linalotokana na gharama za matibabu. Utu wetu unafifia kutokana na kukosa mfumo wa afya wa kujaliana, kuthaminiana. Kukosekana kwa mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii umewafanya watu wengi wasiwe na uwezo wa kupata huduma za matibabu.

ACT Wazalendo tunapendekeza kwamba serikali ihakikishe kila mtanzania anakuwa kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii ili kuwawezesha wananchi wote kupata bima ya afya ya taifa. 20% ya Michango ya wanachama wa Mifuko ya hifadhi ya jamii iwasilishwe NHIF. NHIF itapata wanachama wapya milioni 1.9 na makusanyo ya bilioni 530 kwa mwaka. Pili, Serikali itumie 10% ya mapato ya ndani ya halmashauri kuwaingiza wananchi kwenye hifadhi ya jamii na NHIFkwa kuchangia theluthi ya mchango wao baada ya kujiunga na hifadhi ya jamii kwa hiyari, takribani wanachama milioni 7.4 wanaweza kujiunga na NHIF na makusanyo ya Bilioni 620. Tatu, Serikali iwalipie 100% wanufaika wa TASAF kwenye hifadhi ya jamii na NHIF.

Takribani ni watu milioni 6.3 na makusanyo ya bilioni 470. Nne ili kutekeleza mapendekezo yote hapo juu, Serikali itenge kwenye bajeti ya kila mwaka asilimia 2.5 ya Pato la Taifa kwa ajili ya kugharamia matibabu na hivyo kuwezesha wananchi milioni 11 kuwa na Bima ya Afya pamoja na wategemezi wao

Huduma kwa walipatwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto haziridhishi wala hazikidhi mahitaji ya nchi. Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi, 2024 jumla ya visa 149,081 viliripotiwa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Nchi nzima vituo vya kutolea huduma jumuishi kwa waliofanyiwa vitendo vya ukatili ni 29, idadi hii ni ndogo sana kulinganisha na mahitaji makubwa yaliyopo.

ACT Wazalendo, tunaitaka serikali iweke sera ya afya ya akili ili kuboresha na kutoa huduma bora za afya ya akili, pia serikali ifanye marekebisho ya sheria ya afya ya akili ya 2008 Pili, Wafanyakazi wote wa afya kuanzia ngazi ya zahanati wajengewe uwezo wa kutoa huduma za kitabibu na kisaikolojia, na kutoa elimu kwa jamii ili kuweza kutoa huduma za afya ya akili na elimu kwa jamii.

Tatu, Bajeti maalumu itengwe ili kuongeza huduma ya afya ya akili kwenye ngazi ya jamii. Nne, Wizara ya Afya iweke mpango mahususi wa kuboresha huduma ya afya ya akili kwa watu wazima, vijana na watoto.Tano, huduma za afya ya msingi ziboreshwe kuhakikisha huduma bora za afya ya akili na kuzuia magonjwa ya akili zinapatikana.

Hitimisho: Bajeti ya wizara ya afya kama asilimia ya pato la taifa ni ndogo na haikiidhi mahitaji ya Kupungua kwa kufikia lengo la kuwa na jamii yenye afya kwa wote. Pia, mfumo wa ugharamiaji wa afya uliopo haufai, unamtwisha mwananchi mzigo mkubwa wa ugharamiaji wa huduma za afya, ni mfumo ambao hauwezi kutufikisha kwenye lengo ya Afya kwa wote. Bajeti ya Serikali inapaswa kuweka mkazo huduma za afya kwenye ngazi ya zahanati na vituo vya afya ili kuakisi mahitaji ya wananchi katika kupata ‘haki ya afya kwa wote’.