Bondia Sherif Lawal (29) amefariki dunia akiwa hospitali akipatiwa matibabu baada ya kupigwa ngumi iliyomuangusha chini katika pambano lake dhidi ya bondia kutoka Ureno Malam Varela, lililochezwa kwenye ukumbi wa Harrow Leisure Center siku ya Jumapili.

Katika pambano hilo la raundi sita la uzito wa kati lililokuwa likichezeshwa na mwamuzi Lee Every, Lawal mwenye makazi yake nchini Uingereza alianguka raundi ya nne, ambapo madaktari waliopo eneo la tukio walimpa huduma ya kwanza na iliposhindikana alibebwa kwenye Ambulance kukimbizwa katika hospitali ya karibu ambapo baada ya muda alitangazwa kufariki dunia..

Lawal ndio alikuwa akiianza rasmi safari yake ya ngumi na pambano hilo ndio lilikuwa pambano lake la kwanza la kulipwa.

Baada ya tukio hilo bodi ya usimamizi wa ngumi nchini Uingereza imetoa taarifa hii.

“Bodi ya Udhibiti wa Ndondi ya Uingereza inatuma salamu za rambirambi kwa familia ya Sherifdeen Lawal kufuatia kifo chake cha kusikitisha baada ya pambano lake la Jumapili, Mei 12, 2024”

Pambano la Lawal ndio lilikuwa na ufunguzi kwa usiku huo na baada ya taarifa ya kifo chake mapambano yote yaliyosalia yalifutwa.

By Jamhuri