Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Watoto 10 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya upasuaji inayofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia.

Kambi hiyo ya upasuaji ya siku nne inafanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali ya Taifa ya Moyo iliyopo  jijini Lusaka.

Dkt. Godwin Sharau ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alisema katika kambi hiyo wanafanya upasuaji wa kuziba matundu ya moyo, kurekebisha valvu za moyo pamoja na kurekebisha mishipa ya damu ya moyo ambayo haijakaa katika mpangilio wake.

“Tuko nchini Zambia tangu jana tumeanza kufanya upasuaji siku ya leo, tayari tumefanya upasuaji kwa watoto wawili ambao wako katika chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU) wanaendelea na matibabu.  Hadi siku ya jumapili tunatarajia tuwe tumefanya upasuaji kwa watoto 10”, alisema Dkt. Sharau.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutusomesha wataalamu wa JKCI, kutupatia vifaa tiba vya kisasa na kutupatia mazingira rafiki ambayo yametuwezesha kufanya kazi zetu kiufasaha  na kuweza kuwasaidia nchi za jirani ambao hawajafikai hatua kama yetu ya kufanya upasuaji wa moyo”, alisema Dkt. Sharau.

Wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia wakimfanyia mtoto upasuaji wa kuziba tundu la moyo katika kambi maalumu ya upasuaji inayofanyika nchini Zambia. Watoto 10 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wanatarajia kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ya siku tatu ambayo imewezeshwa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel.

Dkt. Sharau pia alilishukuru Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel ambalo limewezesha kufanyika kwa kambi hiyo kwa kutoa vifaa tiba pamoja na kuwasafirisha wataalamu wa JKCI nchini Zambia kwenda kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto.

Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia Mudaniso Ziwa aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa  kwenda katika hospitali hiyo kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto.

“Tangu nimemaliza masomo yangu ya upasuaji wa moyo nchini Israel nimekuwa nikishirikiana na wenzangu wa JKCI kwa kujiongezea ujuzi wa kazi, mwaka jana nilikuwa JKCI kwa muda wa siku tatu kuangalia jinsi wenzangu wanavyofanya upasuaji ili siku za mbeleni nasi tuweze kufanya upasuaji wenyewe ”.

“Kufanyika kwa kambi hii kunazidi kuniongezea ujuzi wa kazi kwani najifunza zaidi, kunapunguza idadi ya watoto wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo nchini Zambia  pia kunaipunguzia Serikali gharama ya kuwapelea wagonjwa kutibiwa nje ya nchi”, alisema Dkt. Ziwa.

Wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia wakipongezana mara baada ya kumaliza kumfanyia mtoto upasuaji wa kuziba tundu la moyo katika kambi maalumu ya upasuaji inayofanyika nchini Zambia. Watoto 10 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wanatarajia kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ambayo imewezeshwa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau akizungumza na wataalamu wa Taasisi hiyo pamoja na wenzao wa hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia mara baada ya kumaliza kufanya upasuaji wa kuziba tundu la moyo wa mtoto katika kambi maalumu ya upasuaji inayofanyika nchini Zambia. Watoto 10 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wanatarajia kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ambayo imewezeshwa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel.

By Jamhuri